Friday, January 10, 2020

Baraza la wafanyakazi ni ‘bunge’ la taasisi, litumieni vizuri



Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Pontian Kitorobombo akiongea katika mkutano wa baraza la Wafanyakazi la THBUB.
Mgeni rasmi (Mwenyekiti wa THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akifungua mkutano wa baraza la Wafanyakazi wa kumi na nane (18) uliofanyika jijini Dodoma Januari 10, 2020.
Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya akiongea katika Mkutano huo. Kushoto kwake ni Mgeni rasmi, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu.
Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia kwa karibu mkutano huo.
*********************************
Na Mbaraka Kambona,
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wametakiwa kutumia vizuri mikutano ya baraza kujadili kwa hekima na kufanya

maamuzi sahihi kwa maslahi ya watumishi wote ili kuleta tija kazini.

Wito huo ulitolewa na Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (Mgeni rasmi) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, katika mkutano wa kumi na
nane (18) uliofanyika jijini Dodoma Januari 10, 2020.

Wakati akifungua Mkutano huo, Jaji Mwaimu aliwaeleza wajumbe kuwa baraza hilo ni kama bunge la taasisi kwa kuwa linaundwa na wawakilishi wa wafanyakazi waliochaguliwa kidemokrasia.

“Baraza hili ni chombo muhimu kilichoundwa kisheria kwa madhumuni ya kuwashirikisha watumishi katika kujadili na kufanya maamuzi yanayohusu maslahi ya ajira kwa lengo la kuleta tija mahala pa kazi”, alisema Jaji Mwaimu.

Jaji Mwaimu aliendelea kueleza kuwa wajibu wa mabaraza kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi yenye tija.

“Baraza la wafanyakazi wajibu wake ni kuhakikisha kunakuwepo na ushirikiano wa kutosha baina ya watumishi na mwajiri ili kuweza kutekeleza ipasavyo majukumu ya taasisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa”, aliongeza.

Aliendelea kuwataka wajumbe kushiriki kikamilifu katika kujadili utendaji wa kazi wa kila siku ili kuuboresha kwani tija na maslahi lazima viwe na uwiano ili kuwe na matokeo bora ya utendaji kazi unaolenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi wanaowatumikia.

Aidha, Jaji Mwaimu alitoa rai kwa wajumbe hao kuwa majadiliano yao yatawaliwe na hekima, busara, uwazi na maelewano ili uwakilishi wao uwe na maana iliyokusudiwa, na yale yote watakayoyajadili wayapeleke na kuwaeleza watumishi wenzao ili kujenga uelewa
wa pamoja.

No comments :

Post a Comment