Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (kushoto), akiangalia namba ya gari la shule ya
Sekondari ya Bwawani Mkoani Pwani inayomilikiwa na Jeshi la Magereza
kusajiliwa kwa namba binafsi badala ya Serikali. Alishangaa magari hayo
na kuagiza kupewa taarifa kwanini magari matatu ya shule hiyo yasajiliwe
kwa namba hizo. Kulia ni Mkuu wa Gereza la Mifugo Ubena, ACP Daimu
Mmolosha. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto),
akiingia jengo la Utawala la Gereza la Mifugo Ubena Bwawani leo kwa
ajili ya kufanya ukaguzi na kuangalia utendaji kazi wa viongozi wa
Gereza hilo. Kulia ni Mkuu wa Gereza hilo, ACP Daimu Mmolosha. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (kushoto), akiangalia ng’ombe wanaofugwa na Gereza
la Mifugo Ubena, Bwawani, Mkoa wa Pwani, leo, kabla ya kutolewa kwenda
machungani. Waziri huyo aliwataka viongozi wa Magereza kufanya biashara
ya maziwa na pia kuchinja ng’ombe na kutafuta soko ndani ya eneo hilo na
pia kusafirisha ili kupambana na soko kama wanavyofanya taasisi zingine
za Serikali. Wapili kulia ni Mkuu wa Gereza la Mifugo Ubena, ACP Daimu
Mmolosha. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (kushoto), akisoma taarifa aliyopewa na Makamu
Mwenyekiti wa Shule ya Sekondari Bwawani, Mkoani Pwani, alipofanya ziara
ya kushtukiza katika shule hiyo, leo. Pia alishangaa magari matatu ya
shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza kusajiliwa kwa namba
binafsi badala ya Serikali na alitoa siku moja aletewe ofisini kwake
taarifa ya maandishi kuhusiana na magari hayo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akiondoka na gari yake
katika shule ya Sekondari Bwawani ya Jeshi la Magereza iliyopo Mkoani
Pwani, leo, baada ya
kumaliza ziara yake shuleni hapo. Waziri huyo
alishangaa magari matatu ya shule hiyo kusajiliwa kwa namba binafsi
badala ya Serikali. Aliagiza kupewa taarifa kwanini magari hayo
yasajiliwe kwa namba hizo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
********************************
Na Mwandishi Wetu, Pwani.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene amefanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya
Sekondari Bwawani ambayo inamilikiwa na Jeshi la Magereza na kubaini
madudu ikiwemo magari ya Jeshi yamesajiliwa kwa namba binafsi.
Waziri Simbachawene alianza ziara
yake kwa kutembelea Gereza la Kilimo Ubena na baadaye kuelekea katika
shule hiyo ambazo zote zipo jirani ndani ya Kata ya Bwawani Mkoani
Pwani.
Akizungumza na uongozi wa shule
hiyo, Simbachawene alisema Sekondari hiyo ni mali ya umma lazima mali za
shule hizo zisajiliwe kwa namba za Jeshi la Magereza zinazojulikana kwa
kifupisho cha MT (Magereza Tanzania).
Alisema haiwezekani magari matatu
ikiwemo ya Mkuu wa Shule hiyo imesajiliwa kwa namba binafsi, lori pamoja
na gari lingine mali ya shule hiyo, kitendo hicho ni uvunjifu wa
taratibu za serikali na anahitaji kupewa taarifa ya maandishi.
“Mkuu wa Gereza Ubena wewe ndio
kiongozi hapa, nakuagiza umfikishie ujumbe CGP (Kamishna Jenerali wa
Magereza), ifikapo kesho mchana nipate taarifa ya shule hii ikiwemo
kwanini magari ya Jeshi yamesajiliwa kwa namba ‘private’ (binafsi), na
pia nipate CV za walimu wa shule hii pamoja na watumishi wote,” alisema
Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “inawezekana shule
hii ikawa nikijiwe fulani ambacho watu wanajipatia fedha, mpaka magari
wanasajili kwa namba private ili wafanyie nini?, gari la serikali
tunajua hata kama itakua inasomba mawe, lakini sio ajabu hiyo gari
inafanya kibarua huko mtaani inafanya vibarua vya watu, inabeba
matofali, unaitofautisha vipi na magari mengine, siwezi kuhukumu moja
kwa moja naomba nipate taarifa ya maandishi kutoka kwa CGP kupitia
kwako.”
Waziri Simbachawene kutokana na
mapungufu hayo aliyoyaona, alitaka kujua zaidi ufaulu wa wanafunzi
wanamaliza masomo yao, pia alitaka kujua mapato na matumizi ya shule
hiyo ambayo amesema inamazingira mazuri, eneo zuri lakini uongozi
umeshindwa kuiitangaza na haina umaarufu wowote hapa nchini.
Kwa upande wake Makamo Mkuu wa
Shule hiyo, Solomon Mwambingu alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1981,
na kuhusu ufaulu inafanya vizuri kuanzia kidato cha nne hadi cha sita.
“Shule inafanya vizuri kitaaluma,
matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka jana 2019 wanafunzi wote walifaulu,
pia kidato cha nne walifanya vizuri na matokeo ya kidato cha sita
wanafunzi wote walifaulu na hakukua na hakukua na daraja zero wala
daraja la nne,” alisema Mwambingu.
Aidha, Waziri Simbachawene kwa
upande wa Gereza la Mifugo aliwapongeza kwa kutunza mifugo iliyopo
katika gereza hilo, na kuwataka kuwepo na soko la nyama kwa kuchinja
ng’ombe ili waweze kuuza na kupata mapato kupitia ufugaji wa kuvuna.
“Lazima magereza ijitegemee,
gereza la mifugo halina hata nyama za kuuza, tunataka uchungaji wenye
faida, kuwepo na ‘brandy’ yenu, mnaweza mkachukua mfuko mkaweka nyama na
kuandika bwawani meat, na pia kuzalisha maziwa yakutosha, hivyo ndivyo
kujitangaza,” alisema Simbachawene.
Pia aliwataka aliagiza kuwa,
mifugo mbalimbali ng’ombe zichinjwe na nyama ziweze kutangazwa kwa kuwa
na utambulisho maalumu ili kuliletea mapato Jeshi hilo kwa kuwa wana
eneo hilo.
Kwa upande wake Msimamizi wa
Shamba la Magereza katika Gereza hilo, Charles Masuka alisema shamba
hilo lina ekari 12 ambapo wanafuga ngombe, mbuzi, kondoo na bata, hivyo
shamba hilo linatoa ngombe wa nyama ambapo wanatoa kwa wahitaji.
“Tunashukuru kiongozi kwa
kututembelea, ujuoio wake umetupa hamasa, na shmaba hili ni kubwa lina
mifugo 2,335, shmaba hili linategemewa utoaji wa ngomnbe wa nyamba,”
Masuka.
Simbachawene alimaliza ziara yake
ya siku moja katika Gereza hilo, na aliwataka viongozi wa Gereza hilo
wampe ushirikiano Mkuu wa Jeshi hilo, kwa kuwa na mipango mizuri ya
kulipeleka mbele Jeshi hilo, na aliwataka waendelee kuchapa kazi zaidi
pamoja na kuhakikisha wanajitegemea kwa chakula ili Magereza nchini
yaweze kusonga mbele.
No comments :
Post a Comment