Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula
akizungumza na Wahitimu wa kada ya Famasi (Hawapo pichani) wakati wa
warsha fupi ya kutoa vyeti vya kuhitimu na usajili iliyofanyika katika
ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.
Mfamasia Mkuu Bw. Daud Mmasi
akizungumza na wahitimu wa kada ya Famasi (Hawapo pichani) wakati wa
warsha fupi ya kutoa vyeti vya kuhitimu na usajili iliyofanyika katika
ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula
akimkabidhi mmoja wa wahitimu wa kada ya Famasi cheti cha taaluma pamoja
na usajili katika warsha iliyofanyika jijini Dodoma.
Wahitimu wa kada ya Famasi wakila
kiapo kilichoongozwa na msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth
Shekalaghe katika warsha ya kuwatunuku vyeti vya taaluma na usajili
iliyofanyika leo jijini Dodoma.
*******************************
Na WAJMW-DOM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt.
Zainab Chaula amewasihi wahitimu wa kada ya famasi kutoka vyuo
mbalimbali nchini na nje ya nchi kuheshimu na kufuata misingi na
miongozo ya
taaluma hiyo ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Chaula amesema hayo mapema
leo wakati alipohudhuria warsha fupi ya kuwatunuku vyeti vya kuhitimu na
usajiri wahitimu zaidi ya 100 waliohitimu shahada ya Famasi katika vyuo
mbalimbali nchini.
“Ninaomba mkawe wanyenyekevu mkiwa
maeneo yenu ya kazi, kuzingatia kanuni na misingi ya taaluma ni jambo
muhimu la kufuata kwa kila mmoja wetu, nidhamu mahala pa kazi huleta
umakini katika kazi yako, jamii inawategemea ili muweze kutoa huduma
nzuri kwa wananchi”. Amesema Dkt. Chaula.
Dkt. Chaula ameendelea kusisitiza
kuwa taaluma hiyo ni muhimu sana nchini kwani wagonjwa wanategemea
kupata dawa sahihi ambazo zitatolewa na wafamasia hao ili ziwasaidie
kupona maradhi yanayowasumbua.
Aidha, Dkt. Chaula amewataka
Wahitimu hao kushirikiana kwa karibu na madaktari pamoja na wahudumu
wengine wa afya wakiwemo manesi ili waweze kusaidia katika kutoa huduma
bora za afya na kusaidia wananchi kupata nafuu na kupona kabisa maradhi
yanayowasumbua.
Kwa upande wake Msajili wa Baraza
la Famasi nchini Bi. Elizabeth Shekalaghe amewataka wahitimu hao kwenda
kuisaidia jamii na kuziba baadhi ya mapengo ya taaluma hiyo ambayo ina
watumishi wachache na uhitaji ni kubwa nchini ambapo hivi sasa Tanzania
ina wafamasia takribani 1200 waliosajiliwa na Baraza hilo nchi nzima.
No comments :
Post a Comment