*********************
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Selemani Jafo ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Elimu
Kibaha kutumia rasilimali za shirika
kujiimarisha kiuchumi.
Jafo alitoa agizo hilo jana jijini hapa wakati wa kuzindua bodi mpya ya Shirika hilo inayoongozwa na Profesa Raphael Chibunda.
Alisema Shirika limekuwa na
rasilimali nyingi ikiwamo ukubwa wa ardhi ambao kama bodi itafanya
ubunifu itaweza kuitumia kufanya uwekezaji wenye tija utakaosaidia
shirika kujiimarisha kiuchumi na kujitegemea.
Hata hivyo katika kutekeleza hilo,
Jafo alionya uongozi wa shirika na bodi ya shirika hilo kuwa makini na
uwekezaji ambao wataamua kuufanya na kusisitiza kuwa ni lazima kuwe na
uwekezaji wenye tija ambao utakuwa na manufaa.
“Shirika la Elimu Kibaha lina
ardhi kubwa sana, ambayo kama mtakuwa wabunifu mtakuja na uwekezaji
ambao utasaidia sana kuimarisha uchumi wa shirika, mnaweza kuja na
maduka ya kisasa pale.
“ Lakini nitoe angalizo, ni lazima
uwekezaji mtakaoamua kuufanya muwe makini kwa kuwa na uwekezaji wenye
tija, maana kunawatu wajanja wanaweza kuja na maandiko yao feki na
kufanya uwekezaji ambao hauna tija.”
Aidha, Jafo alisema ni vyema Bodi
hiyo ikaandeleza na kuchagiza maono ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere
ambaye aliamua kuanzisha Shirika hilo ili kupambana na maadui watatu
ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.
Jafo pia aliitaka Bodi kuhakikisha
inaimarisha taasisi za shirika hizo kama hospitali ya Tumbi, chuo na
shule zilizo chini ya Shirika ili ziendelee kufanya vizuri na
kuwanufaisha wananchi wanaozunguka shirika na watanzania kwa ujumla.
Jafo pia alilipongeza Shirika hilo kwa Hospitali ya Tumbo
kuja na ubunifu wa kutengeneza maji tiba(drip) ambao umesaidia
kuipunguzia serikali gharama za kuagiza maji hayo sambamba na shule ya
sekondari kibaha na Chuo cha Ufundi (TDF) kufanya vizuri.
MKuu wa wilaya ya Kibaha,
Assumpter Mshama ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Bodi alisema
changamoto inayofanya Shirika hilo kutosonga mbele ni ufinyu wa bajeti.
Mshana ambaye pia alikuwa ni
mjumbe wa bodi iliyopita aliomba serikali kuhakikisha inatoa majibu ya
kuruhusu au kukataa maandiko mradi ambayo Shirika inaomba kutekeleza kwa
haraka ili kuweza kusonga mbele.
“Tumekuwa tunakwama sana kutokana
na kuchelewa kwa serikali kutoa kauli ya ndio au hapana katika maandiko
mradi ambayo Shirika tumekuwa tukiomba kutekeleza.
“ Unapeleka andiko, mwaka mmoja,
miwili hupati jibu lakini tukipata majibu mapema ya kama ndio tuendelee
au hapana inakasoro badilisheni hili na lile, au mradi huu haufai kabisa
ili kuja na mawazo mengine, hivyo tunawaomba wataalamu wa TAMISEMI
kufanyia kazi maandiko tunayowaletea.”
Naye Mwenyekiti wa Bodi, Profesa
Chibunda alisema Bodi yake inakwenda kutekeleza maagizo aliyoyatoa na
kulifanya shirika liimarike zaidi.
Pia alioamba ushiriki wa karibu wa Shirika katika hospitali ya Tumbi na Shule zake ambavyo kwa sasa viko chini ya Serikali.
“Tunaona kuna haja ya kubadilishwa
kwa mfumo wa uendeshaji, tunataka ya shirika kwenye shule, hopitali ya
Tumbi ili Shirika liweze kuwekeza.”
Shirika la Elimu Kibaha ni Shirika
la umma linalotoa huduma mbalimbali, lililopo Mkoa wa Pwani,
lilianzishwa mwaka 1963 kama mradi wa pamoja chini ya wafadhili watano-
Serikali ya Tanganyika kwa kipindi hicho kwa upande mmoja pamoja na nchi
nne za Kinordic (Dernmark, Norway, Finland na Sweden) kwa upande
mwengine.
Kwa kipindi hicho mradi huu ulijulikana kama “Tanganyika
Nordic Project” mpaka mwaka 1970 ambapo mradi huu ulikabidhiwa rasmi kwa
Serikali ya Tanzania na kuitwa Shirika la Elimu Kibaha. Na kusajiwa
chini ya sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969, marejeo ya
mwaka 2002.
No comments :
Post a Comment