**********************************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linamshikilia JOSEPH SHILA [29] Mwalimu Shule ya Msingi Mwakareli na
Mkazi wa Mwakareli kwa tuhuma za wizi wa fedha Tshs.Milioni 34,000,000/=
mali ya mwalimu mstaafu GIDEON NGOLAKO MWALUJOBO [60] Mkazi wa
Mwakareli.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe
30.06.2020 majira ya saa 19:00 Usiku huko Kijiji na
Kata ya Mwakareli,
Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya baada ya kupata
taarifa toka kwa msiri. Mtuhumiwa alifanikiwa kuiba pesa hizo mali ya
mwalimu mstaafu GIDEON NGOLAKO MWALUJOBO [60] Mkazi wa Mwakareli kupitia
akaunti 6140201871 kwa kutumia “NMB Mobile” katika Tawi la NMB Mbalizi
Road baada ya kupata namba ya siri ya mhanga ambaye walikuwa ni Walimu
wa Shule moja na marafiki wa siku nyingi.
Mtuhumiwa pia anajihusisha na
uwakala wa kusajili laini za simu kwa kutumia mfumo wa kisasa wa alama
za vidole ambapo aliweza kutengeneza laini ya simu kwa jina la Mhanga na
kutokana na kuaminiana na mhanga pia alikuwa ana mpa kadi yake ya Benki
kwa ajili ya kumtolea fedha.
Katika upekuzi uliofanywa nyumbani
kwa mtuhumiwa amekutwa na fedha taslimu Tshs.Milioni 20,780,000/=, Kadi
ya Benki NMB, Simu tatu [03] aina ya Tecno na laini mbili za simu.
Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika
mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
WITO WA KAMANDA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa wito kwa
wananchi kuwa makini na kadi zao za Benki ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
wanatunza namba ya siri ili kujiepusha na matukio ya wizi. Aidha
anasisitiza kuendelea kuhakiki usajili wa laini zetu kwa kubonyeza *106#
chagua 2, ingiza nambari ya kitambulisho chako cha NIDA kisha utapata
kujua kitambulisho chako kimetumika kusajili laini ngapi na endapo kuna
dosari zozote ni vyema kutoa taarifa mapema katika mamlaka husika kwa
hatua zaidi.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linawashikilia watuhumiwa watano wa familia moja 1. CHAUSIKU MAHMOD [50]
Mke wa Marehemu, 2. IDRISA ALLY [20] 3. HAWA ALLY [20] 4. SALIMA ALLY
[19] na JUMANNE ALLY [30] kwa tuhuma za mauaji ya ALLY HAMIS @ MAZINGE
[66] Mkazi wa Ubaruku.
Tukio hili limetokea mnamo
tarehe 26.06.2020 majira ya saa 00:40 Usiku huko Kitongoji cha Mbuyuni
kilichopo Kijiji cha Mpakani, Kata ya Ubaruku, Tarafa ya Rujewa, Wilaya
ya Mbarali. Mkoa wa Mbeya ambapo watuhumiwa walimvizia marehemu akiwa
amelala kisha kumkata kwa panga sehemu ya shavu la kulia na kidevuni.
Chanzo cha tukio ni tamaa ya
mali kwani mke na watoto wa marehemu walipanga kuuza eneo wanaloishi
ambalo mnunuzi alipanga kujenga “Filling Station” lakini wakati wa uhai
wake marehemu aliwakatalia kuuza eneo hilo kwa sababu sehemu ya eneo
hilo kuna nyumba ambayo wanaishi hivyo marehemu alionekana ni kikwazo
katika mipango yao. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya
kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
WITO WA KAMANDA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI kwa jamii kuacha
tamaa ya mali ambayo kwa kiasi kikubwa husababisha mauaji ya watu wasio
kuwa na hatia na badala yake watafute mali kwa kufanya kazi
itakayowasaidia kujipatia kipato halali. Jeshi la Polisi halitasita
kumchukulia hatua za kisheria mtu, watu au kikundi cha watu
kitakachojihusisha na uhalifu wa aina yoyote.
Aidha anatoa rai kwa wananchi
kuendelea kulipa ushirikiano Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kutoa
taarifa za uhalifu na wahalifu pia kuwapa ushirikiano Polisi Kata
waliopo katika maeneo yao ili tuweze kutokomeza uhalifu na matukio yote
ambayo ni kero kwa jamii.
TAARIFA YA KIFO CHIMALA.
Mnamo tarehe 25.03.2020 majira ya
saa 07:00 Asubuhi huko Chimala, Wilaya ya Mbarali na Mkoa wa Mbeya,
TULIZO KONGA [34] Mkazi wa Chimala alifariki dunia nyumbani mnamo tarehe
27.03.2020 alizikwa katika makabuli ya Chimala na mazishi hayo
yalihudhuriwa na ndugu wa pande zote mbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Daktari wa Hospitali ya Mission Chimala ilieleza kuwa marehemu alikuwa
na tatizo la kiafya kwani alikuwa na uvimbe kichwani na walishampeleka
Hospitali ya Mission Ikonda na baadae Hospitali ya Taifa Muhimbili na
alitakiwa kufanyiwa upasuaji lakini ndugu wa marehemu walikataa kwa
kuogopa angepoteza Maisha. Pia kutokana na tatizo hilo alikuwa amepata
ugonjwa wa kifafa na hivyo tangu Madaktari waamue afanyiwe upasuaji
marehemu hakuwahi kupata tiba ya upasuaji hadi mauti yanamkuta.
Baada ya wiki mbili kupita
walifika Kituo cha Polisi Chimala kutoa malalamiko yako kwamba 1.
Hawakujulishwa marehemu pindi anaugua 2. Marehemu alipofikishwa
Hospitali ya Mission Chimala hawakupata fursa ya kumuona mpaka
walipoambiwa na Daktari kuwa amefariki 3. Wakati wa kuchukua mwili wa
marehemu kutoka Chumba cha kuhifadhiwa maiti Hospitali ya Meta
hawakushirikishwa kumuandaa wala hawakumuona 4. Wakati wa mazishi
hapakuwa na ratiba ya kuaga mwili hivyo hawakumuona na wala hawakuwa na
uhakika kama aliyezikwa ndiyo marehemu ndugu yao. Hivyo kwa ujumla
walikuwa na mashaka na kifo cha ndugu yao.
Polisi tulifanya uchunguzi wa
awali na hatimaye tuliwasiliana na Mkuu wa Mashtaka Mkoa kwa ajili ya
kupata Amri ya Mahakama ya kufukua mwili. Baada ya amri ya Mahakama
kutolewa, tulimuandaa Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Vifo [PATHOLOGIST]
Dkt.Muller wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Mnamo tarehe 30.06.2020 majira ya
saa 16:00 jioni huko katika makabuli yaliyopo Kijiji cha Igumbilo
lilifanyika zoezi la kufukua mwili wa marehemu kwa kushirikiana na ndugu
wa marehemu, uongozi wa serikali ya Kijiji, Daktari Bingwa wa Uchunguzi
wa Vifo Dkt Muller na Jeshi la Polisi.
Baada ya kufukua mwili huo, ndugu
wa marehemu walipata fursa ya kuuona na kuutambua na baadae uchunguzi wa
kina ulienda kufanyika Hospitali ya Mission Chimala akiwemo Daktari
kutoka upande wa ndugu wa marehemu. Pia katika uchunguzi huo kuna
sampuli zilizochukuliwa na kupelekwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
Kanda ya Nyanda za Juu kwa uchunguzi zaidi.
Kwa sasa tunasubiri majibu ya
kitaalamu kutoka kwa Daktari Bingwa aliyefanya uchunguzi huo na majibu
kutoka Maabara ya Mkemi Mkuu wa Serikali kutokana na sampuli
zilizopelekwa.
WITO WA KAMANDA.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI anatoa wito kwa
ndugu wa marehemu na jamii kwa ujumla kuwa watulivu wakati tunasubiri
majibu ya kitaalamu kutoka kwa Daktari Bingwa aliyefanya uchunguzi huo
na majibu kutoka Maabara ya Mkemi Mkuu wa Serikali ili haki iweze
kutendeka.
No comments :
Post a Comment