Thursday, April 30, 2020

JAJI AUGUSTINO RAMADHANI KUAGWA KITAIFA



**********************************
Dar es Salaam, 30/4/2020
Mwili wa aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Augustino Ramadhani unatarajiwa kuagwa rasmi kitaifa kesho Ijumaa Mei Mosi, mwaka huu katika viwanja vya Karimjee, na mazishi yatafanyika Mei 2 Kimara jijini Dar es salaam.
Kiongozi huyo ataagwa Kitaifa kwa mujibu wa Sheria ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa ya
mwaka 2006.
Taarifa iliyotolewa leo na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Kelvin Mhina ilieleza kwamba taratibu zote za mazishi na maandalizi zinafanywa na kusimamiwa na Kamati ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa inayoongozwa na
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa.
‘‘Siku ya Ijumaa kutakuwa na Mazishi ya Kitaifa katika viwanja vya Karimjee kuanzia saa 6:00 mpaka saa 8: 00 mchana.’’ilieleza taarifa hiyo.
Aidha Mhe. Mhina alisema Jaji Ramadhani atazikwa siku ya Jumamosi Mei 2, mwaka huu katika eneo la makaburi ya familia yaliyopo Kimara King’ongo jijini Dar es Salaam.
Mazishi yatafanyika kuanzia saa 9: 30 alasiri na kutanguliwa na ibada itakayofanyika katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Albano, jijini Dar es
Salaam kuanzia saa 6:30 mchana.
Ibada itafanyika katika kanisa ambalo alikuwa akisali, mwanakwaya wa kanisa, kushiriki kupiga kinanda na kulitumikia kwa nyakati tofauti.
Jaji Ramadhani alifariki dunia Aprili 28, mwaka huu saa 2:05 asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam, baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya saratani na mwishoni kupata Mshtuko wa Moyo (Heart Attack).
Marehemu Jaji Ramadhani alianza kuugua mwaka 2011 na kugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ambapo alitibiwa katika hospitali mbalimbali nje na ndani ya
nchi. Hospitali alizotibiwa ni pamoja na hospitali za Apollo na Bangalow nchini India, Afrika ya Kusini, Nairobi Agha Khan na Dar es salaam Agha Khan.

No comments :

Post a Comment