
Kumekuwa na taarifa kwenye
mitandao ya kijamii ikiwemo Jamii Forum ambazo bila
kuchanganua
zinatuhumu kwamba Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila inasababisha
vifo kwa wagonjwa. Uongozi wa hospitali unapenda kuwahakikishia Umma wa
Watanzania kwamba habari hizi si za kweli na hazitoi picha halisi ya
huduma ambazo zinazotolewa hospitalini hapa.
Takwimu tulizonazo zinaonyesha
kwamba wagonjwa wanaotibiwa MNH- Mloganzila wameongezeka katika makundi
yote. Wagonjwa wa nje wameongezeka kutoka 17,115 katika kipindi cha
robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 kufikia wagonjwa 25,493 katika
kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 ambalo ni ongezeko la asilimia
48.8. Aidha, wagonjwa wanaotibiwa na kulazwa wameongezeka kutoka 1,459
katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia
wagonjwa 2,795 katika kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 ambalo ni
ongezeko la asilimia 91.6.
Wakati huo huo idadi ya vifo
(mortality rate) ikipungua kutoka asilimia 14.9 iliyokuwepo katika
kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba, 2018 na kufikia asilimia
10.4 katika kipindi cha Julai-Septemba 2019.
Aidha, takwimu za MNH-Upanga
zinaonyesha kwamba katika kipindi cha robo mwaka cha Julai hadi Septemba
2018 wagonjwa waliolazwa walikua ni 12,375 ambapo kulitokea vifo 1,000
(mortality rate) ambayo ni asilimia 8.1. Vilevile katika kipindi cha
Julai hadi Septemba 2019 MNH Upanga ililaza wagonjwa 17,230 na kati ya
hao vifo vilikua 1,673 ambayo ni asilimia 9.7(mortality rate).
Hivyo basi takwimu kati ya
MNH-Mloganzila na MNH-Upanga za asilimia ya wagonjwa waliofariki
hazitofautiani sana ambapo MNH-Upanga ni asilimia 9.7 wakati
MNH-Mloganzila ni asilimia 10.4 katika robo ya Julai – Septemba, 2019.
Hatua hii inaonyesha juhudi ambazo zinafanyika za kuboresha utoaji wa
huduma katika MNH- Mloganzila zinazaa matunda.
Moja ya sababu ambazo imeelezwa
na mtoa taarifa kwamba Madaktari wanaotoa huduma MNH-Mloganzila ni
wanafunzi waliopo katika majaribio si za kweli, hivyo tungependa
kufafanua kwamba Hospitali ya MNH-Mloganzila ina Madaktari Bingwa 52,
Madaktari wa kawaida 50 na kwa sasa ina Madaktari tarajali 53.
Licha ya Madaktari Bingwa hawa
walioajiriwa MNH-Mloganzila kutoa huduma lakini pia wanashirikiana na
Madaktari Bingwa kutoka MNH-Upanga katika kutoa huduma hapa
MNH-Mloganzila, vilevile hospitali hii ina madaktari wawili waliobobea
wenye hadhi ya Profesa kutoka Korea nao wapo wanatoa huduma.
Hivyo sio kweli kwamba madaktari
ambao wapo mafunzoni wanafanyakazi bila usimamizi kwani hospitali
imeweka utaratibu wa kila mgonjwa anayefika kupata huduma anaonwa na
Daktari Bingwa kwa ajili ya maamuzi.
Wakati uongozi wa hospitali
ukifanyia kazi tuhuma na malalamiko yaliyotolewa juu ya utoaji huduma
katika taarifa hii, tunapenda kuutarifu Umma kwamba tangu MNH ipewe
dhamana ya kusimamia hospitali hii, tumejielekeza katika kutatua
changamoto zilizokuwepo katika utoaji huduma na kwa kiasi kikubwa
imeonyesha mafanikio ambayo yanaonyesha kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa
na pia kuna ushuhuda wa wagonjwa ambao wametibiwa na kuridhika na
utoaji wa huduma zetu.
Tunawahakikishia Watanzania
kwamba huduma zinazotolewa katika Hospitali ya MNH-Mloganzila
zimeboreshwa na tunawakaribisha Watanzania wenye jukumu la kuelimisha
jamii waje kuzungumza na wataalam na waone jinsi huduma zinavyotolewa
ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa jamii.
Imetolewa na
Prof. Lawrence M. Museru
Mkurugenzi Mtendaji,
MNH-Mloganzila.
No comments :
Post a Comment