Mwenyekiti wa shirika la ECLAT
Foundation, Peter Toima akizungumza baada ya kuikabidhi Serikali
madarasa manne ya shule ya msingi Mazinde Toima ya Kijiji cha Loiborsoit
B.
Mwalimu wa shule shikizi ya
Mazinde Kata ya Loiborsoit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Kaika
Elias akiwaonyesha wageni namna alivyokuwa anawafundisha watoto chini ya
mti kabla ya shirika la ECLAT Foundation kukabidhi madarasa manne.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania
Chaula akiwapungia mkono wanafunzi wa shule shikizi ya Mazinde Kata ya
Loiborsoit baada ya kuzindua madarasa manne yaliyojengwa na shirika la
ECLAT Foundation, awali wanafunzi hao walikuwa wanasomea chini ya miti,
kulia ni Mkurugenzi wa shirika la Upendo Dk Fred Heimbach.
****************************
WANAFUNZI 306 wa chekechea, darasa
la kwanza na la pili wa shule shikizi ya Mazinde Kata ya Loiborsoit,
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, waliokuwa wanasomea chini ya miti
wameondokana na adha hiyo baada ya shirika la ECLAT Foundation kujenga
madarasa manne, matundu 16 na ofisi ya walimu.
Awali, wanafunzi wa eneo hilo
wanaosoma elimu ya msingi inawalazimu kutembelea umbali wa kilomita 16
hadi shule ya msingi Loiborsoit A na kilomita 17 mpaka shule ya msingi
Ruvu Remit.
Mwenyekiti wa ECLAT Foundation,
Peter Toima akizungumza jana wakati akikabidhi shule hiyo kwa mkuu wa
wilaya hiyo Zephania Chaula alisema walichukua hatua hiyo baada ya
uongozi wa kijiji hicho kufikisha kwao tatizo hilo.
Toima alisema shirika la ECLAT
Foundation kwa kushirikiana na taasisi ya Upendo ya Ujerumani
wamefanikisha ujenzi wa madarasa manne matundu 16 ya vyoo na ofisi mbili
za walimu.
“Japokuwa katika hayo madarasa
manne wananchi walianza kujenga mawili ambayo hayakukamilika hivyo sisi
tuliyamalizia kwa gharama zetu,” alisema.
Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya
Simanjiro Zephania Chaula aliupongeza uongozi wa ECLAT Foundation kwa
kufanikisha ujenzi huo kwani utapunguza adha ya wanafunzi kutembelea
umbali mrefu wa kwenda shule na kurudi nyumbani.
Alitoa onyo kwa baadhi ya
wanasiasa wa wilaya hiyo wanaozusha maneno potofu dhidi ya shirika la
ECLAT Foundation kwani wameandikishana mkataba na halmashauri ya wilaya
hiyo.
“Wanasiasa uchwara waache maneno
nitawachukulia hatua kali kama na wewe unataka kusifiwa fanya mambo ya
maendeleo tutakusifia na wewe siyo kusababisha maneno ya uchochezi
yasiyo na maana,” alisema.
Ofisa elimu ya msingi wa
halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Silvanus Tairo alisema shule hiyo
itasajiliwa hivi karibuni kwa jina la shule ya msingi Mazinde Toima na
kuondokana na shule shikizi.
Mwalimu wa shule hiyo Kaika Elias
alisema wanafunzi wote 306 alikuwa anawafundisha peke yake kwani mwalimu
aliyekuwa anashirikiana naye aliondoka eneo hilo.
Mwalimu Elias alimshukuru Toima
kwa kujenga shule hiyo kwani wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu
kwenda kusoma shule za jirani.
Mwanafunzi wa darasa la kwanza
Samwel Alamayani alimshukuru Toima kwa kujenga madarasa hayo kwani
walikuwa wanasoma chini ya miti hivyo upepo vumbi na mvua zilikuwa
kikwazo kwao.
Mwanafunzi wa darasa la pili
Rachel Elia alisema baada ya shule hiyo kujengwa hawatakwenda zaidi ya
kilomita 32 kwenda shule za jirani na kurudi nyumbani kila siku.
No comments :
Post a Comment