Sehemu mbalimbali
za eneo la Mradi wa Maji Ng’apa katika Manispaa ya Lindi ukiwa katika
utekelezaji kama ilivyokutwa na kamera ya Idara ya Habari (MAELEZO)
wakati wa ziara ya timu ya Maafisa Habari waliotembelea mradi huo hivi
karibuni Mkoani Lindi.
Picha na MAELEZO.
………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
DAR ES SALAAM
AZIMIO namba
64/292 la mwaka 2010 la Umoja wa Mataifa linatamka kuwa huduma ya maji
na usafi wa mazingira ni haki ya msingi ya binadamu na pia ni hitaji
muhimu kwa maisha ya
viumbe hai na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Uwepo wa
rasilimali za maji za kutosha, miundombinu ya usambazaji maji na usafi
wa mazingira, na uwezo wa kiuchumi wa kuwekeza na kuendesha huduma za
maji ni masuala ya msingi na muhimu katika kufikia lengo hilo.
Katika kutekeleza
Sera ya 9 Maji ya Taifa ya mwaka 2002, Wizara ya Maji ina jukumu la
kuhakiki ubora na usalama wa maji katika vyanzo vya maji na mitandao ya
kusambaza maji kwa lengo la kulinda afya za wananchi na mazingira.
Hali ya huduma ya
maji nchini huangaliwa kwa kuzingatia miundombinu ya maji iliyopo na
idadi ya watu wanaopata huduma ya maji, ambapo kwa maeneo ya mijini,
kiwango hicho hukokotolewa kwa kuangalia idadi ya wateja waliounganishwa
kwenye mtandao wa maji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira.
Huduma ya maji
katika maeneo ya mijini hutolewa na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa
Mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa, Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo
na maeneo yanayohudumiwa na Miradi ya Kitaifa.
Mamlaka hizo
zimeendelea kutekeleza miradi ya maji kwa kujenga, kukarabati na kufanya
upanuzi wa miundombinu ya majisafi katika maeneo ya miji hiyo, ambapo
malengo ya Serikali ni kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji
katika Miji Mikuu ya Mikoa kufikia asilimia 95 na Miji Mikuu ya Wilaya,
Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2020.
Malengo ya
Serikali ni kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji
Mikuu ya Mikoa kufikia asilimia 95; na Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo
na Miradi ya Kitaifa kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2020. Kwa upande
wa huduma ya uondoaji wa majitaka, lengo la Serikali ni kuongeza huduma
hiyo kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020.
Hadi mwezi Aprili
2019, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo
yanayohudumiwa na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji
Mikuu ya Mikoa ni asilimia 80 na kwa Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo
na Miradi ya Kitaifa upatikanaji wa huduma hiyo ni asilimia 64.
Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Lindi (LUWASA) inatekeleza Mpango wa
Uboreshaji wa Huduma ya Maji katika Mji wa Lindi (Mradi wa Maji Ng’apa)
unaolenga kutoa huduma ya majisafi kwa wakazi wote waishio eneo la
Manispaa ya Lindi na kuondoa changamoto iliyopo ya wananchi hao
hulazimika kufuata maji umbali mrefu kupitia Virula(Vioski).
Akizungumza
katika mahojiano maalum na Maafisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO)
waliofanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na
Serikali Mkoani Lindi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Lindi (LUWASA), Mhandisi Juma Sudi
anasema anasema mradi huo umekamilika kwa asilimia 92 na hali ya
upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Lindi ni asilimia 75 kwa
sasa.
Mhandisi Sudi
anasema mradi huo ulioanza miaka miwili ulioanza mwaka 2013 na
kutarajiwa kukamilika mwaka 2015, una jumla ya visima saba
vinavyozalisha maji wastani wa mita za ujazo 7500 kwa siku, huku
mahitaji halisi ya huduma ya maji katika Manispaa ya Lindi ni wastani wa
mita za ujazo 5000.
Alisema mwezi
Februari mwaka huu, Serikali ilitoa kiasi cha Tsh. Bilioni 32 kwa ajili
ya kukamilisha hatua mbalimbali zilizosalia katika mradi wa maji wa
Ng’apa na mkandarasi mpya wa mradi huo kampuni ya Shanx Corporation
Company Ltd Ltd tayari ameanza kazi hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa Mwezi Julai mwaka huu.
‘’Serikali
imeweka fedha nyingi sana katika mradi huu,ni uwekezaji mkubwa unaleta
maji katika maeneo yote ya Mji, tunamshukuru sana Rais Dkt, John
Magufuli kwa kutoa fedha hizi amefanya maamuzi magumu, sisi LUWASA
tumejipanga kuhakikisha tunapeleka huduma ya maji katika maeneo yote ya
mjini’’ alisema Mhandisi Sudi.
Aidha Mhandisi
Sudi anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa tatizo la huduma ya maji
katika Mji wa Lindi linatatuliwa kwa haraka, Serikali kupitia Wizara ya
Maji imetoa kiasi cha Tsh Bilioni 2.9 kwa ajili ya kujenga mtandao wa
mabomba katika Mji wa Lindi ili kuhakikisha kuwa wakazi wote wanapata
huduma ya maji wakiwa majumbani kwao.
‘’Mwanzo kabisa
wananchi wa Manispaa ya Lindi walikuwa wakipata huduma ya maji kutoka
katika chanzo cha kitunda ambacho kipo ng’ambo ya bahari ambao ulikuwa
ukizalisha wastani wa mita za ujazo 2000 kwa siku na hata hivyo hakuweza
kukidhi mahitaji, hivyo kukamilika kwa mradi huu wa Ng’apa utakuwa
mkombozi kwa wananchi wa Manispaa ya Lindi’’ alisema Mhandisi Sudi.
Anaongeza kuwa
moja ya kazi inayofanywa na mkandarasi mpya kwa sasa ni pamoja na
kuhakikisha anakamilisha kuweka mfumo katika mtambo ili kusukuma maji
katika visima vyote vilivyopo umbali wa kilometa 13 kutoka katika chanzo
cha Ng’apa pamoja na kukamilisha kazi ndogondogo zilizosalia katika
mradi huo.
Kwa upande wake
Bi Amina Ally Mkazi wa Kilimahewa Manispaa ya Lindi, aliipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano kwani kwa sasa wameokoka na matatizo ya
ukosefu wa huduma ya maji katika maeneo yao kwani hapo awali walikuwa
wakitembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.
‘’Tunaishukuru
Serikali kwani imetutua ndoo kichwani sisi akina Mama, kwa sasa Maji
yanapatikana katika maeneo yetu hatufuatani tena na akina Baba kwa ajili
ya kutupeleka kuchota maji, ambayo yaliyokuwa yakipatikana maeneo ya
porini, ambako kulikuwa na vitisho mbalimbali kwa sisi akina mama’’
anasema Amina.
Anaongeza kuwa
kwa sasa afya zao zimeimarika kwani hawabebi mizigo mizito kichwani ya
ndoo walizokuwa wakisafiri nazo kwa umbali mrefu, kwani Serikali
imerahisisha kwa kiasi kikubwa kwa kufunga mtandao wa mabomba ambayo
yamerahisisha huduma ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kilimahewa,
ambao jiografia yakekwa kiasi imetawaliwa na milima mingi.
Aidha anasema
kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo lao imekuwa nzuri
kwani virula (vioski) vilivyofungwa katika sehemu ya eneo la Kilimahewa
vipo karibu na makazi ya wananchi na maji hayo ni safi na salama kwa
matumizi mbalimbali ya nyumbani.
Naye Bi. Zubeda
Hamadi, Mkazi wa Kilimahewa anasema akina Mama wa eneo la Kilimahewa
wanaipongeza Serikali ya Awamu kwa mageuzi makubwa inayoendelea
kuyafanya katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, ambapo huko
nyuma walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji, ambayo hayakuwa
yakikidhi mahitaji ya nyumbani.
‘’Linapokuja
suala la maji, sisi akina Mama tumekuwa tukipata shida sana na
kutaabika, lakini tunamshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa ujumla
kutuletea maji sasa hivi maji yanatoka kwa wakati, yapo safi na salama
kwa matumizi’’ alisema Bi. Zubeda.
Bi. Elizabeth
Amosi mkazi wa mapoteni Manispaa ya Lindi, anasema akina mama na familia
nyingi sasa zina furaha, huduma ya maji imeokoa ndoa za familia nyingi
kwani wanaume wengi walikuwa wakigombana na wake zao kutokana na
kuchukua muda mrefu wa kwenda na kurudi majumbani wakati wa zoezi la
kutafuta maji.
‘’Waume zetu
walikuwa na wivu sana ni jambo gumu sana kumwambia mume umetumia masaa
2-3 kwa ajili ya kwenda kutafuta maji katika umbali wa karibu kilometa
2-3 kutoka katika majumba yetu, hayo ndio yalikuwa maisha yetu, lakini
kwa sasa shida na matatizo hayo yamekwisha’’ alisema Bi. Elizabeth.
Usimamizi
madhubuti wa rasilimali za maji unahitaji ushirikiano wa wananchi na
wadau mbalimbali ambao ndio watumia maji na wasimamizi wa kwanza wa
rasilimali hizo ikiwa ni mkakati na jitihada za kuongeza upatikanaji wa
huduma ya maji nchini.
No comments :
Post a Comment