*********************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji
wa huduma za jamii unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano umechangia
kuzalisha ajira milioni 12.6 kwenye sekta mbalimbali nchini.
Ameyasema
hayo leo (Jumatano, Aprili mosi, 2019) wakati akiwasilisha hotuba kuhusu
Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka
2020/2021.
“Mafanikio
haya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uboreshaji wa huduma
za jamii yameenda sambamba na uzalishaji wa ajira zipatazo milioni 12.6
zikiwemo ajira za moja kwa moja milioni 11.7 kwenye sekta mbalimbali
nchini,” amesema.
Akitoa mfano
Waziri Mkuu amesema sekta za afya, elimu na utawala zimetoa ajira za
kudumu kwa kuajiri watumishi 28,403 katika mamlaka za Serikali za Mitaa;
ufufuaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) pamoja na kuboresha
viwanja vya ndege umetoa jumla ya ajira 2,970 huku ujenzi wa viwanda
nchini ukichangia ajira 41,900.
“Mradi wa
reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa umewezesha kuzalishwa ajira
zipatazo 13,177 za kitaalam na zisizo za kitalaam. Kati ya hizo, ajira
za kitaalam kwa wazawa ni asilimia 46.5. Pia, kupitia mradi huu kumekuwa
na utoaji wa zabuni zenye thamani ya shilingi bilioni 664.7 kwa
wazabuni na wakandarasi wa ndani 640,” ameongeza.
“Mradi wa umeme
wa Mwalimu Nyerere kupitia maporomoko ya mto Rufiji umezalisha jumla ya
ajira 3,897 ikiwemo ajira za wazawa 3,422.”
Amesema
jumla ya mafundi 845,348 walipata ajira za mikataba na muda kwenye
ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo Hospitali za
Wilaya, vituo vya afya, zahanati, madarasa, nyumba na majengo maeneo
mapya ya utawala, miradi ya barabara chini ya TARURA kwa kutumia Force Account.
Akifafanua
zaidi, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa katika
usimamizi madhubuti wa sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa
viongozi na watumishi wa umma. “Usimamizi huo, umewezesha viongozi na
watendaji wa umma kuwajibika ipasavyo kwa wananchi ambao ndiyo waajiri
wao. Sambamba na hilo, nidhamu Serikalini imeongezeka kutokana na
Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wazembe, wadanganyifu
na wasio waadilifu.”
Waziri Mkuu
amesema mafanikio yote hayo yanachangiwa na uongozi mahiri wa Rais Dkt.
John Pombe Magufuli. “Tunapotaja mafanikio haya tuna kila sababu ya
kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwani uongozi wake mahiri na wenye uthubutu
ndiyo msingi mkuu wa mafanikio yaliyopatikana.”
“Dhana na
falsafa aliyojenga ya Hapa Kazi Tu imesaidia kubadili mtazamo wa
Watanzania wengi ambapo sasa tunashuhudia uwajibikaji wa kiwango cha juu
wa mtu mmoja mmoja, katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na
uzalishaji iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni na kwingineko badala
ya tabia ya awali ya baadhi ya wananchi wachache kupoteza muda mwingi
katika shughuli zisizokuwa na tija kwa Taifa.”
No comments :
Post a Comment