Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,
akisalimiana na Wabunge wakati akiingia Bungeni, kabla ya kusoma hotuba
ya mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali, pamoja na makadirio ya
mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge
kwa mwaka 2020/2021, Aprili 1, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***********************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kutekeleza Mradi wa
Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) ambapo vijiji vilivyounganishiwa
umeme nchini vimeongezeka kutoka vijiji 2,118 mwaka 2015 hadi vijiji
9,001 mwezi Machi 2020.
Amesema kuwa
jumla yataasisi 11,128 zikiwemo za elimu, afya, dini, mashine za
kusukuma maji na huduma za biashara zimenufaika na mradi, hivyo
mafanikio hayo pamoja na mengine makubwa yaliyopatikandani ya kipindi
cha takriban miaka mitano yamesaidia kuimarisha hali ya kiuchumi wa
Taifa na kijamii kwa ujumla.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 1, 2020) akiwasilisha Bungeni
hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge
kwa mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma.
“Mheshimiwa Spika,tarehe
20 Novemba 2015 wakati akifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli aliwaahidi wananchi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Tano
itawatumikia na kuwajali.
Waziri Mkuu
amesema katika kutekeleza azma hiyo, ujenzi wa miundombinu muhimu ya
kiuchumi hususan ya usafiri na usafirishaji sambamba na uimarishaji wa
huduma muhimu za kijamii ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele
na Serikali ya Awamu ya Tano.
Amesema
ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa, ufufuaji wa Shirika la
Ndege la Tanzania na urejeshwaji wa mali za ushirika mfano, NCU,
SHIRECU ni kati ya hatua za msingi zinazochukuliwa na Serikali katika
kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda ifikapo 2025.
Waziri Mkuu
amesema hatua nyingine ni pamoja na urejeshwaji wa mali za Mamlaka ya
Mkonge Tanzania, ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere,
ulinzi wa maliasili na rasilimali za Taifa pamoja na ujenzi na ukarabati
wa miundombinu ya Elimu, Afya na Maji.
“Katika
kipindi hiki cha miaka mitano, tumeshuhudia miradi hiyo muhimu ikiwa
katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa mfano, ujenzi wa Reli ya
Kati kwa kiwango cha Kimataifa ambao hadi Machi 2020 umetumia sh.
trilioni 2.96 na kukamilika kwa asilimia 75 kwa kipande cha Dar es
Salaam hadi Morogoro na asilimia 28 kwa kipande cha Morogoro hadi
Makutupora.”
Amesema
utekelezaji wa mradi huo umewezesha utoaji wa zabuni zenye thamani ya
sh. bilioni 664.7 kwa wazabuni na wakandarasi wa ndani 640, ajira
zipatazo 13,177 za kitaalam na zisizo za kitalaam zimezalishwa na kati
ya hizo, ajira za kitaalam kwa wazawa ni asilimia 46.5 ikilinganishwa na
asilimia 53.5 ya wageni.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Serikali inatumia gharama kubwa katika kujenga
miundombinu hiyo wezeshi ya kiuchumi kwa lengo la kulifanya Taifa kuwa
na uchumi imara wa kujitegemea na wenye kuhimili ushindani. Fedha hizo
pia zimekuwa chanzo cha ajira na zabuni kwa Watanzania zinazowasaidia
kuongeza kipato.
“Mradi huu
utakapokamilika utaongeza ufanisi wa huduma za usafiri na usafirishaji
wa bidhaa na abiria pamoja na kupunguza gharama za uchukuzi pia
utachochea ukuaji wa miji na sekta nyingine kama vile kilimo, viwanda,
utalii na biashara. Vilevile, mradi huu utakuwa chanzo cha ongezeko la
mapato ya Serikali yatakayosaidia katika kuboresha maslahi ya watumishi
na huduma za kijamii kama vile afya, elimu na maji.”
Vilevile,
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji wa
Julius Nyerere linalotarajiwa kuzalisha Megawati 2,115, hadi Machi 2020
mradi huo umegharimu sh. trilioni 1.28 na umekamilika kwa asilimia
10.74.
Amesema
kukamilika kwa bwawa hilo kutalihakikishia Taifa letu umeme wa uhakika
na wa nafuu zaidi. Aidha, ongezeko hilo la uzalishaji wa umeme
litawezesha shughuli za uzalishaji viwandani kuwa za uhakika, tija,
ufanisi na gharama nafuu zaidi. “Vilevile, mradi huu utachangia kwa
kiasi kikubwa katika juhudi za kuhifadhi mazingira kutokana na
kuongezeka kwa matumizi ya nishati ya umeme badala ya kuni.”
Hata hivyo,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa kila mwananchi kuendelea kuunga mkono
jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya
uongozi mahiri na thabiti wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya
kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga
vita rushwa.
Wakati huo
huo, Wazirti Mkuuamesema Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini
yake inaliomba liidhinishe jumla ya sh. 312,802,520,000; kati ya fedha
hizo, sh. 88,429,156,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh.
224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile
Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 121,786,257,000 kwa
ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo, sh. 113,567,647,000 ni kwa
ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya
matumizi ya maendeleo.
No comments :
Post a Comment