*********************************
Na WAJMW-DOM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema
ugonjwa wa
Corona unaelekea kuisha nchini ambapo mikoa zaidi ya 15 haijaripoti
mgonjwa yeyote wa Corona kwa zaidi ya wiki.
Waziri Ummy amesema hayo leo
wakati alipotembelea kituo cha afya cha Mkonze kilichotengwa kwa ajili
ya kuwahudumia watu waliopata maambukizi ya ugonjwa wa Corona jijini
Dodoma na kukuta vitanda vikiwa tupu bila kuwa na mgonjwa yeyote kwa
zaidi ya wiki.
Waziri Ummy amesema kupitia
Waganga wakuu wa Mikoa 15 nchini wamethibitisha kutokua na mgonjwa wa
Corona na Mikoa mingine yenye wagonjwa imeripoti kuwa wagonjwa hao
wanaendelea vizuri.
Aidha, Waziri Ummy amewashukuru
watoa huduma za afya wa kituo cha Mkonze kwa kazi nzuri walioifanya ya
kuwahudumia wagonjwa na kuchukua tahadhari zilizosaidia wahudumu hao
kutopata maambukizi ya Corona.
Pamoja na hayo Waziri Ummy amesema
licha ya ugonjwa wa Corona kuelekea kumalizika nchini, amewataka
wananchi kutobweteka na kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia
maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono mara
kwa mara kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kuvaa barakoa za vitambaa
wanapokua kwenye mikusanyiko
No comments :
Post a Comment