Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akisikiliza maelezo kutoka
kwa mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la
Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima (hayupo pichani) walipokutana Jijini
Dodoma ambapo Japan imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika Nyanja
mbalimbali za maendeleo.
Makamu wa Rais wa
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima
akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) Jijini Dodoma ambapo JICA
imeahidi kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo nchini Tanzania.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa tano kushoto) akiwa
katika picha ya pamoja na mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la
Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima (wa tano
kulia), pamoja maafisa wengine waandamizi kutoka JICA, Wizara ya Fedha
na Mipango na Wizara ya Uchukuzi baada ya mazungumzo yaliyofanyika
Jijini Dodoma kati ya pande hizo mbili.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akiteta jambo na
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru nje ya
Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma baada ya kumalizika
kwa mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Makamu wa Rais wa Shirika la
Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) Dkt. Nobuko Kayashima.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akimwongoza
mgeni wake kutoka nje ya Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango (jengo la Treasury Square),
Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA)
Dkt. Nobuko Kayashima, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika Jijini
Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) akiagana na
mgeni wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan
(JICA) Dkt. Nobuko Kayashima (kulia) pamoja na kurugenzi Msaidizi wa
JICA, Bi. Yuriko Doi, nje ya jengo la Treasury Square, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akipeana mkono na mgeni
wake, Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan
(JICA) Dkt. Nobuko Kayashima, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika
Jijini Dodoma ambapo Japan imeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania katika
Nyanja mbalimbali za maendeleo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
*************************************
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha
na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameiomba Serikali ya Japan kupitia
Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) kusaidia
upatikanaji wa fedha kwa
njia ya mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza
miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ikiwemo reli ya
kisasa, nishati na kilimo.
Dkt. Mpango
ametoa maombi hayo Jijini Dodoma, wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Makamu wa Rais wa JICA, Dkt. Nobuko Kayashima, ambapo
wawili hao wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa
miradi inayokusudiwa kufadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika
hilo.
Amesema kuwa hivi
sasa Serikali imeelekeza nguvu na fedha zake za ndani kujenga Reli kwa
kiwango cha Kimataifa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme kwa
njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani (Nyerere Hydral
Power Plant), na kwamba miradi inahitaji fedha nyingi ambazo anaamini
Japan inaweza kusaidia upatikanaji wake.
“Tumeanza
kutekeleza miradi hii kwa kutumia fedha zetu za ndani na tunaiomba
Serikali ya Japan kuzishawishi taasisi zake za fedha kwa kushirikiana na
taasisi nyingine kutupatia mikopo yenye masharti nafuu ili tuweze
kukamilisha miradi hiyo muhimu kwa Taifa” alisema Dkt. Mpango
Alifafanua kuwa
kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza shughuli za kiuchumi na kibiashara
hapa nchini pamoja na nchi jirani ambazo hazijapakana na Bahari huku
nishati ya umeme ikitarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme kwa ajili ya
kuendesha reli hiyo pamoja viwanda.
Aidha, Dkt.
Mpango amemwomba kiongozi huyo wa JICA kusaidia Wizara na Serikali kwa
ujumla kuendeleza rasilimali watu ama nguvu kazi kwa kuwapatia fursa ya
masomo nchini Japan wataalam kutoka Wizara yake na maeneo mengine
serikalini ili kuongeza ubobezi wa wataalam hao katika sekta ya uchumi,
fedha, pamoja na tiba hususan matibabu ya moyo na figo.
“Pia ninaliomba
Shirika lako lisaidie kuboresha miundombinu ya barabara za kuzunguka
Jiji la Dodoma kutokana na mahitaji makubwa baada ya Dodoma kuwa Makao
Makuu ya Nchi, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Nsalato-Dodoma” aliongeza Dkt Mpango
Alisema kuwa
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa-Msalato unahitaji kujengwa njia ya kuruka
na kutua ndege pamoja na ujenzi wa majengo ya abiria.
“ Pia nimewaomba
wenzetu ambao wanauzoefu mkubwa watusaidie katika kilimo cha mpunga na
nimetoa mfano wa Bonde la Ruvu ambalo ni kubwa na lina fursa ya
kuzalisha mchele wa kutosheleza mahitaji ya ndani na nje na tukichagua
eneo moja na kulitumia vizuri tutamaliza mahitaji ya mchele katika Taifa
letu” alisisitiza Dkt. Mpango
Akijibu maombi ya
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makamu huyo wa Rais wa
JICA, Dkt. Nobuko Kayashima, alikubali maombi ya kusaidia kuendeleza
rasilimali watu ambapo kwa kuanzia Shirika hilo limeahidi kutoa nafasi
ya watumishi 15 kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Sekta nyingine
kupata ufadhili wa masomo nchini Japan.
Amesema Serikali
ya Japan kupitia Shirika lake litaendelea kushirikiana na Tanzania
katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi ambapo
miradi mipya inayokusudiwa kufadhiliwa na Shirika lake ni Mradi wa
Upanuzi wa Bandari ya Kigoma, Ujenzi wa Barabara ya Arusha-Holili na
Mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Zanzibar.
Kuhusu
uendelezaji wa kilimo, Dkt. Kayashima ameahidi kuwa Shirika lake
litaendelea kujihusisha na kuendeleza zao la mpunga hapa nchini ili
kuwasaidia wakulima kujikimu kimaisha pamoja na kusaidia nchi
ijitosheleze kwa chakula.
No comments :
Post a Comment