Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali itaendelea
kuimarisha ufuatiliaji wa elimu kwa kuboresha Idara ya Uthibiti Ubora wa
Shule kwa lengo la
kuhakikisha Elimu inatolewa kwa kiwango ili kupata
matokeo na wahitimu bora.
Profesa Ndalichako amesema hayo
ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma alipokuwa akitoa tathmini ya matokeo
ya darasa la nne, kidato cha pili na nne ambapo amesema lengo la
Serikali ni kuhakikisha inazifikia shule na kuwa karibu nao zaidi na
tayari wathibiti ubora 400 wameajiriwa.
“Katika kuimarisha uthibiti ubora
wa shule mwaka huu tumeajiri wathibiti ubora 400 ili kuimarisha utendaji
wa idara hii na kuwafikia wadau na shule ili kuziwezesha kuboresha
ufundishaji na ujifunzaji,” amesema Profesa Ndalichako.
Aidha, Waziri Ndalichako amesema
matokeo haya ni ya kwanza tangu kuanza kutekeleza Mpango wa Elimu bila
Malipo ambao baadhi ya watanzania hawakuamini kama ungefanikiwa lakini
matokeo yameonyesha mafanikio na ufaulu umeongezeka kutoka 67.91% mwaka
2015 hadi kufikia 80.65% mwaka 2019.
Wakati huo huo Ndalichako kwa
niaba ya Wizara amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani
yao pamoja na walimu kwa kuwa bega kwa bega na wanafunzi wao na
kuwawezesha kupata matokeo mazuri.
No comments :
Post a Comment