Moja ya vyumba vya kituo cha
ununuzi wa madini kilichopo ndani ya Mgodi wa Almasi wa Williamson
mkoani Shinyanga kitakachotumika kwa ajili ya kununua asilimia tano ya
madini ya almasi katika mgodi huo.
…………………………………………………………………………………
Waipongeza Serikali…
Na Greyson Mwase, Shinyanga
Wafanyabiashara wadogo wa
madini ya almasi mkoani Shinyanga wanatarajia kuuziwa
asilimia tano ya
almasi inayochimbwa na Mgodi wa Almasi wa Williamson kama njia mojawapo
ya kuwainua kiuchumi na kuimarisha masoko ya madini yaliyopo mkoani
Shinyanga.
Akizungumza na wanahabari
kutoka Idara ya Habari MAELEZO tarehe 06 Februari, 2020 kweye kituo
kipya kilichoandaliwa kwa ajili ya kuuzia madini hayo mkoani Shinyanga,
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Joseph Kumburu
alisimulia kuwa kupitia mkutano wa wadau wa madini na Waziri wa Madini,
Doto Biteko uliofanyika mapema Julai mwaka jana, wafanyabiashara wadogo
wa madini waliomba kuuziwa asilimia tano ya madini ya almasi na Mgodi
wa Williamson kama njia mojawapo ya kuimarisha biashara ya madini hayo
na kujiongezea kipato huku Serikali ikipata kodi mbalimbali.
Alisema kuwa, Serikali kupitia
Wizara ya Madini na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ilifanya
mawasiliano na Mgodi wa Williamson ambapo ilikubaliwa kuanza kwa
mchakato ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha awali kitakachotumika
kwa ajili ya kuuza madini husika kwa wafanyabiashara wadogo wa madini
kwa njia ya mnada.
Katika hatua nyingine,
Mhandisi Kumburu alisema Serikali inaandaa utaratibu wa kugawa makinikia
yaliyokuwa yanamilikuwa na Mgodi wa Williamson kwa wachimbaji wadogo wa
madini ili waweze kuyachenjua na kupata madini kwa ajili ya kuyauza.
Akizungumza kwa niaba ya
wachimbaji wa madini katika mkoa wa Shinyanga, Katibu wa Chama cha
Wachimbaji wa Madini Mkoani Shinyanga, Gregory Kibusi aliipongeza
Serikali kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa hatua
iliyochukua katika kuhakikisha wachimbaji wananufaika na rasilimali za
madini.
Alifafanua kuwa tangu
kuanzishwa kwa masoko ya madini, wafanyabiashara wa madini mkoani
Shinyanga wamekuwa wakiuza madini yao kwa uhuru na kulipa kodi
mbalimbali Serikalini huku ulinzi ukiimarishwa kwenye masoko ya madini.
Katika hatua nyingine, Kibusi
aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuacha utoroshaji wa
madini na kuanza kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa.
No comments :
Post a Comment