Monday, June 1, 2020

Serikali yaziunganisha TPB, TIB kuongeza Ufanisi


Na Immaculate Makilika, MAELEZO
SERIKALI imeziunganisha benki zake mbili za biashara, Benki ya Posta Tanzania (TPB Bank Plc) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB Corporate Limited) ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma ikiwemo kuunganisha taasisi zinazotekeleza majukumu yanayofanana, ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
“Kwa muktadha huu, Serikali imeamua kuunganisha benki zake mbili za biashara, yaani Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate kuanzia Juni 1 2020.
Kwa hatua ya awali, Benki ya TPB itachukua mali na madeni ya Benki ya TIB Corporate na muunganiko huu utafanya benki kuwa na mali takribani trilioni moja”, amesema Mbuttuka.
Amefafanua Mbuttuka, Serikali imechukua uamuzi huu kwa lengo la kuboresha utendaji wa benki inazozimiliki ili kuwa na benki moja ya biashara ambayo ni imara.
Aidha, amesema muungano huu unalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiutendajii, kimfumo, kimuundo, na kitaswira ili benki hii iweze kuhimili ushindani wa kibiashara kwenye sekta ya
fedha.
“Muunganiko huo hautakuwa na athari katika huduma za kibenki, wala hakuna mfanyakazi atakayepoteza ajira. Aidha, Serikali inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kuhakikisha utendaji wa benki zake unaimarika na maslahi ya wenye amana na wateja wote yanalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu za usimamizi wa benki na taasisi za fedha”, amesema Mbuttuka.
Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, wateja wote wa Benki ya TPB na Benki ya TIB Corporate wataendelea kuhudumiwa kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo.

No comments :

Post a Comment