Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (wa pili kulia) akipokea sehemu
ya malipo ya dola milioni 100 (Sh. bilioni 250) kutoka Kampuni ya
Madini ya Barrick ikiwa ni makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya
Serikali ya Tanzania na kampuni hiyo yaliyofikiwa Disemba 2019. Wa
kwanza kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Mhe. Palamagamba Kabudi. Wa tatu ni Naibu waziri wa Madini
Mhe. Stanslaus Nyongo, akifuatiwa na Bw. Hilaire Diarra Mwakilishi Mkazi
wa Kampuni ya Barrick na Bw. Luiz Correia Meneja Mkuu Mgodi wa North
Mara, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Palamagamba Kabudi na viongozi
mbalimbali wakimsikiliza Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick
Dkt. Denis Mark Bristow aliyekuwa akifuatilia hafla ya makabidhiano ya
mfano wa hundi ya dola milioni 100 kati ya Kampuni hiyo na Serikali, kwa
njia ya mtandao akiwa nchini Afrika Kusini, tukio hilo limefanyika
katika ukumbi wa Kambaraje wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Bw. Hilaire
Diarra Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya Barrick (Kulia) na Bw. Luiz
Correia Meneja Mkuu Mgodi wa North Mara, wakimsikiliza Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayumo pichani) alipokuwa
akizungumza na viongozi wa Serikali na vyombo vya Habari baada ya
kupokea sehemu ya malipo ya dola milioni 100 (Sh. bilioni 250) kutoka
Kampuni ya Madini ya Barick, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza jijini Dodoma na
vyombo vya habari wakati wa hafla ya kupokea sehemu ya malipo ya fidia
ya Sh. bilioni 250 kutoka Kampuni ya Madini ya Barick, jijini Dodoma,
tarehe 26 Mei, 2020.
Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James kulia na Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga wakimsikiliza Waziri wa Fedha na
Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayumo pichani) alipokuwa
akizungumza na viongozi wa Serikali na vyombo vya habari baada ya
kupokea sehemu ya malipo ya Sh. bilioni 250 kutoka kampuni ya
madini ya
Barick, Jijini Dodoma.
(Picha na Saidina Msangi-Wizara ya Fedha na Mipango)
*********************************
Na Farida Ramadhani na Josephine Majura
KAMPUNI ya
Barrick imeilipa Tanzania dola milioni 100, sawa na takriban sh. bilioni
250, ikiwa ni sehemu ya malipo ya dola milioni 300 ambazo Kampuni hiyo
ya Madini ilikubali kulipa kama fidia ya kodi.
Mfano wa Hundi ya
kiasi hicho cha fedha imekabidhiwa na Meneja Mkazi wa Kampuni ya
Barrick, Bw. Hilaire Diarra kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango, kwa niaba ya Serikali, Jijini Dodoma tarehe 26 Mei,
2020.
Akizungumza baada
ya kupokea hundi hiyo mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo
Mwenyekiti wa Timu ya Serikali ya Majadiliano na Barrick ambaye pia ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.
Palamagamba Kabudi na Kamati yake, Dkt. Mpango alisema tukio hilo ni
mwanzo wa makubaliano ya mkataba wa msingi kati ya Serikali ya Tanzania
na kampuni hiyo yaliyofikiwa Disemba 19, 2019 na kusainiwa rasmi Januari
24, 2020.
Dkt. Mpango
aliyataja makubaliano mengine yaliyofikiwa kati ya Serikali na kampuni
hiyo kuwa ni kuundwa kwa Shirika la Madini la Twiga lenye umiliki wa
pamoja likalofanya kazi nchini katika kusimamia uendeshaji wa migodi ya
Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara pamoja na migodi mingine nchini ambapo
Serikali ya Tanzania itashiriki katika utoaji wa maamuzi kuhusu
uendeshaji wa migodi, mipango, manunuzi pamoja na masoko ya madini.
“Tulikubaliana
kuhakikisha kuwa faida za kiuchumi zinazotokana na migodi ya Bulyanhulu,
Buzwagi pamoja na North Mara zigawanywe kwa msingi wa usawa wa asilimia
50 kwa 50 kati ya washirikania ambapo hisa za Serikali zinazotokana na
faida za kiuchumi zitatolewa katika mfumo wa mrabaha, kodi pamoja na
kupata asilimia 16 ya faida kutokana na makampuni hayo kufanya kazi
nchini” alisema Dkt. Mpango
Dkt. Mpango
alisema mbali na makubaliano hayo, kampuni ya Barrick imekubali kutoa
kiasi cha dola za Marekani milioni 5 kwa ajili ya kufanya upembuzi
yakinifu wa ujenzi wa Mtambo wa kuchakata madini nchini (smelter).
“Kampuni ya
Barrick pia imekubali kuanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kuahidi kutoa hadi dola milioni 10 kwa kipindi cha miaka kumi
kwa ajili ya utoaji wa mafunzo yanayohusu sekta ya madini”, aliongeza
Dkt. Mpango.
Alisema Kampuni
ya Barrick ilikubali kutoa dola 6 kwa kila ounce ya madini itakayouzwa
(ikijumuisha mchango kwenye Mfuko wa Mandeleo ulioanzishwa na Kampuni ya
Barrick Tanzania) ili kusaidia jamii zinazozunguka maeneo ya migodi
pamoja na kutoa kiasi cha dola milioni 40 kwa ajili ya kuboresha kipande
cha barabara kati ya Bulyanhulu na Mwanza na kujenga nyumba na
miundombinu yake.
“Naipongeza
Kampuni ya Barrick kwa kuanza kutekeleza makubaliano haya na natoa wito
kwa kampuni nyingine za madini na wawekezaji wengine katika sekta hiyo
kuiga mfano mzuri uliooneshwa na Kampuni hii katika kuhakikisha kunakuwa
na hali ya usawa katika uendeshaji wa shughuli za madini nchini kwa
faida ya pande zote mbili” alisisitiza Dkt. Mpango.
Naye Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto
James alisema kuwa fedha hizo tayari zimeshapokelewa kwenye Mfuko Mkuu
wa Serikali.
Kwa upande wake
Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Dennis Mark Bristow
ambaye alikuwa akifuatilia makabidhiano hayo kwa njia ya mtandao na
kutoa hotuba yake akiwa nchini Afrika Kusini alimpongeza Mhe. Rais Dkt.
John Pombe Magufuli pamoja na Timu yake kwa kufanikisha majadiliano
yaliyosaidia kuanzishwa kwa ushirikiano wa dhati kati ya Kampuni yake na
Serikali.
Alisema kuwa
wataendeleza ushirikiano wao na Tanzania na kwamba wanaamini kuwa
ushirikano huo utakuwa wa mfano si tu kwa Afrika bali utakuwa ni
ushirikiano wa mfano kwa Dunia nzima.
Aliahidi
kuendelea kuboresha miundombinu ya maeneo ya migodi wanayomiliki nchini
na kueleza kuwa wanajiolojia wanafanyakazi kwa bidii ili kuirudisha
hadhi ya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha uzalishaji dhahabu duniani.
No comments :
Post a Comment