*****************************
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.
Joachim Wangabo amewataka wananchi wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha
wanawaepuka wanasiasa wenye lengo la kuvuruga amani na mshikamano wa
wanarukwa, kusababisha mifarakano baina ya wananchi na hatimae kushindwa
kufanya shughuli za kimaendeleo katika mkoa.
Amesema kuwa umuhimu wa kuilinda
amani unatokana na upekee wa mwaka 2020 kwakuwa ndio mwaka wa uchaguzi
mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais, na kutahadharisha kuwa katika
kuelekea kwenye uchaguzi huo kutakuwa na harakati kadhaa za kisiasa, na
kuwataka wanarukwa kuwaepuka wanansiasa wasioitakia mema nchi yetu.
Mh. Wangabo ameyasema hayo
alipokuwa akitoa salamu zake za mwaka mpya katika ibada ya kuukaribisha
mwaka 2020 iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristu Mfalme,
mjini Sumbawanga.
“Tuwaepuke wanasiasa wa namna hiyo
ili tudumishe umoja wetu, amani yetu na mshikamano wetu, Tusikubali
kuyumbishwa na wanasiasa katika kipindi cha mwaka huu, ni mwaka wa
uchaguzi kila mtu anataka kupitia migongo ya wananchi ya wanarukwa ili
kutimiza matakwa yake,” Alisema.
Aidha, aliwataka wananchi hao
kuzingatia kuwa miaka yote wanarukwa wamekuwa wamoja na hawajawahi
kuyumbishwa na pia maisha baada ya uchaguzi na hivyo kutoshawishiwa kwa
urahisi na watu wachache wanaotaka kutekeleza matakwa yao yasiyoitakia
mema amani iliyopo.
No comments :
Post a Comment