***********************
Na Frank Mvungi- MAELEZO
Serikali imetumia
kiasi cha Shilingi Trilioni 2.957 kutekeleza mradi wa Ujenzi wa Reli ya
Kisasa kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) huku kasi ya utekelezaji
ikiongezeka.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo Jijini Dodoma , Msemaji Mkuu wa Serikali na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Dkt.
Hassan Abbasi amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendelea kama
ulivyopangwa.
“Mradi wa SGR
kwa kipande cha Dar es Salaam na Morogoro umefikia asilimia asilimia 75
wakati kipande cha Morogoro Makutopora Singida kimefikia takribani
asilimia 28”, Alisisitiza Dkt. Abbasi
Akifafanua Dkt.
Abbasi amesema kuwa watanzania wataanza kutumia usafiri huo wa kisasa
kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro mwaka huu wa 2020 hivyo ile
ahadi ya Serikali kwa wananchi itatimia kama ilivyopangwa na kwa wakati.
Kwa upande wa
kipande cha Mwanza-Isaka Dkt.Abbasi amesema kuwa wakati wowote tenda
itatangazwa ili kumpata mkandarasi atakayejenga reli hiyo kwa kipande
hicho ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa mwezi Desemba 2019
Jijini Mwanza kwa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano.
Akizungumzia
baadhi ya wanasiasa wanaobeza juhudi za Serikali kuwaletea wananchi
maendeleo kupitia miradi kama SGR Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali
haitarudi nyuma katika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwa hata
wanaobeza watanufaika na miradi hiyo ikiwemo ndege na umeme.
Kwa upande wa
utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere(JNHPP) ,
ujenzi wa eneo la kuchepusha maji ya mto Rufiji ili ujenzi wa ukuta wa
bwawa uanze limekamilika kwa asilimia mia moja, Aidha bwawa hilo
linatajwa kuwa kati ya mabwawa makubwa 70 ya kuzalisha umeme wa maji
Duniani na kwa Afrika litakuwa la nne kwa ukubwa.
Kwa upande wa
kiwango cha fedha kilicholipwa hadi hasa Dkt. Abbasi amesema kuwa
Shilingi Trilioni 1.275 kati ya Trilioni 6.5 zimeshalipwa ambapo kazi
zote zinaendelea kama ilivyopangwa.
Katika hatua
nyingine Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara zote kesho
Machi 2, 2020 na watatembelea mradi wa SGR ili kujionea utekelezaji
wake.
Akizungumzia
utekelezaji wa mradi wa Chelezo katika Ziwa Victoria Dkt. Abbasi
amesema kuwa umekamilika kwa asilimia 100 na Shilingi Bilioni 32.8
zimeshalipwa na katikati ya mwezi Machi Itaanza kufanya kazi , huku
ukarabati wa MV Victoria umefikia asilimia 89 na Bilioni 14
zimeshalipwa, Wakati MV Butiama ukarabati wake umefikia asilimia 86 na
Bilioni 3 zimeshalipwa kati ya Bilioni 4 zilizotengwa kwa ajili ya mradi
huo.
“ Ujenzi wa meli
mpya na ya kisasa katika Ziwa Victoria itakayokuwa na uwezo wa kubeba
abiria 1200 na Tani 400 za mizigo umefikia asilimia 52 hadi sasa na
unaendelea kutekelezwa kwa kasi kama ilivyopangwa.
Utaratibu wa
Msemaji Mkuu wa Serikali kukutana na vyombo vya habari unalenga kuileta
Serikali kwa pamoja na wananchi kwa kueleza utekelezaji wa miradi ya
maendeleo inayotekelezwa kwa maslahi yao katika maeneo mbalimbali hapa
nchini.
No comments :
Post a Comment