Chuo Kikuu cha Kenyatta
Baadhi ya raia waliowekwa Karantini eneo la Chuo Kikuu cha Kenyatta
nchini Kenya, wamezua tafrani baada ya kutishia kujiua kwa kujirusha
kutoka ghorofani, wakidai kunyanyaswa na Serikali wakilazimishwa kulipa
ada ya Karantini.
Raia hao wamesema hawana uwezo wa kulipa ada hiyo, kwani waliambiwa kuwa
Serikali imesimamia kila kitu kuhusu wagonjwa watakaowekwa Karantini.
Kupitia video iliyoripotiwa na kituo cha televisheni cha NTV nchini
humo, imewaonesha raia hao wakipiga kelele kuwa wanataka kujirusha
kutoka ghorofani kutokana na kadhia hiyo, huku wahudumu wa afya
wakiwasihi kuacha kufanya hivyo.
Baada ya kubadilisha uamuzi wao, mmoja wa watu waliotaka kufanya kitendo
hicho amesimulia, "nilitolewa nyumbani nikiwa na shida ya kifua na
kukohoa, nikapelekwa kupimwa kisha nikaletwa hapa Kenyatta, lakini siku
nataka kutoka nikaambiwa huwezi kutoka mpaka ulipe, nikauliza nalipa
nini wakati Serikali imesimamia kila kitu?".
Mgonjwa mwingine amesema kuwa aliletwa chuoni hapo akisumbuliwa na kifua
na si Corona lakini hakupewa matibabu na amewekwa chuoni hapo kwa siku
zaidi ya 21 kwa kuwa hana pesa za kulipa.
Kwa pamoja, wananchi hao wameiomba Serikali ya Kenya kuwaangalia upya
kwa kuwa hawana pesa za kulipia, hivyo wanaombwa waachiwe kwa sababu wao
si wahalifu.
No comments :
Post a Comment