Na Josephine Majura, Peter Haule-KIGOMA
WAZIRI
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), ameuagiza
uongozi wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kutafuta eneo jipya, kubwa,
lenye hadhi ya kujengwa soko la Kimataifa badala ya eneo linapojengwa
Soko la Kimkakati la Kimataifa la Mnanila, lililoko katika mpaka wa
Burundi na Tanzania.
Maagizo
hayo ameyatoa wakati alipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa soko
hilo la Kimkakati la Kimataifa akiwa katika ziara ya kikazi mkoani
Kigoma kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatiwa
fedha na Serikali.
Dkt.
Mpango alisema kuwa hajaridhishwa na ubora wa ujenzi wa soko hilo
ambalo linatarajiwa kuwa la kimataifa kutokana na kujengwa katika eneo
dogo, na ujenzi wake uko chini ya kiwango ikilinganishwa na kiasi cha
shilingi bilioni 1.3 kilichotumika kujenga miundombinu ya mradi huo
uliolenga kuchochea shughuli za biashara na kiuchumi kati ya wananchi wa
Tanzania na Burundi.
Alisema
kuwa atatuma timu ya wataalamu kuchunguza na kufanya ukaguzi maalaum
ili kubaini watu waliohusika kushauri soko hilo lijengwe katika eneo
lisilokuwa na hadhi pamoja na kuchunguza matumizi ya fedha za mradi huo
zilivyotumika.
Aidha,
Dkt. Mpango alisema iwapo utabainika udanganyifu wa matumizi ya fedha
hizo hatua kali zitachukuliwa na kwa kuanzia ataanza na ofisini kwake
kujua vigezo vilivyotumiwa na wataalam wake walioishauri Wizara
iidhinishe matumizi ya kiasi hicho cha fedha huku wakijua kuwa eneo
linalojengwa mradi huo halina sifa ya kujengwa miundombinu
“Mtafute
eneo lingine tofauti ambalo linaweza kweli kubeba dhana ya Soko La
kimataifa ili tukuze biashara na wananchi wetu wapate kipato na
Halmashauri iweze kulipa na kugharamia maendeleo ya nchi yetu lakini kwa
mawazo madogo hivi hatuta sogea” alisema Dkt. Mpango.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina, amesema
atashughulikia kwa haraka dosari zilizobainika katika ujenzi wa Soko la
Mnanila. Ambalo malengo yake ni kuboresha maisha ya wananchi na
kuongeza kipato cha Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe na mkoa wa Kigoma
kwa ujumla ili iweze kujitegemea.
Naye
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilayaya Buhigwe Bw. Anosta Nyamwoga,
alimuahidi Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango
(Mb), kwamba Halmashauri yake itatafuta eneo jipya kwa ajili ya ujenzi
wa soko kubwa la kimataifa kwa haraka.
Awali,
baadhi ya wakazi wa Kata ya Mnanila, akiwemo Bw. Amon Ndabita,
walieleza kutoridhishwa na ujenzi wa soko hilo na kwamba
hawajashirikishwa katika kupendekeza eneo linalofaa kwa ujenzi wa soko
hilo la kimkakati la kimataifa ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu
shilingi bilioni 2.3 zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na
Mipango chini ya radi wa kuziwezesha Halmashauri kujitegemea kimapato.
Katika
hatua nyingine, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Dkt. Philip Isdor
Mpango (Mb) alimpa muda wa siku 15 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma Bw. Anosta Nyamwoga, kuwalipa
mamalishe, vibarua, mafundi waliojenga Soko hilo la Kimkakati la
Kimataifa Munanila ambao wamelalamika mbele yake kutolipwa fedha zao
tangu mwezi Julai mwaka 2019.
“Nakuagiza
uwalipe fedha zao zote wanazodai na utajua utakako zitoa fedha hizo,
uwalipe na wewe utawadai wakandarasi wakulipe fedha zako kwani ulitakiwa
kuhakikisha wananchi hawa wanapata haki zao” alisisitiza Dkt. Mpango
Dkt.
Mpango yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma kukagua miradi ya
maendeleo inayopewa fedha na Serikali ambapo ametembelea Miradi ya
Ujenzi wa Kituo cha Afya Munzeze, Ujenzi wa Jengo la Mkuu wa Wilaya ya
Buhigwe, Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe na Ujenzi wa Soko la Kimkakati
la Kimataifa Mnanila.
Mwisho
No comments :
Post a Comment