
Dodoma,
VIONGOZI katika Sekta ya Ushirika
kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zazibar wamekubaliana kuongeza
ushirikiano katika sekta hii ili kuweza kubadilishana uzoefu wa namna
bora ya jinsi ya kusimamia na kuimarisha vyama vya ushirika hapa nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati
wa kikao kati ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume
ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Bara (TCDC), Dkt. Benson Ndiege na
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Zanzibar, Khamis David Simba,
kilichofanyika Jijini Dodoma leo Jumanne, Novemba 27, 2019.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika
Tanzania Zanzibar, Khamis David Simba ambaye ameambatana na Viongozi wa
Taasisi ya fedha ya Ushirika Zanzibar Faraja Union Limited (Financial
Access Reliability by Joint Action – FARAJA) yupo katika ziara Tanzania
Bara kutembelea na kujionea mafanikio yaliyopatikana katika baadhi ya
vyama vya ushirika vinavyofanya vizuri katika mikoa ya Dar Es Salaam,
Dodoma na Iringa.
Akiongea katika kikao hicho,
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya
Ushirika Tanzania Bara (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amewapongeza viongozi
kutoka Zanzibar kwa uamuzi wao wa kufanya ziara ya kujifunza na kupata
uzoefu kutoka Tanzania Bara kwenye vyama vya ushirika vinavyofanya
vizuri ili waweze pamaoja na mambo mengine kuiendesha kwa mafanikio
Taasisi ya FARAJA.

“Vyama vya Ushirika ni taasisi
nzuri na zina manufaa makubwa kwa Wanaushirika, tatizo ni baadhi ya
viongozi wanaoviendesha na kuvisimamia vyama vya ushirika kutokuwa
waaminifu na waadilifu, hivyo lazima viongozi wa Ushirika tuweke mfumo
mzuri wa kusimamia vyama hivi,” amesema Dkt. Ndiege.
Dkt. Ndiege amewataka viongozi wa
ushirika kutoka Zanzibar kujifunza na kujielimisha kutokana na mafanikio
na changamoto watakazojionea kwenye uendeshaji wa vyama vya ushirika
watakavyovitembelea hapa nchini ikiwa ni pamoja na Shirikisho la Vyama
vya Ushirika nchini (TFC) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo
(SCCULT).

Mrajis wa Vyama vya Ushirika
Tanzania Zanzibar, Khamis David Simba, amesema kuwa lengo la ziara yao
kama viongozi wa Serikali wanaosimamia Sekta ya Ushirika Zanzibar na
viongozi wa Taasisi ya FARAJA limeleta matumaini makubwa kutimia kwa
kuwa wameweza kubadilshana mawazo na uzoefu na viongozi wenzao wa
Tanzania Bara kwenye uendeshaji na
usimamizi wa Vyama vya Ushirika.
“Tumejifunza mengi na tumepata
darasa zuri, kwa kubadilishana mawazo na kubaini baadhi ya sababu
zinazotufanya tusiweze kupata mafanikio makubwa katika uendeshaji na
usimamizi wa Vyama vya Ushirika katika maeneo yetu,” amesema Khamis
David Simba, Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania Zanzibar.
FARAJA ni taasisi ya fedha
inayoundwa na Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), Vyama vya
Uzalishaji na Vikundi vya Wajasiliamali vilivyosajiliwa rasmi kwa mujibu
wa Sheria ya Vyama vya Ushirika ya Zanzibar. Taasisi hii inaendeshwa
kwa kufuata misingi na kanuni za ushirika na Inafanya kazi Zanzibar
(Unguja na Pemba).
No comments :
Post a Comment