Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerlai mstaafu Nicodemus Mwengela
wakiangalia ramani ya mkoa wa Songwe wakati wa hafla ya uzinduzi ofisi
ya ardhi mkoa wa Songwe jana. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Wilson
Ruge.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikata utepe kuzindua ofisi ya
ardhi mkoa wa Songwe jana. Wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Songwe
Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemus Mwengela na kulia ni Kamishna
Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Songwe Suma Mwakasitu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati ya ardhi mkazi
wa Songwe Bi. Mary Shaurini wakati wa hafla ya uzinduzi ofisi za ardhi
mkoa wa Songwe jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali
mstaafu Nicodemus Mwengela.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na
wananchi wa mkoa wa Songwe waliokabidhiwa hati zao za ardhi jana. Wa
pili kulia Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemus
Mwengela.
(PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
************************************
Na Munir Shemweta, WANMM SONGWE
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka
halmashauri nchini kutumia ramani zilizoandaliwa na kutolewa na Wizara
ya Ardhi kupitia idara yake ya Upimaji na Ramani kwa kuwa ndiyo yenye
jukumu la kutafsiri mipaka ya nchi.
Akizungumza
wakati akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali mstaafu
Nicodemus Mwengela ramani mbili za Tanzania pamoja na ile ya mkoa wa
Songwe jana, Dkt Mabula alisema, Wizara kupitia idara yake ya upimaji na
ramani ndiyo yenye mamlaka ya kuandaa na kutoa ramani nchini tofauti na
zile zinazotolewa na watu wengine ambazo wakati mwingine zinakuwa na
upotoshaji wa mipaka.
Alisema, katika
kuepukana na sintofahamu inayoweza kutokea, halmashauri nchini zinapaswa
kutumia ramani zinazotolewa na wizara ya ardhi na kuzisambaza katika
shule za msingi na sekondari ili kuepuka aina yoyote ya upotoshaji
unaoweza kutokea kwa wanafunzi.
‘’Ninaziomba
halmashauri nchini kutumia ramani zinazotolewa na wizara kupitia idara
ya upimaji kwa kuwa inatoa ramani zenye uhakika wa mipaka iliyotafsiriwa
na wataalam tofauti na watu wengine wanaotoa ramani zenye upotoshaji wa
mipaka ‘’ alisema Mabula
Naibu Waziri
Mabula ambaye alizindua pia ofisi ya ardhi mkoa wa Songwe alisema,
wizara yake itatoa ramani ya Tanzania kwenye mikoa yote na kubainisha
kuwa ramani hizo ndizo zinazotakiwa kutumika kwa kuwa zina vielelezo
vinavyokubalika.
Akigeukia
uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa, Dkt Mabula alisema uzinduzi wa
ofisi hizo ikiwemo ya mkoa wa Songwe ni jitihada za serikali ya awamu ya
tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kusogeza huduma za sekta ya
ardhi karibu na wananchi.
Kupitia uzinduzi
wa ofisi hizo za ardhi aliwataka wananchi pamoja na wadau kuzitumia
ofisi za ardhi za mikoa kupata huduma za sekta hiyo na kusisitiza kuwa
wakifanya hivyo watakuwa wamekidhi matarajio ya Raisi Magufuli kusogeza
huduma za ardhi karibu na wananchi.
Aidha, Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alionesha umuhimu na faida
ya kuwa na hati ya ardhi kwa wananchi wa mkoa wa Songwe na kuwaeleza
kuwa wanaweza kuitumia katika shughuli za kiuchumi kwa kuchukulia mkopo
benki na kutolea mfano wa jinsi hati ya kwanza kutolewa mkoa huo mwaka
1939 ambayo sasa iiko katika mkoa wa Songwe ilivyotumika kuchukulia
mkopo na wamiliki wake.
Kwa upande wake
Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali mstaafu Nicodemus Mwengela
alisema uanzishwaji ofisi za ardhi za mikao utausaidia mkoa wake kutatua
migogoro ya ardhi kwa kuwa wananchi wake hawatahitaji tena kwenda
umbali mrefu kama ilivyokuwa hapo nyuma.
Naye Kamishna
Msaidizi wa Ardhi katika ofisi ya Ardhi mkoa wa Songwe Suma Mwakasitu
alisema, ofisi yake ambayo tayari inazo hati na nyaraka mbalimbali
zilizohamishiwa kutoka iliyokuwa ofisi ya kanda mkoa wa Mbeya itaendelea
kufanya ziara kwenye wilaya nne inazohudumia kwa lengo la kuwaelimisha
wananchi kuhusuiana na huduma inazotoa ili waweze kuitumia ofisi hiyo.
No comments :
Post a Comment