Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene akizungumza na Maafisa na Askari wa Gereza la
Mahabusu Segerea, wakati alipofanya ziara katika Gereza hilo, jijini Dar
es Salaam, leo. Waziri huyo pia alifanya ziara katika Gereza Kuu la
Ukonga na Keko na kulitaka Jeshi la Magereza kujitegemea, na Serikali
ipo katika mchakato wa kuhakikisha mahabusu nao wanafanya kazi kama
ilivyokuwa kwa wafungwa. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar
es salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (katikati), akitoka Gereza Kuu Ukonga, baada ya
kumaliza ziara yake ya kutembelea Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam,
leo. Akizungumza na Maafisa na Askari wa Gereza la Segerea, Ukonga na
Keko, Simbachawene alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha
mahabusu nao wanafanya kazi kama ilivyokuwa kwa wafungwa ili kuwezesha
Jeshi la Magereza kujitegemea kwa chakula. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa
Magereza Mkoa wa Dar es salaam, ACP. Solomon Urio, na kulia ni Mkuu wa
Gereza Ukonga, ACP. Nsajigwa Mwankenja.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (kushoto), akimsikiliza Afisa Rasilimali Watu wa
Gereza Kuu la Mahabusu Segerea, ASP. Hellen Jairo alipokuwa anauliza
swali wakati Waziri huyo alipokuwa anazungumza na Maafisa na Askari wa
Gereza hilo, jijini Dar es salaam, leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene akimshika ng’ombe wa maziwa anayefugwa na Gereza
Segerea jijini Dar es Salaam, leo, ikiwa ni hatua ya kujitegemea kwa
chakula kwa Gereza hilo. Alifanya ziara gerezani hapo na kuwataka
viongozi kuhakikisha wanajitegemea, na pia kulima matunda na mboga za
majani kwa Magereza yote ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (kushoto), akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la
Magereza, wakati alipokuwa anawasili katika Gereza Kuu la Mahabusu
Segerea, jijini Dar es Salaam, leo, kwa ziara ya siku moja kusisitiza
Magereza ya Mkoa huo kujitegemea kwa chakula.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (wapili kulia), akiangalia miche ya mikorosho
inayozalishwa na Gereza Kuu la Mahabusu Segerea, Mkoani Dar es Salaam,
wakati alipofanya ziara katika gereza hilo, leo, kusisitiza Magereza ya
Mkoa huo kujitegemea kwa chakula. Kulia ni Mkuu wa Gereza hilo, Kamishna
Msaidizi wa Magereza (ACP), George Wambura.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene (aliyevaa Kaunda suti kulia), akipokea salamu kutoka
kwa Maafisa wa Jeshi la Magereza, wakati alipokuwa anawasili
katika
Gereza la Mahabusu Keko, jijini Dar es Salaam, leo, kwa ziara ya siku
moja akisisitiza Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam kujitegemea kwa
chakula. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Magereza wa Mkoa huo, Kamishna
Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon Urio. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………………………………………………….
Na Felix Mwagara, MOHA, Dar.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuhakikisha
Mahabusu waliopo katika Magereza mbalimbali nchini wanaanza kufanya kazi
kama ilivyokuwa kwa wafungwa.
Amesema mchakato huo ambao tayari
umeanza, utakapo kamilika utaleta mapendekezo madhubuti ya jinsi gani ya
kuwatumia mahabusu hao pamoja na wafungwa katika kufanya kazi za
uzalishaji mali na kuhakikisha Jeshi hilo linajitegemea kikamilifu.
Akizungumza na Maafisa na Askari
Magereza katika Magereza ya Segerea, Ukonga na Keko jijini Dar es
Salaam, leo, kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya siku moja ya
kusisitiza magereza yanajitegemea nchini, alisema ili binadamu ale
lazima afanye kazi, na pia vitabu vitakatifu vinasisitiza hilo, hivyo
mahabusu wanapaswa kufanya kazi kwa kuwa nao wanakula vyakula
magerezani.
“Kuna mjadala mkubwa tunaendelea
kuchakata kuhusu mahabusu waweze kufanya kazi, lakini lengo letu sio
kuwafanyisha kazi za sulubu, au kazi zinazotweza utu wao, hapana, wao
pamoja na wafungwa wana adhabu wanayoitumikia, tunataka kuwatumia katika
kuzalisha, kwahiyo watafanya kazi kama watu wengine wanavyofanya kazi,
hili naomba lieleweke,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “Mjadala
unaendelea na tutakuja na majibu jinsi ya kuwatumia mahabusu na
wafungwa, lakini tutakuja na majibu yenye mapendekezo tutashirikiana,
lakini tunataka kuwatumia kwa nia njema ya kuzalisha, kama mnavyojua
binadamu asipofanya kazi asile na imeandikwa katika vitabu vitakatifu,
kama mtu umemfungia ndani alafu hafanyi kazi na anadai chakula na ajue
kwamba asipofanya kazi hana haki ya kula, wewe umekuja ni mahabusu ili
upeleke tonge hapa lazima uzalishe, huwezi kusema sifanyi kazi kwasababu
ni mahabusu, hapana tutakulinda hata kwa bunduki utafanya kazi.”
Alisema lazima kuwepo na mtazamo
mpana, mkubwa katika masuala ya kuzalisha na kujitegemea kwa Jeshi la
Magereza, kwa ajili ya kuzalisha pamoja na kutatua matatizo mengine
ndani ya Jeshi hilo ikiwemo kujenga nyumba, kulipa umeme pamoja na
mahaitaji mbalimbali ya Jeshi hilo.
“Kama nilivyosema mjadala bado ni
mkubwa kwa wafungwa na tunafahamu wapo chini ya Magereza, lakini hao
wengine tumepewa tuwatunze wapo chini ya vyombo vingine, hivyo
tunaendelea na mchakato wa kujadiliana kuhusu hilo, na ukikamilika
tutawaletea majibu,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, dhana ya Jeshi
hilo kuzalisha na kujitegemea ni agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dkt.
John Magufuli kulitaka jeshi hilo kuzalisha kwa wingi ili kujitosheleza
na kujitegemea.
Aidha, alilitaka Jeshi hilo
kuhakikisha Magereza ya Mkoa wa Dar es Salaam yaanze kufanya kilimo cha
mboga za majani na matunda pamoja na ubunifu wa uzalishaji mwingine
katika mkoa huo, na magereza yaliyopo mikoani yaendelee na kilimo cha
mpunga, mahindi, ufugaji pamoja na uzalishaji wa aina nyingine
wanaoendelea nao katika maeneo yao.
Alisema kupitia uzalishaji mali
huo utawezesha kupata fedha baada ya kuuza na kusaidia majukumu mengine
ya Jeshi kuliko kutegemea fedha za matumizi mengine (OC) ambazo utolewa
na Serikali kwa Jeshi hilo.
Pia Waziri Simbachawene amelitaka
Jeshi hilo kuhakikisha wanahakiki mali zote za Jeshi ikiwemo mashamba
yajulikane, na pia ijulikane yana hati au hayana, na mifugo ya Jeshi
hilo ipo wapi na idadi yake ikiwa ni lengo la kutambua mali hizo na
kuwekwa wazi kwasababu ni mali za umma.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza
Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Solomon
Urio, alimshukuru Waziri huyo kwa kufanya ziara katika Mkoa huo na
kuwaomba viongozi mbalimbali nchini waweze kutembelea magereza ili
waweze kujifunza na kujua kazi mbalimbali zinazofanywa na Jeshi mkoani
humo.
“Tunakushukuru kwa kututembelea
Mheshimiwa Waziri, na maelekezo uliyotaoa tutayafanyia kazi, na pia
tunawaomba viongozi mbalimbali waweze kutembelea Magereza na kujua kazi
mbalimbali tunazozifanya,” alisema ACP Urio.
Simbachawene amemaliza ziara yake
ya siku moja kwa kutembelea magereza hayo, ambayo ni Gereza Kuu la
Mahabusu Segerea, Gereza Kuu la Ukonga na Gereza la Mahabusu la Keko,
ambapo katika ziara yake alipokua taarifa ya utendaji kazi kutoka kwa
Wakuu wa Magereza hayo pamoja na kuahidi changamoto zao kufanyiwa.
No comments :
Post a Comment