
Naibu Waziri (Elimu), Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwita Waitara akitoa
hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kazi wa Makatibu wasaidizi wa Tume ya
Utumishi wa Walimu wa Wilaya, Tanzania Bara. Mkutano huo uliofanyika
katika ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo jijini Dodoma,
Novemba 26 na 27, 2019.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa
Walimu, Bibi Winifrida Rutaindurwa akitoa maneno ya kumkaribisha mgeni
rasmi (Naibu Waziri – TAMISEMI, Mhe. Mwita Waitara) katika mkutano wa
kazi wa Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wa Wilaya,
Tanzania Bara.

Baadhi ya Makatibu Wasaidizi wa
Tume ya Utumishi wa Walimu wakiwa wanamkaribisha mgeni rasmi (hayupo
pichani) katika ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo jijini
Dodoma.

Naibu Waziri (Elimu), Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwita Waitara (katikati
mwenye tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya
Tume ya Utumishi wa Walimu pamoja na wageni waalikwa kutoka Chama cha
Walimu Tanzania, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Chuo
cha Serikali za Mitaa, Hombolo katika mkutano wa kazi wa Makatibu
Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kutoka Wilaya za Tanzania Bara.

Baadhi ya Makatibu Wasaidizi wa
Tume ya Utumishi wa Walimu wakiwa katika hali ya utulivu wakati wa
mkutano wa kazi uliofanyika Novemba 26 na 27, jijini Dodoma.
…………………
Katibu
Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutaindurwa
amesema jumla ya walimu 4,046 wa shule za msingi na sekondari
wamefukuzwa kazi kutokana na
makosa mbalimbali yakiwemo utoro kazini,
kukiuka maadili na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi.
Rutaindurwa
ameyasema hayo jana katika mkutano wa siku mbili uliolenga kuwajengea
uwezo Makatibu Wasaidizi wa TSC kutoka Wilaya zote Tanzania Bara
uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, jijini
Dodoma.
Katika
Maelezo ya kumkaribisha Naibu Waziri (Elimu) wa Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Mhe. Mwita Waitara, Rutaindurwa alisema kuwa tangu
TSC ianze kufanya kazi mwezi Julai, 2016 walimu 7,123 walifunguliwa
mashauri ya kinidhamu baada ya kukiuka maadili ya kiutumishi.
“Mheshimiwa
Naibu Waziri katika makosa yaliyotendwa kwa kipindi cha miaka mitatu,
makosa 5,447 yalikuwa ya utoro kazini, makosa 1,290 kukiuka maadili,
makosa 162 uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi na makosa mengine kwa
ujumla wake yalikuwa 224”, alieleza Rutaindurwa
Alifafanua
kuwa TSC imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kiutumishi kwa mujibu wa
Sheria Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu ambapo walimu 4,046
walifukuzwa kazi, walimu 930 walipewa onyo/karipio, walimu 284
walipunguziwa mshahara, walimu 244 walisimamishiwa nyongeza ya
mshahara, walimu 237 walishushwa cheo na walimu 14 walipewa adhabu ya
kufidia hasara.
Alieleza
kuwa walimu wengi walikutwa na makosa ya utoro wakati wa zoezi la
uhakiki wa watumishi kwa kuwa waliondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila
kufuata taratibu na kuruhusiwa na waajiri wao, hivyo walichukuliwa
hatua za kinidhamu.
“Wengi
wa walimu waliotiwa hatiani kwa makosa ya utoro, walikuwa wameenda
masomoni bila kupata ruhusa kutoka kwa waajiri wao na zoezi la uhakiki
wa watumishi lilipofanyia ndipo ikagundulika kuwa ni watoro na mchakato
wa kuwachukulia hatua za nidhamu ukaanza,” alisema.
Akifungua
Mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Naibu
Waziri anayeshughulikia elimu katika ofisi hiyo, Mhe. Mwita Waitara
alieleza kuwa TSC bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha walimu
wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu za kiutumishi ili
wajiepushe na makosa ya kinidhamu.
Aliweka
bayana kuwa Serikali haijivunii kuwafukuza kazi walimu wake
iliyowaajiri yenyewe ikizingatiwa kuwa bado kuna changamoto ya upungufu
wa walimu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa
kweli tunasikitika kuwa idadi ya walimu waliofukuzwa kazi ni kubwa,
lakini ni lazima watumishi wa umma muelewe kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli haina huruma
kabisa na watumishi wazembe wasiozingatia Maadili na Miiko ya kazi yao”,
alisema Mhe. Waitara.
Pamoja
na hayo, Mhe. Waitara alieleza kuwa walimu wamekuwa na kero na
malalamiko mbalimbali yanayosababishwa na kutowajibika kikamilifu kwa
baadhi ya watendaji wa wanaoshughulikia masuala yao.
Alieleza
baadhi ya kero hizo kuwa ni kucheleweshwa kwa malipo ya kusafirisha
mizigo kwa walimu waliostaafu, walimu waliostahili kupandishwa madaraja
kutopandishwa kwa wakati, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kukataa kupitisha barua za walimu wanaoomba kuhama kutoka Wilaya moja
kwenda nyingine na walimu kutotendewa haki katika mashauri ya nidhamu.
Kutokana
na changamoto hizo, Naibu Waziri alipiga marufuku tabia ya baadhi ya
Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ya kuzuia kupitisha barua za
walimu wanaoomba uhamisho na kueleza kuwa wao sio wenye mamlaka ya
kutoa uamuzi wa ombi la mwalimu anayetaka kuhamia wilaya nyingine.
“Ni
marufuku kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzuia
kupitisha barua za walimu wanaoomba uhamisho. Wao wanapaswa kupitisha,
kuweka maoni yao na kuruhusu maombi hayo yaende kwa mhusika
aliyeandikiwa. Mwenye mamlaka ya kukubali au kukataa ombi la uhamisho wa
mwalimu ni Katibu Mkuu, TAMISEMI,” alisisitiza Mhe. Waitara.
Aidha,
Mhe. Naibu Waziri aliiagiza TSC kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali
za Mitaa kuandaa orodha ya walimu waliostahili kupandishwa madaraja
lakini hawakupandishwa na kuiwasilisha TAMISEMI ili taratibu nyingine
ziweze kufanyika.
No comments :
Post a Comment