……………………………………………………………………
Iringa,
Wizara ya Kilimo imekamilisha
maandalizi ya miongozo itakayotumiwa na wakulima wa Mkoa wa Iringa
kuwezesha kufahamu kanuni na teknolojia bora za uzalishaji na usimamizi
wa zao la
mpunga baada ya kuvuna.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
mkutano wadau mjini Iringa jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa
ya Umwagiliaji Marco Ndonde aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
alisema kukamilika kwa miongozo hiyo kutasaidia tija katika kilimo cha
mpunga kuongezeka.
Aliongeza kusema Wizara ya Kilimo
ina jukumu la kuhakikisha uzalishaji na tija vinaongezeka na pia upotevu
unapungua ili kufanya kilimo kuwa cha kibiashara na hatimaye kuwa na
usalama wa chakula, lishe na kuongeza kipato.
“Zao la mpunga ni muhimu nchini
kwa sababu linachukua nafasi ya pili baada ya mahindi kama zao la
chakula na biashara” alisema Ndonde
Alibainisha kuwa takwimu za wizara
ya kilimo zinaonesha kwamba uzalishaji wa mpunga kwa sasa ni wastani wa
tani nne hadi tano kwa hekta kwenye kilimo cha umwagiliaji ambapo
kwenye kilimo kinachotegemea mvua ni wastani wa tani 1.8 hadi 2.
Ndonde aliongeza kusema matokeo ya
tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa uzalishaji unaweza kufikia
wastani wa tani 8.0 kwa hekta endapo kanuni na teknolojia bora za kilimo
zitazingatiwa.
Katika mkutano huo Wizara ya
Kilimo imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na Shirika la
RUDI kwa utekelezaji wa mradi wa RICE unaotekelezwa katika skimu 12 wenye lengo la kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mpunga
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi
huo toka Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) nchini Ajuaye Sigalla
alisema tayari wamefanikiwa kutoa mafunzo ya moja kwa moja kwa wakulima
3000 wa skimu ya Magozi na wengine 9000 wa mkoa wa Iringa kupitia vyombo
vya habari.
Ajuaye alisema Shirika la Chakula
na Kilimo la Umoja wa Mataifa litaendelea kusaidia juhudi za Serikali
katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya
Usalama wa Chakula Josephine Amolo alisema Wizara ya Kilimo tayari
inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mazao Baada ya Kuvuna (National Postharvest Management Strategy), kwa lengo la kupunguza upotevu wa mazao nchini.
“Upotevu wa mazao wakati na baada
ya kuvuna unakadiriwa kuwa kati ya asilimia 30-40 hali inayotakiwa
kudhibitiwa ili wakulima wanufaike na jasho lao” alisema Amolo
Miongozo hiyo imeandaliwa ili
iweze kutumiwa na wakulima wa Mkoa wa Iringa pamoja na maeneo mbalimbali
nchini kuongeza tija kwenye zao la mpunga.
No comments :
Post a Comment