Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekagua miradi
ya elimu inayotekelezwa katika Halmashauri ya Kasulu mkoani Kigoma yenye
thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 13.
Miradi
hiyo ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi
Kasulu, Chuo cha Ualimu Kabanga na jengo la Utawala la shule ya
Sekondari Grand.
Akizungumzia
maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga mara baada ya kukagua,
Waziri Ndalichako amesema chuo hicho kinajengewa upya miundombinu yote
baada ya ile ya awali kuchakaa sana na kushindwa kukarabatiwa.
Ameongeza
kuwa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho unagharimu zaidi ya bilioni
10, na kuwa utakapokamilika utabadili taswira ya mji huo kwa kuwa
majengo yanayojengwa ni ya kisasa na imara ambayo yatadumu kwa muda
mrefu.
Akizungumzia
mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala na utengenezaji wa mfumo wa
maji katika shule ya sekondari ya Grand, Profesa Ndalichako amesema
umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 534 na kwamba utakapokamilika
utaongeza morali ya walimu kufundisha na kusaidia wanafunzi waliopo
katika shule hiyo.
Mradi
mwingine uliotembelewa na Waziri wa Elimu ni ujenzi wa Chuo cha Ufundi
Stadi cha wilaya ya Kasulu ambao upo katika hatua za mwisho ambao
umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.97. Jumla ya majengo 15
yatajengwa na kitachukua wanafunzi 320 watakaokuwa wakilala chuoni
hapo.
Waziri
Ndalicahko amewataka wananchi wa wilaya ya Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa
ujumla kutumia fursa ya kuwepo kwa vyuo mbalimbali katika Halmashauri
hiyo kujipatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa ama kujiajiri
ili kujiletea maendeleo binafsi na ya mkoa wa Kigoma.
Mkuu
wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange ameishukuru Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia kwa namna ilivyojikita katika kupanua wigo wa
elimu. Amesema kuwa katika wilaya yake kuna maeneo ambayo ni ya wafugaji
na watoto hawakuwa wakienda shule lakini kwa sasa zimejengwa shule
shikizi katika maeneo hayo ya mbali hivyo kuwezesha watoto kusoma na
kuleta matokeo chanya.
Kanali
Anange amesema baada ya Serikali kutekeleza Sera ya Elimu bila ada
kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi, hivyo kupelekea Serikali
kupanua miundombinu katika ngazi zote za elimu ili kuwezesha fursa za
masomo kwa wanafunzi ikiwemo na kuongeza walimu.
Aliongeza
kuwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu itawezesha
vijana wa Kitanzania kupata elimu katika mazingira bora.
Naye
Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji wa Elimu ya Ualimu (TESP), Ignas Chonya
amesema ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Kabanga awamu ya
kwanza unatarajiwa kukamilika Oktoba 2020 na chuo kitakuwa na uwezo wa
kuchukua wanachuo 400 kwa wakati mmoja na kwamba chuo kinatarajiwa
kuanza mafunzo mwaka huu.
No comments :
Post a Comment