Walimu wa Kilimani Sekondari
wakijumuika kwenye chakula cha mchana walichoandaliwa na kampuni ya
URISINO Ltd kwenye hoteli ya WAG Hill baada ya shule hiyo kufanya vizuri
kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.Picha zote na Baltazar
Mashaka
.Mkurugenzi wa kampuni ya URISINO
Ltd Mhandisi Mnandi Mrutu Mnandi, akizungumza walimu wa shule ya Kilimai
Sekondari kabla ya hafla ya chakula alichowaandalia kuwapongeza kwa
matokeo mazuri ya kidato cha nne.

Walimu wa Kilimani Sekondari
wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa URISINO td Mhandisi
Mnandi Mrutu Mnandi wa saba kutoka kushoto, baada ya hafla ya
kuwapongeza iliyoandaliwa na mkurugenzi na kufanyika WAG Hill Hotel.Wa
sita kutoka kushoto ni Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Ilemela
Emmanuel Malima.
**********************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
MKURUGENZI wa kampuni ya URISINO
Ltd, Mhandisi Mnandi Mnandi amesema uwekezaji wa serikali kwenye sekta
ya elimu utumiwe na walimu wa shule za sekondari za
umma kuvunja ufalme
wa shule binafsi kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na
kuiondolea serikali aibu.
Pia kampuni yake inatambua juhudi
za serikali ya awamu ya tano mbali na kuboresha sekta ya elimu
inaridhishwa na utendaji wa Rais John Magufuli hasa jitihada zake za
kutoa elimu bure na kuhakikisha wanafunzi wa elimu ya juu wanapata
mikopo.
Mhandisi Mnandi alitoa kauli hiyo
kwenye hafla ya kuwapongeza walimu wa Sekondari ya Kilimani kwa matokeo
mazuri ya kidato cha nne na cha pili mwaka jana, hafla iliyofanyika WAG
Hill Hoteli jana.
Alisema atashirikiana na walimu wa
Kilimani na wadau mbalimbali kuweka malengo ya kuondoa sifuri ili
kuiunga mkono jitihada za serikali kuwapa elimu bora watoto wa wananchi
masikini na kuhakikisha hakuna mwanafunzi atapata sifuri kwenye
matokeo ya kidato cha nne mwaka huu.
Mhandisi Mnandi, alisema serikali
ya awamu ya tano imeboresha na kujenga miundombinu ya shule mbalimbali
ikiwemo Kilimani sekondari , kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi
kidato cha nne, huku wanafunzi wa vyuo vikuu wakinufaika na mikopo.
Alisema ili kuunga mkono juhudi
hizo kampuni yake imejenga ofisi ya walimu, kulipa gharama ya Ankara ya
umeme, gharama za kuunganisha huduma ya maji na kugharamia safari za
mafunzo kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri ambapo sasa anakuja na
mkakati wa kuondoa sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne.
“Niliguswa kuwa naweza kujitolea
kuwa balozi wa Rais Magufuli ili kusaidia elimu kwa kutumia kipato
kidogo ninachopata kwenye miradi inayotekelezwa na serikali kupitia
kampuni ya URSINO Ltd ili kuifanya Kilimani sekondari kuwa shule bora
nchini na 2020 bila sifuri Kilimani inawezekana,”alisema.
Mkurugenzi huyo wa URISINO
alieleza kuwa serikali za awamu zilizopita zilifanya mengi lakini Rais
Magufuli ameleta heshima kwenye elimu kwa kuwawezesha watoto wenye
wazazi wasio na uwezo kusoma bure kwa usawa na hivyo walimu waisadie
kuondoa sifuri na kuiondolea aibu hiyo kwenye matokeo ya mitihani.
“ Mwaka 2020 na kwa kuwa hatutaki
kuona sifuri, tuliona tukae na walimu ili kuwapongeza na kuwaondoa
kwenye dhana, tuwatoe katika mazingira yao, tuone tunafanya nini ili
tupate matokeo chanya kwa kuondoa ziro,”alieleza Mhandisi Mnandi .
Alisema walimu wa Kilimani kwa
mbinu za ufundishaji, wana uwezo wa kuvunja utawala wa shule binafsi na
watoto wakifaulu vizuri ni faraja kwa walimu, wazazi na serikali,
wakihitimu masomo yao ya kati na ya elimu ya juu watarudi kuitumikia
serikali na kurejesha fedha zilizotumika kuwasomesha.
Mhandisi Mnandi alisema serikali
inataka maendeleo na akawataka walimu kuacha ubinafsi bali washirikiane
kuwachochea watoto kujifunza kwa bidii ili kuisaidia serikali na
wananchi kuondoa aibu ya sifuri kwenye shule za kata za serikali ili
kuonyesha zinaweza.
Kwa upande wake Afisa Elimu
Sekondari Manispaa ya Ilemela, Emmanuel Malima, lengo la taasisi hiyo ya
umma ni kupata mafanikio ya elimu kwa kuongeza ufaulu , hivyo ushiriki
wa wadau ni muhimu kwani serikali pekee haiwezi.
“Ilemela tumempata ndugu,mdau na
marafiki wa kweli kampuni ya URISINO.Ni kampuni inayojali walimu na
kuwapa hamasa ili kuleta mafanikio ya elimu, kitendo cha kuwaleta hapa
kitawapa nguvu kubwa ya kuongeza matokeo mazuri maana wanaona
wanathaminiwa na hivyo watafanya kazi zaidi,”alisema Malima.
Naye Mwalimu wa Taaluma wa shule
hiyo Atanass Manyika,alisema imekuwa na mafanikio makubwa ikishika
nafasi ya 70 mwaka juzi kati ya shule 241 kimkoa na mwaka jana ilishika
nafasi ya 47 kati ya shule 246 kimkoa ikiwa ni pili kwa shule za umma
wilayani Ilemela.
Alisema Kilimani inaubeba mkoa wa
Mwanza kwa shule za kata za umma ikiwa na wastani wa ufaulu wa asilimia
94.5 ambapo mwaka jana imeongeza ufaulu kwa wanafunzi wanne kupata
daraja la kwanza, daraja la pili 24, la tatu 15, la nne 27 na wanafunzi
4 walipata sifuri.
Mmoja wa walimu wa shule hiyo
Consolata Mosha kwa niaba ya wenzake aliahidi mwakani hawataki sifuri na
malengo yao ni kupata ufaulu wa daraja la kwanza kwa wanafunzi 30 na
hivyo kila mmoja ajitathmini na kuimba “hatutaki ziro Kilimani.”
No comments :
Post a Comment