BENKI
ya Taifa ya Biashara (NBC) imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za
Serikali ya awamu ya tano ya kuiwezesha nchi kuingia kwenye uchumi wa
viwanda kwa kuendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati
kiuchumi kupitia uwekezaji katika utoaji wa mikopo na mitaji ya
kibiashara.
Hayo yameelezwa jijini Mwanza na
Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Mwanza, Rodgers Masolwa, wakati wa kikao
maalum cha mashauriano baina ya Serikali na wawekezaji na timu ya
Mawaziri na manaibu Waziri kutoka wizara nane, walio kwenye ziara maalum
kwenye mikoa ya Kanda ya ziwa.
Alisema Benki ya NBC ni Benki
Washirika mojawapo wa wafanyabiashara na Serikali ikiwa na historia ya
kipekee nchini ikiwa ni benki ya kwanza iliyoanzishwa kwa mujibu wa
Sheria Na. 1 ya mwaka 1967, na kupitishwa na Bunge Februari 15, 1967.
“Serikali ilichukua uamuzi wa
kuunda Benki ya Taifa ya Biashara ili iweze kupeleka huduma za kibenki
kwa Watanzania na hivyo kuwawezesha wananchi kiuchumi,” alisema na
kuongeza kuwa NBC ndiyo Benki kongwe Tanzania ambayo inaendelea
kuwatumikia watanzania kwa zaidi ya miongo mitano kwa uaminifu mkubwa.
Alisema kwa sasa benki hiyo
inamilikiwa na makampuni matatu, Kampuni ya ABSA Group Limited
inayomiliki asilimia 55 ya hisa, Serikali ya Tanzania inayomiliki
asilimia 30 ya hisa na International Finance Corporation inayomiliki
asilimia 15 ya hisa.
“Umiliki huu wa hisa umetokea
baada ya Serikali yetu kupitisha uamuzi wa kuibinafisisha benki mnamo
mwaka 2000. Benki inaunga mkono dhamira ya dhati ya Serikali ya kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kuifikisha kuwa nchi yenye uchumi wa
kati ifikapo 2025.”
Aidha, Benki ya Taifa ya
Biashara (NBC) inaunga dhamira hiyo kwa kuwawezesha wafanyabiashara
katika sekta mbalimbali za kiuchumi kwa kutoa mitaji ya fedha ikiwa ni
moja ya benki yenye mitaji mikubwa ya kifedha hapa nchini kuliko benki
zingine.
“Tumewawezesha wafanyabiashara
na wawekezaji kwa kuwapatia mitaji mikubwa kuagiza bidhaa muhimu kutoka
nje ya nchi kama vile sukari na mafuta ya Petroli au kuuza nje ya nchi
mazao ya kilimo,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa benki
hiyo inaendelea kutekeleza ajenda yake ya kidijiti, ikiwekeza maradufu
kwenye mifumo ya teknohama ili kurahisisha utekelezaji wa miamala ya
fedha kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa wateja wake.
Aidha alisema, katika kipindi
cha miaka mitatu iliyopita, Benki hiyo imeshusha riba ambayo imekuwa
ikitoza kwenye mikopo, ambapo tangu mwaka 2016, riba kwa mikopo
isiyokuwa na dhamana imeshuka kutoka wastani wa asilimia 22 hadi 17 kwa
mikopo ya kibiashara ya muda mfupi ambapo riba hiyo imeshuka kutoka
wastani wa asilimia 17 hadi 13.9.
“Kwa mikopo ya muda wa kati na
mrefu, riba imeshuka kutoka wastani wa asilimia 11.2 hadi asilimia 10,
nia yetu ni kuona wateja wetu wanavutiwa na riba ndogo ili waweze
kuendeleza biashara zao kwa ajili ya ustawi wa maisha yao,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu( Uwekezaji) Angelah Kairuki, aliipongeza Benki hiyo
kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiwezesha Serikali katika kutekeleza
miradi mikubwa ya kimaendeleo hapa nchini na kuzitaka benki nyingine za
hapa nchini kuiga mfano wa Benki hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza John Mongela alisema Mwanza ni mkoa wa kimkakati ulio na
mazingira mazuri ya uwekezaji ambapo aliwataka wawekezaji wa ndani na
nje kwenda kuwekeza katika mkoa huo wenye fursa nyingi za kiuchumi.
No comments :
Post a Comment