Diwani wa
kata ya Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui akishangaa baada ya
spika kuzimwa wakati akiwatangazia wananchi kuhusu taarifa za kuzuiwa
kwa mkutano wao katika Soko la Maganzo wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga leo Januari 2,2020. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Katibu wa
Jumuiya ya Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui Abdul Ngolomole ambaye
ni Diwani wa Kata ya Songwa (CCM) akiwaomba wananchi kuwa watulivu
baada spika kuzimwa baada ya kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara.
Katibu wa
Jumuiya ya Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui Abdul Ngolomole ambaye
ni Diwani wa Kata ya Songwa (CCM) akizungumza kwenye mkutano na
waandishi wa habari ‘Press Conference’ baada ya kuzuiwa kufanya mkutano
wa hadhara uliolenga kujadili kuhusu Makinikia ya almasi yaliyopo
katika Mgodi wa Mwadui.
Katibu wa Jumuiya ya Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui Abdul Ngolomole akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari.
Diwani wa
kata ya Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui akizungumza kwenye
mkutano na waandishi wa habari ‘Press Conference’ baada ya kuzuiwa
kufanya mkutano wa hadhara uliolenga kujadili kuhusu Makinikia ya almasi
yaliyopo katika Mgodi wa Mwadui.
Kulia ni William Luhende Jijimya wa kata
ya Mondo akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ‘Press
Conference’ baada ya kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara uliolenga
kujadili kuhusu Makinikia ya almasi yaliyopo katika Mgodi wa Mwadui.
Diwani wa kata ya Mwadui Luhumbo Paul
Magembe akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari ‘Press
Conference’ baada ya kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara uliolenga
kujadili kuhusu Makinikia ya almasi yaliyopo katika Mgodi wa Mwadui.
Mchimbaji mdogo wa madini akizungumza na waandishi wa habari.
Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Katika hali isiyotarajiwa mkutano wa wananchi wanaozunguka mgodi wa almasi wa Williamson Diamond LTD ‘Mgodi wa Mwadui’ ulioandaliwa na Madiwani wanaozunguka mgodi huo kujadili hatima ya Masalia ya mchanga wa madini ya almasi ‘Makininikia’umepigwa
marufuku dakika chache kabla ya mkutano kuanza ambapo ghafla viti
viliondolewa huku spika zikizimwa wakati diwani wa Maganzo Lwinzi Mbalu
Kidiga akizungumza.
Tukio
hilo limetokea leo Alhamis Januari 2,2020 majira ya saa sita mchana
ambapo madiwani wa kata zinazozunguka mgodi huo pamoja na wananchi
waliokusanyika katika soko la kata ya Maganzo ‘Mji wa Maganzo’ wilayani
Kishapu mkoani Shinyanga kutakiwa kutawanyika mara moja kwa madai kuwa
ni ‘Order’ Agizo/Amri kutoka juu.
Tukio la
kuzuiwa kufanyika mkutano wa hadhara ni kielelezo cha mgogoro uliozuka
kati Wachimbaji wadogo wanaozunguka mgodi wa Mwadui na Chama cha
Wachimbaji Madini mkoa wa Shinyanga ‘Shinyanga Region Miners Association – SHIREMA’
siku chache baada ya Mgodi wa Williamson Diamond Ltd kuamua kutoa
mchanga wa Makinikia ya Almasi bure kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Katika
kikao hicho pia kilihudhuriwa pia na Waziri wa Madini Dotto Biteko baada
ya wachimbaji kuomba wapewe makinikia ili kuondoa mgogoro kati yao na
mgodi ambapo SHIREMA walipewa jukumu la kusimamia utaratibu mzuri wa
kugawa mchanga huo.
Akitoa
taarifa kwa wananchi kuhusu kusitishwa kwa mkutano huo leo Januari
2,2020 wakati tayari viti na meza kuu vikiwa vimetolewa kwenye soko la
Maganzo palipotakiwa kufanyika mkutano wa hadhara, Diwani wa kata ya
Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madiwani
wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui, ghafla spika zilizimwa na watu
ambao hawakujulikana mara moja hali iliyozua gumzo kwa wananchi
waliokuwa wamejiandaa kusikiliza nini kinajili kwenye mkutano huo.
Kidiga
alisema wameahirisha kufanya mkutano huo hadi siku nyingine kutokana na
Amri kutoka juu iliyowataka waahirishe mkutano huo vinginevyo watawekwa
ndani.
Alisema
chanzo cha kuzuiwa kufanya mkutano ni watu wachache waliojipanga
kuhujumu uchumi wa watu wa Maganzo ili wapate asilimia za chini kwenye
makinikia huku akibainisha kuwa yeye kama diwani hakubali.
“Ndugu
wananchi mmeiona sura ya hapa, sura ya hapa haijakaa vizuri tulikuwa
tumeweka viti kwa ajili ya mkutano wa hadhara lengo na madhumuni ilikuwa
ni kuzungumza changamoto zilizopo katika hata hii na kata za jirani lakini cha kushangaza hapa meza zimetolewa.
Mkutano wetu ulikuwa ni mzuri tu wa kupeana habari haukuwa na ashki
yoyote.,huu mkutano umeahirishwa..kwa Kiswahili kingine Tumezuiwa”,alieleza Kidiga.
“Nimezuiwa
lazima niseme ukweli..Huu mkutano wangu upo ndani ya kisheria na nina
mamlaka ya kuitisha mkutano bila kuuliza kwa mtu yeyote,sheria na katiba
ya nchi inanilinda. Kwa Order kutoka Juu mkutano
huu nimeambiwa nisifanye mara moja..Sasa mara moja maana yake huwezi
kuuliza lakini wanasema chelewa chelewa mwishowe ukweli utaonekana.
“Sisi
hapa ni wakweli,tunataka tuzungumze ukweli na ukweli wenyewe ni kutetea
watu walio chini wapate maslahi siyo waingilie watu wachache,hiyo
biashara haipo.”,alisema Kidiga huku akishangiliwa na wananchi.
“Mmetuchagua
kwa ajili ya kusimamia haki zenu siyo baadhi ya watu wanufaike,hiyo
biashara haipo..Tumezuiwa sawa,sisi tuko chini ya sheria hakuna mtu
aliye juu ya sheria lakini ilikuwa halali yetu tufanye mkutano huu na
madiwani wa kata jirani, tulikuwa tumepanga tuzungumzie kuhusu Makinikia
basi.
Tumeambiwa
tukifanya mkutano tutawekwa ndani na tukiendelea ku – force udiwani
ndiyo basi tena. Ndani tutakwenda kwani waliomo ndani siyo watu?.
Tukiwekwa ndani basi Rais Magufuli atakuja kutuwekea dhamana kwani
tunatetea wanyonge. Tumetii amri,tutafanya mkutano siku nyingine
.Nilitaka niseme hilo ili msisambae kienyeji kwani tuliwaita kwenye
mkutano na wengine mmetoka mbali”,alieleza Kidiga.
Kidiga
alisema SHIREMA imekuwa ikifanya vikao vyake na kufanya mambo bila
kuwashirikisha madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui akidai
kuwa haina nia nzuri ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini wilayani
Kishapu.
Hata
hivyo baada ya mkutano huo uliokuwa umezungukwa na askari polisi
wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wilaya ya Kishapu Emmanuel Galiyamoshi
kuahirishwa,Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui,waliamua kufanya
mkutano na waandishi wa habari ‘Press Conference’ ili kueleza lengo la mkutano wao.
Katibu wa
Jumuiya ya Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui Abdul Ngolomole ambaye
ni Diwani wa Kata ya Songwa (CCM) alisema hawakubaliani na kitendo cha
SHIREMA kumpatia Mkandarasi anayesafirisha mchanga wa madini kutoka
Mwadui kupewa asilimia 75 ya mauzo ya almasi na wachimbaji wadogo kupewa
asilimia 15.
“Tunataka
Mkandarasi wa kusafirisha makinikia atangazwe hadharani kupitia zabuni
kwani mkandarasi aliyepo sasa ni Mkandarasi wa mfukoni ambaye ni Junior
Construction ya Mbunge wa Kishapu Suleiman Nchambi,ni mkandarasi ambaye
amebuniwa na SHIREMA ,huyu ni mtu mkubwa sana, mamlaka zipo lakini
kwanini hazisemi?. Sisi tunapotaka kufanya mkutano kuwaeleza wananchi
ukweli tunaonekana tunataka kuzuia maslahi ya watu flani”,alisema Ngolomole.
“Baada
ya kulalamikia hizo asilimia 15 SHIREMA wameongeza asilimia kwamba
mchimbaji mdogo apate asilimia 37.5 ambayo haiwasaidii wanyonge.Sisi
madiwani tumekubaliana wananchi wapate zaidi ya asilimia 60 ili
kuwasaidia wanyonge,ndicho anachokitaka Mhe. Rais John Pombe Magufuli
kwani hajatoa Makinikia haya ili wachache wanufaike nayo”,alifafanua Ngolomole.
“Sisi
madiwani tunawataka wananchi wasikubali kufanya kazi chini ya SHIREMA
kwani inanyonya wananchi wamejiwekea fedha kwenye makinikia haya na
wamekuwa wakiwatoza wachimbaji wadogo shilingi 200,000/= tena bila risti
ili wapewe usajili SHIREMA. Tunataka wananchi wapewe mamlaka ya
kuchagua viongozi wa kuwasimamia kutoka kwenye vikundi vyao vya
uchimbaji”,alisema Ngolomole.
“Tumezuiwa
kufanya mkutano kwani inaonekana tunaingilia maslahi ya watu
binafsi.Kwenye mkutano tulitaka tuwaeleze wananchi mapendekezo ya
madiwani na kupokea maoni ya wananchi kuhusu makinikia”,alisema.
Ngolomole
alimuomba Rais Magufuli wakati anatoka kwenye mapumziko yake Chato
mkoani Geita apitie Maganzo kukutana na wachimbaji wadogo wa madini ili
kutatua mgogoro huo wa makinikia.
Kwa
upande wake diwani wa kata ya Mwadui Luhumbo Paul Magembe, William
Luhende Jijimya wa kata ya Mondo walisema hawapo tayari kuona wananchi
wananyonywa na hawatarudi nyuma huku wakimuomba Rais Magufuli kuwasaidia
wachimbaji wadogo wa madini wilayani Kishapu.
Nao
wananchi waliozungumza na waandishi wa habari,akiwemo Ramadhani
Amani,Bala Masanja na Hamis Sizya walisema zoezi la kupewa makinikia
lilitolewa bila asilimia hivyo wanashangaa kuona baadhi ya viongozi
wanatumia fursa hiyo kujipatia kipato na kuomba serikali kujali
wanyonge.
Kufuatia
malalamiko yaliyotolewa na wananchi pamoja madiwani kuhusu
SHIREMA,Viongozi wa Chama cha Wachimbaji Madini mkoa wa Shinyanga
(SHIREMA) ambao ni Hamza Tandiko (Mwenyekiti) na Gregory Kibusi (Katibu)
walikataa kuzungumza na waandishi wa habari wakidai kuwa watatoa
taarifa kuhusu Makinikia kwenye kikao chao na vikundi vya wachimbaji
wadogo wa madini Januari 3,2020.
No comments :
Post a Comment