Sunday, February 2, 2020

DKT KALEMANI AZINDUA MATUMIZI YA GESI ASILIA UDSM



Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa tatu kutoka kulia) akisikiliza maelezo ya namna mtambo wa gesi asilia uliopo eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unavyofanya kazi wakati wa hafla ya uzinduzi wa matumizi ya gesi asilia chuoni hapo, Februari 1, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akikagua migahawa iliyounganishiwa gesi asilia iliyopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na baadhi ya nyumba zilizounganishiwa nishati hiyo katika eneo la Mwenge Mlalakuwa, Februari 1, 2020.
………………………………………………………………………………………………
Veronica Simba – Dar es Salaam
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amezindua matumizi ya gesi asilia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), leo Februari 1, 2020 ambapo kwa hatua hiyo ya awali,
migahawa minne chuoni hapo imeanza kutumia huduma hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Dkt Kalemani amesema dhamira ya serikali ya kutumia gesi asilia inayopatikana nchini kwa maendeleo ya Taifa iko palepale tofauti na wanavyoamini baadhi ya watu kuwa nishati hiyo haipewi kipaumbele katika matumizi yake.
“Gesi hii tutaendelea kuitumia sambamba na matumizi mengine ya nishati ikiwemo kuzalisha umeme ili kujenga uchumi wa viwanda.”
Akifafanua, Waziri amesema mathalani, takribani asilimia 80 ya gesi inayozalishwa kwa sasa hapa nchini inatumika kuzalisha umeme na kwamba umeme unaozalishwa na gesi asilia kwa Tanzania ni asilimia 57 sawa na megawati 892, akibainisha kuwa huo ni mchango mkubwa sana wa sekta ya nishati kwenye uchumi wa nchi.
Hata hivyo amesema, pamoja na kiasi kikubwa cha gesi kutumika kuzalisha umeme, kiasi kingine kinatumika katika shughuli nyingine mbalimbali ambazo ni pamoja na kuunganisha viwandani, kwenye makazi ya watu na migahawa kwa ajili ya kupikia pamoja na kutumika katika magari.
Katika kuweka msisitizo wa matumizi ya gesi asilia katika magari, Dkt Kalemani ametoa agizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati pamoja na watendaji wakuu wa Taasisi zote zilizo chini yake, kuhakikisha magari yote yanayoagizwa kuanzia sasa, yawe ni yale yenye mfumo wa kutumia gesi badala ya petroli na dizeli.
Akizungumzia faida za kutumia gesi asilia kwa shughuli mbalimbali, amesema ni pamoja na utunzaji wa mazingira kutokana na uwepo wa kiasi kidogo cha hewa ya ukaa pamoja na  gharama nafuu kwa mtumiaji ambayo inakadiriwa kuokoa asilimia 40 ikilinganishwa na gharama za aina nyingine za nishati.
Kuhusu mipango ya serikali kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya kupikia, Waziri ameeleza kuwa, mpango huo umeanza kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani na baadaye mikoa mingine pia itafikiwa.

No comments :

Post a Comment