
Msajili wa Bodi ya Usajili wa
Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa (Kushoto), Mkurugenzi Msaidizi
wa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Imaculata Senje na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara Hamdoun
Masoor wakiwa katika Mkutano wa Wataalamu wa Mipango Miji Nchini
unaoendeleo jijini Dodoma leo tarehe 27 Novemba 2019.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili
wa Wataalamu wa Mipango Miji Profesa Wilbert Kombe (Kushoto), Mkurugenzi
wa Kampuni ya City Plan Vicent Shaidi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam Dkt Dawah Magembe wakiwa katika Mkutano wa
Siku tatu wa Wataalamu wa Mipango Miji unaofanyia jijini Dodoma leo 27
Novemba 2019.

Baadhi ya wajumbe wakiwa katika mkutano wa Wataalamu wa Mipango Miji unaoendelea jijini Dodoma leo 27 Novemba 2019.

Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdoun Mansoor
akiwasilisha mada katika mkutano wa Wataalamu wa Mipango miji
unaoendelea jijini Dodoma leo tarehe 27 Novemba 2019.
………………
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Mwenyekiti wa
Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji Profesa Wilbert Kombe
amesema tofauti kubwa kati ya mipango ya kiuchumi na ile ya maendeleo
ya ardhi ndiyo
chanzo kikubwa cha kutokuwepo miji iliyopangika na kutaka
kuwepo ushirikishwaji ili kuwa na miji iliyopangika.
Profesa Kombe
alisema hayo leo tarehe 27 Novemba 2019 katika mahojiano maalum wakati
wa kikao cha siku tatu cha Wataalamu wa Mipango kinachoendelea jijini
Dodoma.
Alisema, kwa sasa
mipango, sera na utekelezaji kuhusiana na masuala ya mipango miji vipo
lakini tatizo kubwa ni tofauti katika mipango ya kiuchumi na maendeleo
kwenye sekta ya ardhi kwa ujumla.
Mwenyekiti huyo
wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji ambayo iko chini ya
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa,
tatizo lingine linalochangia suala hilo ni uelewa mdogo wa wananchi
kuhusiana na manufaa wanayoweza kuyapata katika ardhi iliyopangwa
‘’Mtu ukipanga
ardhi yako unaongeza thamani hata kabla haijaongezewa huduma nyingine
kama vile maji na umeme ndyo maana kuna tofauti kubwa kati ya anayeuza
ardhi iliyopangwa na yule ambaye haijapangwa’’ alisema Profesa Kombe.
Alihimiza uwepo
wa ushirikiano baina ya Serikali na sekta nyingine katika masuala
mbalimbali yanayohusu upangaji miji ili kuepuka kuwa na maeneo
yasiyopangwa ambayo mwisho wa siku ni kuwa na makazi holela.
Kwa upande wake
Msajili wa Bodi ya Wataalamu wa Mipango Miji Hellen Mtutwa alisema,
Mkutano wa wataalamu wa mipango miji unaoendelea unawakutanisha
wataalaumu wote wa mipango miji kutoka serikalini na sekta binafsi ukiwa
na lengo la kuboresha mipango miji nchini na kubainisha kuwa msisitizo
mkubwa ni ushirikishwaji kwenye mipango ya matumizi ya ardhi.
Kwa mujibu wa
Mtutwa, Ushirikishwaji wa sekta mbalimbali katika mipango miji ya maeneo
mbalimbali nchini siyo tu utarahisisha masuala ya upangaji miji bali
utaepusha hasara kwa wananchi na serikali kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa City Plan Consultants (T) Limited Dkt Juma Mohamed aliiomba
serikali kuipa kipaumbele mipango ya maendeleo ya ardhi kwa kuwa ardhi
ndiyo kila kitu hususan katika masuala yanayohusu shughuli za binadamu.
Dkt Mohameda
alisema, tatizo kubwa kwa wananchi wengi ni kutegemea matokeo ya haraka
kwenye sekta hiyo wakati suala hilo linaweza kuhitaji mipango ya muda
mrefu hasa katika masuala ya Mipango Kabambe.
No comments :
Post a Comment