Thursday, June 4, 2020

Wakulima wapewa mbinu ya kupata masoko ya uhakika

NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe. Picha ya Maktaba Na Mwandishi Wetu, Bahi
NAIBU Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, ametoa wito kwa wakulima nchini kutumia Ushirika hususani Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala kwa lengo la kupata masoko na bei za uhakika.
Wito huo umetolewa wakati wa kikao na viongozi wa Skimu ya Umwagiliaji ya wakulima wa zao la
Mpunga wa Bonde la Bahi Juzi alipokuwa katika ziara ya kikazi Wilayani Bahi, mkoani Dodoma.
Alisisitiza  kwamba Serikali ina dhamira ya dhati ya kumuinua mkulima ili anufaike na kilimo chake. “Hivyo ni vyema wakulima wakatumia mifumo ya Ushirika pamoja na vituo vya ukusanyaji mazao katika maeneo yao kwa ajili ya urahisi wa kufikisha mazao yao katika maghala ya uuzaji kwa ajili ya kupata bei yenye tija itakayopatikana kupitia minada rasmi,”amesema.
Aidha, Naibu Waziri alitoa agizo kwa watendaji kushirikiana na wakulima wa Skimu ya Bahi kujenga Ofisi ya kuhudumia Skimu hiyo ndani ya eneo la Skimu kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wakulima na kuboresha kilimo cha umwagiliaji kinachofanyika hivi sasa.
Amesema kuwa ni matazamio ya Serikali kuwa suala hilo litakapotekelezwa kwa ufanisi ni dhahiri kuwa litakuwa ni mfano  wa kuigwa katika maeneo mengine ya Skimu kama hiyo.
Ameongeza kuwa ofisi hiyo itasaidia wakulima kupata huduma kwa urahisi kupitia Afisa Kilimo, Afisa Ushirika pamoja na Wataalamu wengine ambao watapatikana katika miradi hiyo.
Naibu Waziri Bashe aliwashauri wakulima kutumia nguvu zao kwa pamoja kuboresha mifumo ya Kilimo waliyonayo ili kuongeza tija na ufanisi zaidi katika Kilimo na amewataka wakulima kuchangia maendeleo yao wenyewe kupitia maamuzi yao ya pamoja ya kuchangia kiasi cha mavuno yao kulingana na uzalishaji wa mkulima na kuuza mazao hayo kwa malengo ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Changamoto hizo ni pamoja na ujenzi wa maghala, kuboresha na kukarabati miundo mbinu ya Skimu za Kilimo.
“Tunaweza kuamua kuhifadhi kwenye ghala gunia mbili za mazao ya mkulima hiki kikiwa ni wastani wa kiwango cha chini na kwa pamoja tukaamua kuyauza mazao hayo kwa mnada wa uwazi ambapo mapato yatakayopatikana yatusaidie wenyewe kuimarisha kilimo chetu,” amesisitiza Bashe.
Katika Kikao hicho Naibu Waziri aliwaagiza viongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Bahi kutenga maeneo maalum ya uuzaji wa mazao ya wakulima wadogo wadogo ili kuwa na urahisi kukutana na wauzaji katika hatua za soko la awali, akisisitiza maeneo hayo kuwa na mizani zilizokaguliwa ili wakulima wauze kwa vipimo sahihi na si vinginevyo.
Bashe amewataka viongozi wa Skimu, viongozi wa Wilaya ya Bahi kushirikiana kwa pamoja na wadau wa maendeleo pamoja na taasisi za kifedha kuangalia namna bora ya kuongeza thamani ya mpunga huo kwa kuanzisha kiwanda chenye kinu cha kukoboa mpunga na hatimaye kuuza mchele.
Jambo ambalo wakulima hao waliliunga mkono kutokana na kuongeza ubora wa thamani na kuongeza kipato kwa wakulima.
Pamoja na mambo mengine, Naibu Waziri ameagiza watendaji wa Wilaya ya Bahi kwa kushirikiana na Serikali kuratibu zoezi la kuwatambua wakulima kwa lengo la kuanzisha kanzidata ya wakulima pamoja na upatikanaji wa vitambulisho kwa wakulima wa Bonde la mpunga la Bahi.
Akifafanua kuwa Skimu hiyo ikawa ni mfano utakaoendelezwa katika maeneo mengine ili kuongeza tija na ufanisi kwa wakulima.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemshukuru Naibu Waziri wa Kilimo kwa kufika katika Wilaya hiyo kuona shughuli mbalimbali za Kilimo zinazoendelea wilayani hapo.
Mkuu huyo amepongeza juhudi zinazoendelea hususani za uimarishaji wa Ushirika kwa mfumo wa Stakabadhi ya ghala ambao unaendelea kutekelezwa Wilayani hapo kipindi hiki ambapo minada ya mazao ikiendelea na wananchi wakinufaika na bei za mauzo za minada hiyo.

No comments :

Post a Comment