Friday, December 6, 2019

Fahamu Changamoto za Mfuko wa Bima ya Afya


 
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambaye ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda (wa pili kulia), akizindua vifurushi vipya vya bima ya afya hivi karibuni katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam.  Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga (kulia), Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Tryphone Rutazamba (kushoto) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii,  Peter Serukamba.  (Na Mpigapicha Wetu)

Na Christian Gaya

Majira. Ijumaa 06.Desemba.2019, www.majira.co.tz
Afya maana yake ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwepo kwa maradhi. Wote tunajua ya kuwa afya bora ni nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha bora na...
kupunguza umaskini.
Kwa mantiki hii afya inalenga kuwa na ustawi endelevu kwa jamii kwa kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa zilizopo katika kuleta maisha bora.
Utafiti kutoka nchi kumi na tano za Kiafrika ikiwemo Tanzania unaonesha idadi kubwa ya watu wa kipato cha chini wanakimbilia kukopa na kuuza rasilimali zao ili kuweza kwenda pamoja na gharama za matibabu. Hali hii imepelekea familia nyingi kuingia kwenye janga la umasikini zaidi na afya zao kuwa mbaya hasa zaidi huko vijijini.
Pamoja na hayo bado serikali kama ya Tanzania, inatumia kiwango kidogo sana cha kipato kwa kichwa cha mtu kwa matumizi ya afya ukiachilia mbali hifadhi ya jamii ukilinganisha na nchi zilizoendelea. Gharama kubwa hasa ya matibabu mara nyingi anaachiwa mwananchi ambaye hana uwezo wa kubeba mzigo bila msaada wowote kutoka serikalini au jumuiya yeyote.
Mpaka sasa ni idadi ya wanachama na familia zao wapatao milioni nne na laki sita (4, 600,000) ambao ni sawa sawa na asilimia nane ya idadi ya watanzania wapatao milioni 55 ndio wanaonufaika na Mfuko huu waTaifa wa Bima ya Afya nchini Tanzania (NHIF). Kwa maana nyingine ni kwamba kila kati ya watanzania 100 ni watu 8 (nane) tu ndio wenye bima ya afya nchini, hii ni idadi ndogo sana.
Mfuko wa bima ya afya uliundwa kwa malengo ya kuwapa huduma ya matibabu kwa ajili ya watumishi wa umma ndiyo maana wigo wake ni mdogo sana. Na lengo la kuongeza wigo wa kuwafikia watanzania wengi zaidi ambao wako katika sekta binafsi, sekta rasmi na sekta isiyo rasmi ambao kwa kweli hawana fursa yoyote ya kupata bima binafsi .
Mpango wa kujiunga na vifurushi vya bima ya afya vya hiari ni muhimu kwa kundi hili kwa ajili ya kupanua wigo wa uwanachama kwa kuandikisha wananchi waliojiajiri au kuajiriwa katika sekta rasmi na isiyo rasmi mpango huu pia utawezesha wale wote ambao hapo awali hawakuweza kupata huduma ya Mfuko wa bima ya afya kutokana na kutokua na ajira rasmi. Kwa kufanya hivyo itawasaidia kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wote katika maisha yao kama sehemu ya hifadhi ya jamii.
Utaratibu wa madai ya bima ya afya kila siku yanazidi kuwa magumu zaidi. Wakati huo huo mambo mengi ya kitaalamu na yasiyo ya kitalaamu yanalipuka na kuingilia kati, lakini wataalamu wa bima ya afya lazima waje na njia na utaratibu maalum wa kukokotoa madai halali, kufukua na kuonesha madai yasiyo halali kwa haraka zaidi kuliko ilivyozoeleka.
Pamoja na changamoto hizo za kiufundi, taasisi za hifadhi ya jamii kama vile bima ya afya lazima watambue ya kuwa wanashughulika na wateja wao ambao kwa wakati huo wanakuwa wako katika hali tete na ya kuchanganyikiwa.
Na ndiyo wakati wa kuwahurumia na kuhakikisha ya kuwa wanatumia teknolojia au wanakwenda kidigitali kuhakikisha ya kuwa huduma zao zinatolewa haraka na kwa ubora wa hali ya juu zaidi ya mategemeo ya wateja ili kuwajengea amani ndani ya mioyo yao iliyovunjika kwa sababu ya majanga hatarishi kama haya ya kuungua au kuunguliwa. 
Kulingana na utafiti kutoka mitaani inaonesha ya kuwa kuna kuna fedha kidogo ambayo iko nje ya mabenki. Na inaonesha ya kuwa mtu wa kawaida mtaani amekuwa akisema kwa muda mrefu ya kuwa hakuna fedha
Na ikumbukwe ya kuwa kipato cha nchi ni mzunguko wa fedha zidisha kwa spidi ya fedha. Hivyo inaonesha pande zote za fedha na spidi ziko chini. Ni muhimu hapa kujua ya kuwa mzunguko wa fedha mara nyingi inasukumwa au kusababishwa na kazi zinazofanywa za kila siku za kiuchumi labda fedha zifyatuliwe na kuingizwa sokoni kwa watumiaji.
Halafu fedha ni chombo cha kati cha kubadilishana kwenye kazi zetu za kiuchumi kutoka kwa mzalishaji mpaka anayepekewa huduma hiyo.
Utengenezaji wa thamani unaweza kufanikiwa kwa kutoa vifurushi vya bima ya afya kwa bei ya chini kwanza. Lakini ikumbuke ya kuwa thamani maana yake ni kile chochote ambacho mtu yuko tayari kulipa kwa ajili ya bidhaa au huduma yako unayouza.
Thamani ya kitu inaweza kutengenezwa kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kuuzwa kwa bei ya chini hivyo vifurushi vya bidhaa au huduma yako na mambo mengine mengi ya kumvutia mteja.
NHIF hukusanya michango na kulipia huduma za matibabu kwa watoa huduma ambao wamewahudumia wanachama wa NHIF kila mwezi. Kutokana na mfumo huo, kutokuwajibika kwa NHIF na watoa huduma kwa niaba ya Mfuko wa NHIF husababisha changamoto za ubora wa huduma kwa wanachama wa NHIF.
Changamoto kubwa inayojitokeza na kujadiliwa na wadau mbalimbali ni huduma zisizoridhisha zinazotolewa na baadhi ya watoa huduma ambao wameingia mkataba na NHIF kuwahudumia wanachama wake.
Wananchi mara nyingi wamekuwa wakikerwa sana na watoa huduma ambapo hawatoi huduma hizo kulingana na vigezo vilivyowekwa matokeo yake ni kwamba wanakuwa na huduma mbaya na kutoa huduma kinyume cha makubaliano yaliyopo baina yao.  
Na haya mazingira huenda yanasababishwa na NHIF yenyewe na pia hata kwa kutofuatilia ubora wa huduma hizo unaotakiwa kufanywa na Mfuko wa NHIF wenyewe.  
Baadhi ya watoa huduma kwa niaba ya Mfuko wa NHIF wanasema wakati mwingine NHIF yenyewe ndiyo inachelewesha kutowalipa madai yao kwa muda muafaka na hivyo kupelekea kukwamisha utoaji wa huduma zao kwa wanachama wa NHIF na familia zao
Ingawa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga anasema ya kuwa madai ya ucheleweshaji wa kulipa madai kwa baadhi ya watoa huduma hayatokani na kukosa fedha za kulipa bali inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujiridhisha kwa madai hayo. 
“Kuna sababu nyingi za kuchelewesha madai, yapo madai yanakuja na viashiria vya udanganyifu hayo huwezi ukalipa mapema ni lazima uhakikishe umejiridhisha ili ulipe fedha halali na ulinde fedha za wanachama zisitumike isivyo halali,” Konga anakiri.

No comments :

Post a Comment