Waziri
wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani (kulia katikati) pamoja na baadhi ya
viongozi waandamizi wa Wizara ya Nishati na taasisi zake wakionyeshwa
ramani ya mtandao wa usambazaji wa miundombinu ya gesi asilia kwa
matumizi ya nyumbani kutoka katika visima vya kuchimba gesi,baada ya
kuzindua ujenzi wa miundombinu hiyo katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani
Lindi. (Na Mpiga Picha Wetu).
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa, Serikali
kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini ( TPDC) itasambaza na
kuunganisha bila malipo miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia kwa
matumizi ya majumbani kwa wateja wa awali katika mikoa yote itayofikiwa
na huduma hiyo nchini.
Hayo ameyabainisha wakati akizindua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya
usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika Kijiji cha
Mnazi Mmoja mkoani Lindi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, Dkt.James
Mataragio( aliyenyosha mikono) akicheza na wakazi wa eneo la Mnazi
Mmoja, mkoani Lindi kufurahia uzinduzi wa ujenzi wa miundombinu ya
usambazaji gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika eneo hilo. (Na
Mpiga Picha Wetu).
Pia Waziri amewataka wakazi wa eneo hilo kuchangamkia fursa hiyo ili
kujiletea maendeleo na kuondokana na uchafuzi wa mazingira, gharama
kubwa za kununua mkaa na kuni pamoja na adha kutafuta kuni porini kwa
ajili ya kupikia, kwani matumizi ya gesi ni salama na nafuu.
Amesema kuwa, baada ya wateja hao kuunganishiwa miundombinu ya
kusambaza gesi asilia katika nyumba zao zikiwemo taasisi mbalimbali,
mteja atawekewa mita ya kupimia kiasi cha gesi anayotumia itakayofanya
kazi kama LUKU za umeme nchini.
Alisema baada ya kufungiwa miundombinu hiyo ya kusambaza gesi asilia,
mteja atatakiwa kununua uniti za gesi kulingana na mahitaji yake kama
ilivyo katika umeme, na kuzitumia endapo zitaisha kabla ya kuongeza
nyingine, mita itafunga hadi pale atakaponunua uniti zingine kuongezea,
mfumo huo unaitwa malipo kabla ya kutumia( Pre- Paid System).
Waziri amesema, kwa familia ya watu sita inakadiriwa kutumia kiasi
cha gesi ya shilingi 30,000 tu, kwa mwezi kwa matumizi yote ya kupikia
bila kubagua aina ya vyakula vinavyotumia muda mrefu jikoni.
Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati) akipata maelezo ya namna
mita ya kupima gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani, inayofanya kazi
kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli
nchini ( TPDC). (Na Mpiga Picha Wetu).
Waziri Dkt.Kalemani amesema, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais
Dkt.John Magufuli imeamua kufanya hivyo ili kuhamasisha matumizi ya gesi
asilia iliyopatikana kwa wingi hapa nchini.
Sambamba na kupunguza ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kuni na
kuchoma mkaa ili kusaidia juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira yetu,
hatua ambayo itawezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia amesema,mradi wa usambazaji wa gesi asilia ni endelevu, ambapo
kwa mwaka wa fedha 2020/2021 wateja wapya 2,000 wataunganishia gesi
majumbani, 300 kati yao wanatoka Mkoa wa Lindi na vitongoji vyake.
Alitaja mikoa inayofuata sasa katika utekelezaji wa ujenzi wa
miundombinu ya kusambaza gesi asilia kuwa ni pamoja na Morogoro, Dodoma
na Singida.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC , Dkt. James Mtaragio amewatoa hofu
watumiaji wa gesi asilia majumbani kwa kuwaeleza kuwa, usanifu na ujenzi
wa miundombinu hiyo imezingatia hatua zote za usalama.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, Dkt.James Mataragio
akizungumza na wakazi wa eneo la Mnazi Mmoja (hawapo pichani) wakati wa
uzinduzi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji gesi asilia kwa
matumizi ya majumbani katika eneo hilo. (Na Mpiga Picha Wetu).
Amesema, lengo la kufanya hivyo ni ili kuhakikisha matumizi ya gesi hiyo yanakuwa salama zaidi kwa mtumiaji na jamii kwa ujumla.
Dkt.Mataragio pia amewaomba wananchi kuondoa hofu katika matumizi ya gesi asilia kwa shughuli za kupikia.
Dkt.Matargio akizungumzia gharama za matumizi ya gesi hiyo
ikilinganishwa na mkaa pamoja na kuni amesema kuwa, kwa ulinganishi
matumizi ya mkaa si chini ya shilingi 4,500 kwa,wakati matumizi hayo
hayo kwa kutumia gesi ni shilingi 1000 tu kwa kupikia.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amesema kuwa,
Mkoa wa Lindi umeandika historia nyingine iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda
mrefu ya ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia itakayokuwa
ikitumika kwa kupikia majumbani, mahotelini kwenye taasisi za afya,
elimu na matumizi mengineyo kama viwandani na kuendeshea magari.
RC Zambi ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na TPDC kwa
kutenga fedha zitakazowezesha utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa
Lindi na baadae kote nchini.
Mkuu
wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi akizungumza na wakazi wa eneo la Mnazi
Mmoja (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa miundombinu ya
usambazaji gesi asilia kwa matumizi ya majumbani katika eneo hilo. (Na
Mpiga Picha Wetu).
Pia Mkuu huyo amewashukuru wananchi mkoani hapa kwa ushirikiano
waliouonyesha katika kipindi chote cha kutekeleza mradi huo na kuwaomba
waendelee na moyo huo wa kizalendo kwani mradi huo ni kwa manufaa yao na
Taifa kwa ujumla.
Pages
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments :
Post a Comment