*********************************
Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewapongeza na kuwashukuru
wanahabari na wasanii wote nchini kwa uzalendo waliouonesha katika
kipindi chote cha maombolezo ya kitaifa ya Hayati Benjamin William
Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ambaye alizikwa kijijini kwake Lupaso, Masasi jana.
Akitoa tathmini yake kuhusu
maombolezo hayo ya kitaifa mjini Lindi leo, Dkt. Mwakyembe amesema kazi
walizofanya wanahabari na wasanii kuelezea wasifu wa marehemu, mchango
wake kitaifa na kimataifa kwa njia ya makala, vipindi maalum, mahojiano
mbalimbali na tungo za kufariji, kuliwaza na kupeana moyo, zimeyabeba
maombolezo yetu ya kitaifa.
“nimefurahishwa sana na
kujitoa kwenu kwa hakika mmeonesha uzalendo wa juu sana kwa taifa letu
,naomba muendelee na moyo huo huo ili kuwa na taifa lenye wasanii na
waandishi wa habari wenye umoja: Dkt. Mwakyembe
Aidha Dkt. Mwakyembe alizidi
kufafanua kuwa kwa hakika wasanii na wanahabari wametekeleza jukumu
walilokuwa nalo bila kuelekezwa, kusukumwa wala kusimamiwa bali kwa
kujituma na kusukumwa na dhamira ya utaifa na uzalendo.
“Ndiyo maana katika hotuba
zake zote kuhusiana na msiba huu, Mheshimiwa Rais hajaacha kutambua
mchango mkubwa wa wanahabari na wasanii katika kuliunganisha Taifa
kipindi hiki kigumu cha majonzi ,hongereni sna wasanii na wanahabari
tembeeni kifua mbele, mmetekeleza wajibu wenu kikamilifu kama
Watanzania” alisema Dkt. Mwakyembe.
No comments :
Post a Comment