Friday, February 28, 2020

MBOGAMBOGA NA MATUNDA KUPATA SOKO KATIKA NCHI ZA ULAYA



Baadhi ya Sampuli za Mazao ya Kilimo kutoka Tanzania yakioneshwa kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Mbogamboga na Matunda yaliyofanyika katika Maonesho ya Fruit Logistica nchini Ujerumani
Mhe Balozi Dkt Abdallah Possi wa Tanzania nchini Ujerumani akiwa katika picha ya pamoja na Wazalishaji na Wafanyabiashara wa Bidhaa za Mbogamboga na
Matunda kutoka Tanzania walioenda kushiriki Maonesho ya MbogaMboga na Matunda yaitwayo Fruit Logistica yaliyofanyika nchini Ujerumani
Mzalishaji wa Bidhaa za Mbogamboga na Matunda kutoka Tanzania akiongea na watembeleaji kwenye banda la Tanzania katika Maonesho ya MbogaMboga na Matunda yaitwayo Fruit Logistica yaliyofanyika nchini Ujerumani.
***********************
Dar es Salaam – Februari 21, 2020
Makampuni kumi na tano (15) yaliojumuisha wazalishaji pamoja na wasafirishaji wa bidhaa za Mbogamboga na Matunda wajiongezea fursa katika soko la Ulaya kufuatia Ushiriki wao
katika Maonesho ya Kimataifa ya Mbogamboga na Matunda yajulikanayo kama Fruit Logistica 2020 yaliyofanyika tarehe 5 hadi 7 Februari, 2020 mjini Berlin nchini Ujerumani.
Mazao yaliyovutia wanunuzi na wadau wengine katika maonyesho hayo ni pamoja na parachichi, rasiberi, pasheni, ndimu zisizo na mbegu, njegere, snow peas na sugar snaps, maharage machanga (green beans), french
Beans, babycarrots, aina mbalimbali za jamii ya pilipili, viungo vya chakula kama vile tangawizi, nana (mint), kitunguu jani (chives), tikiti maji na mafuta ya parachichi.

Taarifa iliyotolewa nchini na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mheshimiwa Balozi Dkt. Abdallah S. Possi imeeleza kuwa mafanikio ya ushiriki wa Tanzania yamekuwa mkubwa kutokana na makubaliano ya
kimkakati yaliyofikiwa baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na wanunuzi wa mbogamboga na matunda wa nchi za Ulaya, hali inayoleta viashiria chanya vya kupata masoko makubwa. Makubaliano hayo yanatarajiwa
kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi za Ulaya, na hivyo kuvutia uwekezaji katika sekta husika nchini.

Wafanyabiashara wameweza kukutana na kuingia makubaliano na wanunuzi, wabia wa biashara na wadau muhimu kama vile Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) na Taasisi ya Kimataifa ya GLOBALG.A.P inayoshughulikia
viwango vya ubora wa bidhaa za kilimo na mifugo.

Taasisi hizo ni wadau muhimu katika kuwawezesha wazalishaji kutumia njia salama, sahihi na endelevu katika uzalishaji na kuwaunganisha na masoko ya kikanda na
kimataifa. Vilevile washiriki waliweza kujifunza teknolojia za kuzalisha, kusindika, kufungasha, kuhifadhi na kusafirisha mazao ya kilimo ili kukidhi mahitaji ya soko la Ulaya.

“Binafsi nilikutana na mzalishaji kutoka Tanzania ambaye ameingia makubaliano na muwekezaji kutoka Ujerumani. Hii inamaanisha Maonesho haya pia yalikuwa ni fursa kwa wazalishaji wa Tanzania kutafuta wabia wa
biashara” amesema Mhe. Balozi Possi.

Aliendelea kusema kuwa, mkakati wa Ubalozi ni kuandaa na kuratibu matukio maalum kama vile Maonesho, Semina, Mikutano ya ana kwa ana ya wafanyabiashara ili kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wadau
muhimu wa nchi za Ulaya. Vilevile, Ubalozi wa Tanzania uliopo Barlin umekuwa ukihimiza ushiriki wa Tanzania katika Maonesho yanayofanyika nchini humo ili kutafuta fursa zaidi za kibiashara.

Mhe. Balozi ameshauri wazalishaji kuimarisha umoja miongoni mwao ili wapate urahisi wa kuwa na wingi wa bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora vinavyohitajika katika soko kubwa la Ulaya kwa ujumla wake.

Fruit Logistica ni Maonesho makubwa ya matunda na mbogamboga katika Bara la Ulaya ambayo kwa mwaka huu yamevutia ushiriki wa waoneshaji zaidi ya 3,300 kutoka kila hatua ya mnyororo wa ugavi (supply chain)
ambao walitoka katika nchi 93 duniani. Kadhalika, Maonesho yalivutia watembeleaji zaidi ya 78,000 kutoka nchi zaidi ya 135.

Kwa Tanzania, TanTrade kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara ya Kimataifa (ITC) na Taasisi inayosimamia Wadau wa Matunda na Mbogamboga, Maua, Viungo vya chakula na Bidhaa zake (TAHA) iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo ikiwa ni matokeo ya mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa Market Access Upgrade Programme (MARKUP) wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa masoko ili kuongeza mauzo ya nje ya nchi kwa bidhaa za kilimo.

No comments :

Post a Comment