Rais wa Burundi , Evariste
Ndayishimiye akizungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais Mstaafu
wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwenye Ikulu ya Gitega nchini Burundi
baada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Marehemu Pierre
Nkurunziza Juni, 26,2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete wakizungumza na Makamu
wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombaza wakati walipowasili kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Bujumbura na baadae walisafiri kwenda Getega
kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, Juni
26, 2020.
Rais wa Burundi Evariste
Ndayishimiye (wa tatu kulia ) akiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwenye uwanja wa Ingoma
uliopo Gitega kabla ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre
Nkurunziza, Juni 26, 2020. Wengine pichani kutoka kushoto ni Mama Salma
Kikwete, Mjane wa Marehemu Nkurunziza, Denise Nkurunziza na Mke wa Rais
wa Burundi Angeline Ndayubaha.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete wakitoa heshima baada ya
kuweka mashada ya maua kwenye kaburi la aliyekuwa Rais wa Burundi,
Pierre Nkurunziza katika mazishi yaliyofanyika Gitega nchini Burundi,
Juni 26, 2020. Wa pili kushoto ni Mama Salma Kikwete na wa Nne kushoto
ni Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Elibariki Maleko
Rais wa Burundi akiagana na Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya mazungumzo yao kwenye Ikulu ya Gitega
ambako alihudhuria mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre
Nkurunziza.
Rais wa Burundi, Evariste
Ndayishimiye akimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati
alipozungumza kabla ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Burundi, Pierre,
Nkurunziza yaliyofanyika Gitega, Juni 26, 2020. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU,
Kasim Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kuisaidia nchi ya Burundi ili
ifanikiwe katika adhma yake ya kutaka kuwa mwanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama ilivyoombwa na aliyekuwa Rais wa
nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza wakati wa uhai wake .
Waziri Mkuu
aliyasema hayo jana (Ijumaa, Juni 26, 2020) alipozungumza kabla ya
mazishi ya Rais Nkurunziza yaliyofanyika kwenye uwanja wa Ingoma uliopo
Gitega nchini Burundi, Mheshimiwa Majaliwa alisema ameshiriki mazishi
hayo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Marehemu
Rais Pierre Nkurunziza alitamani sana kukabidhi madaraka huku akiwa
ametimiza kiu yake ya kutaka Burundi iwe mwanachama wa SADC jambo ambalo
halikuwezekana naamini Mheshimiwa Rais utalisimamia suala hilo
hadi litimie”.
Alisema Rais
Dkt. Magufuli amemtuma afikishe salamu za pole kwa mke na familia ya
marehemu, Rais wa Burundi na wananchi wote kufuatia kifo cha aliyekuwa
Rais wa nchi hiyo marehemu Pierre Nkurunziza kilichotokea Juni 9, 2020.
Waziri Mkuu
alisema Tanzania na Burundi ni ndugu na anaamini undugu na mshikamano
huo utaendelea kuwepo hata baada ya kifo cha Rais Nkurunziza ambaye
alitoa mchango mkubwa katika kuuimarisha mshikamao huo.
Alitumia
fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Burundi kumpa ushirikiano Rais wao mpya
Evariste Ndayishimiye kama walivyofanya kwa marehemu Nkurunziza ili
aweze kuliongoza Taifa hilo vizuri.
Naye, Rais wa
Burundi, Ndayishimiye alisema Serikali yake itayaenzi na kuyaendeleza
mema yote yaliyofanywa na Marehemu Nkurunziza na aliwashukuru viongozi
wote kutoka nje ya nchi yake ambao walishiriki katika mazishi hayo.
Mazishi hayo
pia yalihudhuriwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete,
mkewe Mama Salma Kikwete na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Alipowasili
kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura jana asubuhi Juni 26,
2020, Mheshimiwa Majaliwa alipokelewa na Waziri Mkuu wa Burundi, Prosper
Bazombaza.
Baada ya mazishi hayo Mheshimiwa Majaliwa alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Burundi kabla ya kurejea nyumbani.
No comments :
Post a Comment