Friday, May 29, 2020

OSHA, WENYE VIWANDA WAJADILI UTEKELEZAJI WA SHERIA YA AFYA NA USALAMA KAZINI



Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akizungumza na viongozi na wanachama wa CTI
(hawako pichani) katika kikao kilichofanyika katika ofisi za OSHA, Kinondoni, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Bw. Leodgar Tenga, akichangia hoja katika
kikao kilichofanyika baina ya viongozi wa CTI na OSHA leo katika ofisi za OSHA-Kinondoni Dar es Salaam.
Viongozi na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) wakifuatilia mada mbali mbali kuhusu
utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi zilizowasilishwa kwao na
wawakilishi wa
menejimenti ya OSHA katika kikao kilichofanyika katika ofisi za OSHA leo.
**********************************
Na Mwandishi Wetu
Viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) wametembelea ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kujadiliana na wenyeji wao
namna bora zaidi ya kuboresha mifumo ya usalama na afya katika viwanda hapa nchini.

Ujumbe huo wa viongozi kutoka CTI ambao ulijumuisha baadhi ya wawakilishi wa wanachama wa CTI uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirikisho hilo, Bw. Leodgar Tenga.

Akizungumza baada ya kuhitimisha kikao hicho, Tenga amesema madhumuni ya kikao yalikuwa ni kujadiliana juu ya utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

“Tunafahamu kwamba OSHA ipo kwa mujibu wa sheria na ina kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama wa wafanyakazi katika maeneo ya kazi na
wenye viwanda ndio wahusika wakubwa sana katika hili na kwasababu hiyo tumekuja ili kuona ni kwa jinsi gani tutahakikisha wenye viwanda wanatimiza matakwa ya OSHA,” alisema Bw. Tenga na Kuongeza:

“Kikao kilikuwa kizuri, tumebadilishana mawazo kwa uwazi kabisa, tumewaambia wenzetu wanachama wetu wanasema nini kuhusu utendaji wao na wao pia wamesema jinsi ambavyo wenye viwanda wanatekeleza sheria na pale ambapo pana upungufu kila upande tumeuzungumza na hatimaye tumekubaliana kwamba ipo haja ya wenye viwanda kuelimishwa zaidi kuhusu hii sheria.”

Kwa mujibu wa Bw. Tenga kupitia kikao hicho wanatarajia kutakuwa na uelewa zaidi kwa pande zote mbili na kwamba; kwa upande wa OSHA wataelewa changamoto
ambazo viwanda vinakumbana nazo na wenye viwanda wataelewa ni wanapaswa kufanya katika kuteleza sheria.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda, amewaeleza wenye viwanda kuwa bado kuna changamoto nyingi za kiusalama katika viwanda na
kuwasisitiza kuweka mifumo madhubuti ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.

“Kwahiyo nilipenda nanyi mfahamu kwamba usalama katika viwanda vyetu haupo katika viwango stahiki kwa asilimia zote na ndio maana taasisi yetu imekuja na mpango mahsusi wa kuzuia ajali katika sehemu za kazi ujulikanao kama ‘Vision Zero’ ambao endapo utatekelezwa ipasavyo katika viwanda na sehemu nyingine kazi basi matukio ya ajali yatabaki kuwa historia,” alisema Bi. Mwenda.


Veronica Mbazingwa kutoka kampuni ya Chemicotex, amesema kikao hicho imekuwa ni fursa nzuri kwao ya kujifunza jinsi ambavyo OSHA inashiriki kikamilifu katika kuwasaidia wawekezaji hasa katika kuhakikisha kwamba usalama wa wafanyakazi ambao ndio nguvu kazi kubwa katika uzalishaji wa viwandani unakuwa katika mtiririko unaotakiwa kisheria.

Naye Khalifan Ramadhani wa kampuni ya Advent Construction Ltd, alieleza kuridhishwa kwake na maelezo yaliyotolewa na viongozi wa OSHA katika kikao hicho
ambayo alisema yamejibu maswali mbali mbali aliyokuwa nayo kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi.

Aidha, aliipongeza OSHA kwa kazi nzuri inayofanya katika kusimamia usalama na afya katika maeneo ya kazi hapa nchini.

No comments :

Post a Comment