Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati, imeishauri serikali kutumia vyema
mdororo wa bei ya mafuta duniani, ili kupata mafuta kwa masharti nafuu
na kuanzisha hifadhi ya mafuta kimkakati kwa ajili ya siku zijazo.
Akiwasilisha
maoni ya kamati hiyo bungeni jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstun
Kitandula, alisema ni vyema kwa wakati huu serikali ikazungumza na nchi
rafiki zinazozalisha mafuta ili kupata mafuta hayo.
Alisema
katika kutekeleza hilo ni vyema Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini
(TPDC) liwezeshwe ili kupokea akiba hiyo ya mafuta.
Alisema
tayari ulimwengu umeanza kushuhudia Sekta za Usafiri wa Anga na Utalii
zikisimama, biashara na uzalishaji viwandani kushuka na hivyo kushuka
kwa kiasi kikubwa kwa matumizi ya mafuta na bei yake kuporomoka.
"Kufuatia
mkanganyiko huu na mwenendo usiotabirika wa soko la mafuta ulimwenguni,
ipo haja kwa nchi yetu kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha nchi
inakuwa na akiba ya mafuta ya kutosha wakati wote,” alisema.
Kitandula
alisema kamati pia ilichambua taarifa kuhusu hali ya upatikanaji wa
mafuta nchini na kubaini kuwa, kwa kipindi chote cha Julai 2019 hadi
Februari 2020, hali ya upatikanaji wa nishati hiyo ilikuwa nzuri na nchi
ilikuwa na akiba ya mafuta ya kutosha kwa wastani wa zaidi ya siku 40
kwa kila aina ya mafuta.
“Hii ni ongezeko la asilimia 55 kulinganishwa na siku 15 za akiba ya mafuta zinazotakiwa kwa mujibu wa kanuni,” alibainisha.
Alisema
mfumo wa BPS (Bulk procurement System) umewezesha kupungua kwa gharama
za meli kusubiri kupakua mafuta kutokana na upangaji na usimamizi mzuri
wa uletaji meli za mafuta (laycan) ambao umepelekea muda wa meli
kusubiri kupungua kutoka wastani wa siku 45 kwa siku za nyuma hadi
wastani wa siku tano kwa sasa.
“Kamati
ilibaini kuwa, kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020, gharama
za meli kusubiri imepungua kwa asilimia 18.4 ikilinganishwa na kipindi
kama hicho kwa mwaka 2018/2019,”alifafanua.
Alisema
jumla ya lita 4,161,067,814.92 za mafuta ya dizeli, petroli, ndege na
taa ziliingizwa kwa matumizi ya ndani ya nchi (local) na nchi za jirani
(transit) kwa kipindi cha Julai 2019 hadi Februari 2020.
Kitandula
ambaye ni Mbunge wa Mkinga, alisema katika kiasi hicho cha mafuta,
jumla ya lita 2,398,969,342.12 sawa na asilimia 58 kilikuwa kwa ajili ya
matumizi ya ndani, na lita 1,762,098,472.80 sawa na asilimia 42 kwa
ajili ya nchi za jirani.
Vilevile,
alisema kamati imeridhishwa na hali ya upatikanaji wa mafuta nchini
pamoja na usimamizi mzuri wa uagizaji wa mafuta unaofanywa na wakala wa
uagizaji wa mafuta kwa pamoja (PBPA) kwa kushirikiana na mamlaka
nyingine.
No comments :
Post a Comment