…………………………………………………………………………………………….
Na.Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wateule kwenda
kutatua matatizo ya wananchi katika maeneo yao.
Akizungumza katika hafla ya
kuapisha viongozi aliwateuwa hivi karibuni leo Alhamisi (Julai 16, 2020)
Ikulu, Chamwino Dodoma, Rais Magufuli aliwataka viongozi wateule kwenda
kufanyakazi, kusimamia shughuli za maendelo pamoja na kutatua matatizo
ya wananchi ikiwemo migogoro mbalimbali huku akitolea mfano mgogoro wa
ardhi wa ulipo katika Wilaya ya Chunya, jinini Mbeya.
“Mkatimize wajibu wenu na
kufanyakazi vizuri, mkamtangulize Mungu katika shughuli zenu na
mkawatumikie watanzania na hasa wananchi masikini waliopo katika maeneo
yenu,” alisema Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli alimtaka
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu
Isaac Kazi ambaye ni kati ya viongozi aliowateua kuhakikisha kuwa
hakuna urasimu katika kuwawezesha wawekezaji kutekeleza miradi yao
hapa nchini.
“Tusiwazungushe wawekezaji,
tuwavutie waje kuwekeza nchini, nchi yetu ina maeneo mbalimbali ya
uwekezaji ikiwemo Kigamboni na Kibaha, tuongeze kasi katika utendaji
wetu ili tuendelee kujenga uchumi wetu, na sasa tumeingia uchumi wa kati
basi tujitahidi zaidi” alisisitiza Rais Magufuli
Kwa upande, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliwapongeza
wateule wapya na kuwataka kuwa watumishi wa watu badala ya kuhaha na
madaraka waliyoyapata.
Viongozi walioapishwa ni pamoja na
Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa maeneo mbalimbali
na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC),ambao
waliteuliwa katika nafasi hizo hapo jana Julai 15, 2020.
Mwisho
No comments :
Post a Comment