Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Lukuvi
alitoa maagizo hayo jana jijini Dodoma wakati wa kupokea taarifa ya
Makatibu Wakuu iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo kwa Mawaziri wa Wizara zinazohusika
katika utekelezaji huo kufuatia uamuzi wa Rais John Pombe Magufuli
kuvibakisha vijiji 920 kati ya 975 kwenye maeneo ya hifadhi yaliyokuwa
na mgogoro.
Wizara ambazo Makatibu Wakuu wake wanashiriki kazi ya utekelezaji
maagizo hayo ni Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama
Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Kilimo,
Maji, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Makamu wa Rais ambazo Mawaziri wake
walitembelea maeneo yenye mgogoro na kuja na mapendekezo yaliyopelekea
Rais kuchukua uamuzi huo.
Awali wananchi waliokuwa wakiishi kwenye vijiji vya hifadhi ya misitu
walionekana wavamizi wakati serikali ilitoa hati za usajili kwa vijiji
na wananchi wake kushiriki shughuli mbalimbali zikiwemo za uchaguzi
jambo lililomfanya Rais Magufuli kuchukua uamuzi wa kuvibakisha vijiji
920 baada ya kupata ushauri wa mawaziri wa sekta husika.
Lukuvi alisema, katika kipindi hiki ambacho kamati za wataalamu
zinapitia taarifa za utekelezaji maamuzi kuhusiana na suala hilo lazima
ufanyike uchambuzi wa kina ili kuja majibu yatakayokidhi malengo ya
uamuzi uliofanyika hasa ikizingatiwa baadhi ya maeneo ya vijjiji
hayahitaji kupunguzwa.
‘’Ufanyike uchambuzi wa kina kuona faida itakayopatikana na vijiji
vingapi vitanufaika na tupate taarifa itakayoainisha kila eneo na
makubaliano yake’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kila sekta inayohusika inatakiwa kufanya uchambuzi
katika eneo lake na kutolea mfano Wizara ya Viwanda na Biashara inaweza
kuja na uchambuzi utakaoainisha maeneo ya EPZA yaliyorudishwa kwa
wananchi huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikiainisha maeneo
yaliyopunguzwa kwa shughuli za ufugaji na kilimo na Kamishna wa Ardhi
akibainisha maeneo yaliyofutwa.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema wakati wa utekelezaji kazi ya
uchambuzi ikiendelea wasimamizi wa sheria katika maeneo ya hifadhi
wanapaswa kuendelea kusimamia sheria na kuwatahadharisha kuwa makini
wakati wa utekelezaji majukumu yao ili kuepuka uvunjifu wa amani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary
Makondo alisema kamati ya Makatibu Wakuu imeendelea kufanyia kazi
utekelezaji maamuzi ya vijiji 920 kama walivyoelekezwa.
Kwa mujibu wa Mary, kamati ya Makatibu Wakuu katika kutekeleza maagizo
ya Mawaziri inatarajia kukamilisha kazi ya tahmini ya vijiji 920 katika
muda wa wiki mbili na kuwasilisha taarifa yake kwa mawaziri wa sekta
kama ilivyoelekezwa mwisho wa mwezi huu wa Aprili.
Kwa muda mrefu wananchi wa Vijiji 975 vilivyo katika hifadhi wamekuwa
katika mgogoro kwa kudaiwa kuwa wavamizi na kusababisha nyumba zao
kuchomwa moto huku baadhi yao wakiwa wameishi maeneo hayo kwa zaidi ya
miaka ishirini.
Mgogoro huo ulisababisha Rais John Pombe Magufuli kuingilia kati na
kuridhia vijiji 920 kubaki maeneo ya hifadhi sambamba na kufutwa misitu
ya hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 ili ipangwe upya. Pia Rais
Magufuli alifuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na
ardhi hiyo kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, kilimo na shughuli
za ufugaji.
No comments :
Post a Comment