Wednesday, April 1, 2020

Makonda Awataka Wenye Nyumba Dar Wapunguze Kodi za Nyumba wakati huu wa Janga la Corona


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka wamiliki wa nyumba jijini humo kuwapunguzia kodi ya miezi mitatu wapangaji wao kwa asilimia 50 kutokana na hali ya uchumi ilivyo katika kipindi hiki cha mlipuko wa janga la virusi vya corona.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili Mosi, alipokuwa akizungumza na wananchi katika kituo cha mabasi cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.

“Nimeongea na wenye nyumba na kuwataka wapunguza kodi kwa asilimia 50 ili kusaidia kufanya biashara na kuangalia hali ya uchumi ilivyo kwa sasa kama mnavyofahamu corona imeathiri hali ya kifedha,” amesema Makonda.

Aidha amewaruhusu waendesha pikipiki maarufu bodaboda, kuingia mjini ili kupunguza adha ya usafiri na msongamano katika vituo vya daladala baada ya kutangazwa utaratibu mpya wa ‘level seat’ ili kuepuka maambukizi ya virusi hivyo.

“Tunachotakiwa kufanya hivi sasa ni kusaidia wafanyakazi kuwahi kazini na kufanya shughuli kwa wakati ili tuweze kuepukana na hali ngumu ya maisha,” amesema Makonda.

Pamoja na mambo mengine, Makonda ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Sumatra), kuhakikisha ifikapo kesho jumatano Aprili 2, saa 6:00 mchana wawe wameshabadilisha ruti za magari kuwa fupi.

No comments :

Post a Comment