*******************************
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz amekabidhi vifaa
mbalimbali vikiwamo vitakasa mikoni na barakoa ili kusaidia mapambano
dhidi ya Corona jijini Dar es Salaam.
Rostam amekabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda jijini humo leo Alhamisi Aprili 16, ikiwa ni sehemu ya
ahadi yake kwa Waziri Mkuu wiki iliyopita ya
kutoa Sh bilioni moja
kusaidia vifaa hivyo katika daladala za jiji la Dar es Salaam na
Zanzibar.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Rostam amesema pamoja
na vitakasa mikono hivyo na barakoa alizotoa lakini leo ameongeza
mchango wake kwa hospitali mbalimbali kwa wauguzi wote ambapo amejitolea
barakoa 70,000 ili madaktari na manesi ambao ndiyo wako hatarini kuliko
mtu yeyote.
Vingine ni galoni 6,000 za lita tano za vitakasa mikono na
mashine maalumu za kupuliza dawa ya kupambana na maambukizi ya virusi
hivyo.
“Kama nilivyosemna tuna janga. Janga hili la maradhi ya corona
haliko tu Tanzania lakini lipo sehemu zote duniani. Na kama sote
tunavyojua ugonjwa huu hauna tiba, tiba pekee ni kujihami usiupate.
“Mheshimiwa rais wetu Machi 22 mwaka huu, katika hotuba yake kwa
taifa kuhusu janga hili, akitangaza maradhi ya corona alitupa tahadhari
alituambia kwamba pamoja na kuchapa kazi na kuendelea na shughuli zetu
za kila siku za kutafuta riziki lazima tuchukue tahadhari kwa kunawa
mikono, kutokusanyika na mengineyo.
“Hivi sasa ni wazi kwamba tahadhari hizo inabidi tuzizingatie
kuliko wiki iliyopita au wiki mbili zilizopita, leo hii kwa mara ya
kwanza nimevaa hii kitu inaitwa barakoa na hii nimetengenezewa na mama
yangu kwa hiyo huna haja ya kwenda kuinunua dukani unachukua shuka au
foronya unaifunga na kamba,” amesema Rostam.
Akizungumza namna barakoa hiyo inavyofanya kazi, Rostam amesema
inaweza kukuepusha na maradhi mengi, na kwamba jambo hilo linaweza
kufanyika kwa kila mtu ambapo unaweza kuchukua nguo yako iliyochakaa
ukatengeneza.
Amesema amezungumza na madktari wakamwambia ni vema kuvaa
barakoa wakati unakwenda kwenye msongamano wa watu lakini pia watu
wanaweza kutengeneza wenyewe si lazima kununua madukani.
Pamoja na mambo mengine, Rostam ametoa wito kwa wafanyabiashara
wengine kuisaidia serikali kwa kutoa msaada wa vifaa vya kupambana na
corona akitolea mfano kwa nchi nyingine wafanyabiashara walivyosaidia
nchi zao
“Kama kawaida yangu ningependa kuwaomba wafanyabiashara
wenzangu hili si jukumu la serikali pekee, wafanyabiashara wengi
duniani wameishaidia serikali, tumeona Amazon wamejitolea. Si
lazima uwe mfanyabiashara mkubwa, hata mfanyabiashara wa duka unaweza
kuweka ndoo ya maji dukani na ukaweka vitakasa mikono kwa wafanyakazi
unaweza kuokoa maisha ya watu. Natoa wito kwa
wafanyabisahrawa wakubwa na wadogo kwa kikasi tunachoweza tusaidiane
kuisaidia serikali mzigo huu mzito ili wananchi wengi zaidi wasipate
maambukizi haya,” amesema Rostam.
No comments :
Post a Comment