
Mkuu wa taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma, Sosthenes
Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini
kwake jijini Dodoma leo wakati akitoa taarifa ya kuokoa mamilioni ya
fedha.
…………….
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma imefanikisha kuokoa kiasi cha shilingi
milioni mia moja hamsini na mbili laki tatu thelathini mia tatu
themanini na mbili na senti ishirini na tano (152,330,382.25) baada ya
kufuatilia utekelezaji wa
miradi ishirini na moja (21) yenye thamani ya
shilingi bilioni sabini na sita milioni mia tatu ishirini mia tano
arobaini na mbili na senti tisini na sita (76,320,268,542.96) inayofanyika mkoani Dodoma.
Fedha hizo zimeokolewa kwa
kuwezesha kiasi cha shilingi milioni arobaini na mbili laki mbili tisini
na nne mia tano themanini na mbili na senti ishirini na tano
(42,294,582.25) zilizotumika kwa kazi nyingine kurejeshwa na kutumika
kwenye mradi husika na kuuwezesha kuendelea, na shilingi milioni mia
moja na kumi elfu thelathini na tano na mia nane (110,035,800/=) zilikatwa kama faini kwa mkandarasi kwa kuchelewesha kazi kukamilika ndani ya wakati.
Ufuatiliaji wa miradi hiyo katika
sekta za elimu, afya, maji na ujenzi ulifanyika katika robo ya Oktoba
hadi Disemba, 2019 ili kukagua iwapo thamani halisi ya fedha ilifikiwa
ambapo ushauri na elimu ilitolewa katika maeneo ambayo yalikuwa na
mapungufu yanayorekebishika. Aidha, miradi miwili ya ujenzi katika shule
za sekondari yenye thamani ya shilingi milioni mia nne sabini na moja
na laki sita (471,600,000/=) imeonekana kuwa na viashiria vya
udanganyifu na rushwa katika matumizi ya fedha hivyo tunaichunguza iwapo
kuna jinai.
Katika eneo la uelimishaji ili
kuhamasisha jamii kushiriki kivitendo katika kukemea na kuzuia vitendo
vya rushwa, TAKUKURU iliweka mkazo zaidi katika elimu dhidi ya vitendo
vya rushwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, kampeni ya vunja ukimya: kataa rushwa ya ngono na
kampeni ya UTATU inayopinga vitendo vya rushwa katika eneo la askari wa
usalama barabarani, ambapo vipindi arobaini na tatu (43) vya redio na
runinga vilirushwa, mikutano ya hadhara themanini na nne (84) na semina
themanini na tisa (89) zilifanyika atumishi wa umma na ambapo washiriki
ni wananchi na makundi ya wanasiasa, wanatumbi, sekta binafsi.
Pia katika kukazia makuzi ya
maadili mema kwa vijana klabu mia moja na tatu (103) za wapinga rushwa
katika shule za msingi, sekondari na vyuo zilifunguliwa na klabu mia
ishirini na mbili (122) zilitembelewa na kuimarishwa.
Katika eneo la kupambana na
rushwa, tulikamilisha uchunguzi wa majalada kumi na nne (14) na kufungua
mahakamani kesi saba (7) zilizowahusu viongozi wa Ushirika wa akiba na
kukopa, watumishi wa halmashauri na watu binafsi. Jumla ya malalamiko
mia moja arobaini na saba (147) ya rushwa na makosa yahusianayo
yalipokelewa ambapo maeneo yaliyoongoza ni Ardhi (asilimia 31.4);
Serikali za mitaa (asilimia 22.9); Polisi (asilimia 14.3); Vyama vya
siasa (asilimia 11.4); Mahakama (asilimia 4.3); Elimu (asilimia 4.3) na
sekta zilizosalia asilimia 11.4. Ni muhimu wahusika wa sekta
zinazolalamikiwa sana wajitafakari na kujirekebisha Kwa robo ya Januari
hadi Machi, 2020, pamoja na majukumu mengine TAKUKURU itaendelea
kuhamasisha jamii kuvunja ukimya na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa
ya ambapo tunatarajia kuzishirikisha klabu za wapinga rushwa katika
kutoa elimu hiyo.
Pia tutashirikiana na wadau
wengine, likiwemo Jeshi la Polisi, kutangaza kampeni ya UTATU na
kuhamasisha wananchi kutumia TAKUKURU App kutoa taarifa za vitendo vya
rushwa na jinai nyingine. Vile vile, kwakuwa huu ni mwaka wa uchaguzi
mkuu, tunaendelea kutoa elimu ya kujiepusha na kuzuia rushwa kwenye
uchaguzi, kukusanya taarifa na kupambana kwa mujibu wa sheria na yeyote
atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa inayohusiana na
uchaguzi na nyingine.
Aidha, leo tunatarajia kuwafikisha
mahakamani watu wanne kwa makosa mbalimbali ya rushwa. Wa kwanza ni Bw.
James Gebu Kwangulija mwenye umri wa miaka ishirini na saba (27),
mkazi wa Kikuyu Jijini Dodoma na ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu
wa shahada ya kwanza ya ualimu wa masomo ya sanaa katika Chuo Kil kosa
la kujaribu kutoa hongo ya shilingi laki tisa (900,000/=) kwa Afisa
mitihani wa chuo hicho ili asaidie kuongeza ufaulu (GPA) za wanafunzi
wenzake sita (6), kinyume na kifungu cha 15 (1)b cha Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na rushwa sura ya 329 marejeo ya 2018, Wa pili
tutakayemfikisha mahakamani kwa makosa ishirini na sita (26) ya kuomba
na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1)b cha Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na rushwa sura ya 329 ni Bw. Samwel Mosses Tuppah mwenye umri
wa miaka thelathini na tisa (39), mkazi wa Tegeta Mivumoni,
Kinondoni DSM ambaye ni Mchunguzi wa kuzuia maudhui yasiibiwe (Piracy
Investigator) wa kampuni ya Multichoice Tanzania Limited (DSTV) ya
Jijini DSM. Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba kati ya mwaka 2017 hadi
2019, Bw. Tuppah aliomba na kupokea jumla ya shilingi milioni tano
(5,000,000/=) kama hongo kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Feisal Cable
Networks ya Jijini Dodoma ili asichukue hatua kwa kampuni hiyo ya Dodoma
kwa tuhuma ya kuiba maudhui ya DSTV.
Mwisho tutawafikisha mahakamani
Bw. Rainer Alanus Kapinga mwenye umri wa miaka arobaini na tano (45)
ambaye alikuwa Mganga Mkuu wa wilaya ya Bahi na Bw. Raymond Gaspary
Mhegele mwenye umri wa miaka thelathini na tatu (33) ambaye ni Afisa
TEHAMA wa halmashauri ya wilaya ya Bahi kwa makosa ya matumizi mabaya ya
mamlaka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na
rushwa sura ya 329, kughushi na kutoa nyaraka za uongo kinyume na Sheria
ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 marejeo ya 2002. Uchunguzi wetu
umeonyesha kwamba mwaka 2017 watuhumiwa walighushi na kuwasilisha kwa
mwajiri wao stakabadhi za kiasi cha shilingi milioni tatu na laki tano
(3,500,000/=) wakidai wamenunua vifaa vya TEHAMA huku wakifahamu kwamba
ni uongo.
TAKUKURU inawaasa watu wote
kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani mkono wa sheria ni mrefu.
Tunawashukuru wananchi kwa kuendelea kutupa taarifa na tunazidi kuwasihi
kuwa sehemu ya mapambano haya ili kuleta tija na kuboresha hali ya
maisha ya watanzania wote.
No comments :
Post a Comment