
********************************
Na Mwandishi Maalum
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2019 imeokoa zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 1873 .
Hayo
yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed
Janabi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma za
matibabu ya moyo zilizotolewa na
Taasisi hiyo kwa mwaka 2019.
Prof. Janabi alisema kama
wagonjwa wote hao 1873 waliofanyiwa upasuaji hapa nchini wangetibiwa
nje ya nchi Serikali ingetumia zaidi ya shilingi bilioni 56, lakini kwa
wagonjwa hao kutibiwa hapa nchini matibabu yao yamegharimu kiasi cha shilingi bilioni 28.
“Fedha
za matibabu ya wagonjwa hawa zimelipwa kupitia bima zao mbalimbali za
matibu, wagonjwa wenyewe kujilipia, wadau mbalimbali kuchangia matibabu
ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kulipa na Serikali kugharamia matibabu ya wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu”, .
“Utoaji wa huduma zetu umeongezeka
kwa asilimia 29 ukilinganisha na mwaka 2018.Tumefanya upasuaji mkubwa
wa kusimamisha moyo kwa wagonjwa 464 ambapo vifo vilikuwa asilimia 6 ya
wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji”, alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema Wagonjwa
waliofanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kwa njia ya tundu dogo
linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab
(Catheterization laboratory) walikuwa 1409, wagonjwa sita walipoteza
maisha ambapo ni sawa na asilimia 1.3.
Aidha Prof. Janabi alisema kwa
mwaka 2019 waliona wagonjwa 108,946 wenye matatizo ya moyo. Kati ya
wagonjwa hao wagonjwa wa nje walikuwa 105,142 na wagonjwa waliolazwa
walikuwa 3,804 huku wanaume wakiwa ni asilimia 52 na wanawake asilimia
48.
Wagonjwa wengi wanaotibiwa katika
Taasisi hiyo ni wale wenye matatizo ya Shinikizo la juu la damu,
kutanuka kwa moyo, magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, magonjwa ya valvu
za moyo yanayotokana na maambukizi ya bakteria, umeme wa moyo
kutokufanya kazi vizuri kwa muda mrefu, tatizo la ghafla la umeme wa
moyo kutokufanya kazi vizuri au kwa haraka na mishipa ya damu ya moyo
kuziba.
Alimalizia kwa kuwaahidi
watanzania kwa mwaka wa 2020 wataendelea kutoa huduma bora na za
utaalamu wa hali ya juu kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo,
kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari na
kwa wananchi walioko nje ya mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kupata
huduma za Taasisi hiyo kupitia Hospitali zao za Mikoa na Wilaya.
No comments :
Post a Comment