***********************************
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe.
Paul Makonda leo February 05 amethibitisha kupokea kiasi cha Shilingi
Milioni 600 zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli kwaajili ya ujenzi
wa
Majengo Matano ya Kisasa ya Kituo cha Afya Bunju A kwa lengo la
kusogeza huduma karibu na wananchi.
RC Makonda amesema wakazi wa Bunju
na maeneo ya jirani waliohitajika kufanyiwa Upasuaji walikuwa
wakilazimika kusafiri umbali mrefu hadi Hospital ya Mwananyamala
kwaajili ya huduma hiyo na kutokana na umbali mrefu baadhi yao hufariki
Dunia wakiwa njiani na wengine kutumia gharama kubwa ya usafiri lakini
uwepo wa Kituo hicho sasa wananchi watapata huduma hapo hapo Bunju A.
Aidha RC Makonda amesema ujenzi wa
Kituo hicho unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia leo na utachukuwa
muda wa miezi mitatu hadi kukamilika ambapo ameielekeza Manispaa ya
Kinondoni kuhakikisha inasimamia ipasavyo ujenzi huo.
Pamoja na hayo RC Makonda amesema
kukamilika kwa majengo hayo kutafanya Zahanati ya Bunju A kupanda hadhi
na kuwa Kituo cha Afya ambapo Serikali imepanga kutoa Madaktari na
Wauguzi 58 kwaajili ya kuwahudumia wananchi kituoni hapo.
Hata hivyo RC Makonda amewataka
Wananchi wa Kawe kukaa Mkao wa Kula kwakuwa serikali imepanga kujenga
Kituo Cha Afya Kata ya Kawe ambapo kukamilika kwa Hospital ya Wilaya ya
Mabwepande, Kituo cha Afya Bunju A na Zahanati ya Kawe kutasogeza huduma
kwa wananchi.
Kukamilika kwa Kituo hicho
kutawezesha Wananchi wa Bunju, Mabwepande, Tegeta, Boko, Mbweni, Kawe,
Kunduchi, Madale, Goba na Maeneo ya jirani kuwa na uhakika wa huduma
bora za Afya.
No comments :
Post a Comment