Tuesday, March 3, 2020

WAKURUGENZI TANZANITEONE WAPIGWA MARUFUKU KUINGIA NDANI YA UKUTA UNAOZUNGUKA MIGODI YA TANZANITE



Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima akizungumza na waandishi wa habari juu ya maagizo mbalimbali ya Serikali ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite.
…………………………………………………………………………………………………
WAKURUGENZI wa kampuni ya TanzaniteOne na viongozi waandamizi wa kampuni hiyo
wamepigwa marufuku kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kufanya shughuli yoyote wala kusogelea eneo hilo kwa mita 200.
Kampuni ya TanzaniteOne ilikuwa inamiliki kitalu C kwa ubia na serikali kupitia shirika la madini (Stamico) wa kila mmoja asilimia 50 ila leseni yao ilifutwa hivi karibuni na Tume ya madini na kutangazwa bungeni na Waziri wa Madini, Dotto Biteko.
Ofisa madini mkazi wa Mirerani, Daudi Ntalima akizungumza jana ofisini kwake alisema hatua kali za kisheria dhidi ya viongozi hao wa TanzaniteOne zitachukuliwa pindi wakikiuka agizo hilo.
Ntalima aliwataja wakurugenzi wa kampuni ya TanzaniteOne ambao hawatakiwi kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ni Faisal Shabahi na Hussein Gonga.
Aliwataja wafanyakazi wengine wa kampuni hiyo ni mkuu idara ya ulinzi Abubakari Lombe, msimamizi Thomas Mollel, msaidizi idara ya ulinzi Elisamehe Msuya na msimamizi Baraka Mkongo.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wa kitalu B (Opec) na D ambao wanapakana na kampuni ya TanzaniteOne wamefurahia hatua hiyo kwani migodi yao iliyositisha eneo la mitobozano itaendelea na kazi.
Mmoja kati ya wamiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite, Samuel Rugemalira alisema manyanyaso yote yana mwisho ambao huwa mbaya.
“Hongereni sana Rais John Magufuli, Waziri wa Madini Dotto Biteko na Ofisa madini mkazi Mirerani Daudi Ntalima na Tume ya madini kwa ujumla kutokana na uamuzi huo na wakifika hata soko la mbuzi wanakamatwa,” alisema.
Meneja wa kampuni ya Building Utilities, Charles Chilala alisema wakati wa Mungu umefika kwani amewaletea wachimbaji madini ya Tanzanite, Rais John Magufuli ili awatetee na ndivyo alivyofanya.
Hata hivyo, mkurugenzi wa Tanzanite One, Faisal Shabhai alisema hawana taarifa rasmi za kufukuzwa kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani.
“Tunafuatilia lakini kama ni maagizo ya serikali tutatekeleza bila tatizo lolote lile,” alisema Shabhai.

No comments :

Post a Comment