
Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo
ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu
waliokutana kujadili namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika
vyuo vya elimu ya juu kilichofanyika jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt.Francis Michael
akitoa mada kwa Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kilichohusu namna ya
kupambana na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu
kilichofanyika jijini Dodoma.

Mkuu wa Uelimishaji kutoka Taasisi
ya Kupambana na Kutokomeza Rushwa TAKUKURU Bw. Asseri Mandari akitoa
mada kuhusu jitihada za Taasisi hiyo katika kupambana na rushwa ya ngono
katika sehemu za kazi na katika Sekta ya elimu hasa elimu ya juu katika
kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna ya kupambana na
vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu.


Baadhi ya Wakuu
wa vyuo vya elimu ya juu wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa
zikitolewa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna
ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika Taasisi na Vyuo vya elimu ya
juu nchini.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
…………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imekemea matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Vyuo vya elimu ya juu hasa vitendo vya rushwa ya ngono.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia
Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu wakati akifungua
kikao kilichowakutanisha Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kilichohusu
namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo ya Vyuo vya elimu ya juu.
Dkt. Jingu
ameongeza kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia limekuwa likishamiri katika
Vyuo vya elimu ya juu kwani imeripotiwa kuwa wahadhiri wengi wamekuwa
wakitumia madaraka yao kuwalazimisha wanafunzi kufanya nao ngono kwa
lengo la kuwafaulisha mitihani.
Amesema kuwa sio
wanafunzi pekee wanaokumbana na vitendo hivyo ila hata wafanyakazi
wanaofanya kazi katika Vyuo vya elimu ya juu wanakubwa na vitendo vya
ukatili wa kijinsia hivyo nguvu ya ziada inahitajika katika kupambana na
vitendo hivyo vyuoni.
“Tumeshuhudia
uwepo wa matukio ya ukatili wa kijinsia katika vyuo vyetu vya elimu ya
juu hasa rushwa za ngono hili sio sawa tunatakiwa kulikemea kwa nguvu
zote” alisema Dkt Jingu.
Dkt. Jingu
amesema kuwa katika kuhakikisha tunapambana na vitendo vya ukatili wa
kijinsia Serikali na Wadau wanatekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa
Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto ili kuhakikisha kuwa
vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia nchini vinatokomezwa kwa asilimia
50 ifikapo mwaka 2021 na 2022.
Aidha Dkt. Jingu
amewataka wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanatoa elimu na maelekezo ili
kujenga uelewa wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa
wanafunzi wa kike kwa kwa ajili ya kuepuka matakwa ya wahadhiri
wanaotumia hila kuendekeza ukatili wa kingono vyuoni.
Pia Dkt. Jingu
amewataka Wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanatekeleza Agizo la Waziri
Ummy Mwalimu la kuanzisha madawati ya jinsia katika vyuo vyao ili
kuwezesha kuondokana na vitendo vya kikatili na kujenga mazingira
yaliyosalama katika vyuo vyetu.
Kwa upande wake Mkuu wa
Uelimishaji kutoka Taasisi ya Kupambana na Kutokomeza Rushwa TAKUKURU
Bw. Asseri Mandari amesema kuwa Taasisi hiyo imejipanga kupamabana na
tatizo hilo kwa kuanzisha Kampeni inayaosema “Vunja Ukimya Ondoa Rushwa
ya Ngono” itakayosaidia kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia
hasa kuzuia rushwa ya ngono.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Jinsia kutoka Chuo
Kikuu cha Dar es salaam Dkt. Lulu Mahai amesema kuwa Vyuo vya elimu ya
juu vinawajibu mkubwa wa kuhakikisha wanatoa elimu kuhsu kupambana na
vitendo vya kikatili kwa wanafunzi wa wafanyakazi na wanaamini baada ya
kikao hiki watarudi na kuanzisha madawati ya jinsia na kamati mbalimbali
zitakazosaidia kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia katika
Taasisi na Vyuo vyote nchini.
No comments :
Post a Comment