* Ni baada ya kumtoza mwekezaji sh. milioni 31 za kuendesha vikao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema mtu yoyote anayekwaza wawekezaji nchini atachukuliwa hatua kali,
hivyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amchukulie
hatua Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtwara, Bw. Maisha Selemani
Mtipa baada ya kumtaka mwekezaji alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili ya
gharama za vikao ili
aweze kupatiwa eneo.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa,
Novemba 01, 2019), wakati akifungua Kongamano la Uwekezaji na Maonesho
ya Biashara mkoa wa Mtwara lililofanyika kwenye Viwanja vya Chuo cha
Ualimu Mtwara. “Yoyote anayekwaza uwekezaji nchini kwa kuwasumbua
wawekezaji tutamshughulikia kabla ya kuwasumbua wawekezaji.”
Amesema Bw. Mtipa amemwandikia
barua mwekezaji wa kampuni ya MBR Internation Company Limited akimtaka
alipe sh. milioni 31.6 kwa ajili y a kulipa kamati mbalimbali zikiwemo
sh. milioni 1.95 kwa kamati ya Menejimenti ya Halmashauri.
Waziri Mkuu amesema “fedha
nyingine sh. milioni 2.27 kwa kamati ya kugawa ardhi ya wilaya, sh.
milioni 4.43 kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Fedha,
Utawala na Mipango sh. milioni 5.14 na sh milioni 17.79 Baraza la
madiwani ili wagawane tu, huu ni utaratibu wa wapi? huku ni kufukuza na
kukwaza wawekezaji.”
Waziri Mkuu amesema Serikali
imeshaondoa tozo zaidi ya 150 zilizokuwa zinakwaza wawekezaji kupata
uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo haitaki kusikia mahali
popote panawekwa tozo zenye kuwakwaza wawekezaji. Amesema hatua
zitakazochukuliwa kwa Bw. Mtipa ziwe fundisho kwa halmashauri zote
nchini.
Mapema, Waziri Mkuu
alizungumzia uuzwaji wa korosho na kuagiza kwamba mfumo uliotumika
katika mnada wa kwanza wa uuzwaji wa zao la korosho uliofanyika jana
(Alhamisi, Oktoba 31, 2019) ndio unaopaswa kuendelea, hivyo ameagiza
wahusika wausimamie vizuri ili usiingie dosari.
Alisema Serikali ilibaini
changamoto katika uuzwaji wa mazao mengine ya pamba na kahawa ya uwepo
wa watu ambao wananunua mazao nje ya mfumo kama kangomba, hivyo ni
muhimu wakadhibitiwa ili fedha zote ziende kwa wakulima.
Pia Waziri Mkuu aliagiza
maandalizi yawe yanakwenda pamoja na msimu kama suala la magunia
wasiachiwe watu wa ushirika pekee bali Wakuu wa Mikoa na Wilaya nao
washiriki katika kutatua tatizo hilo ili minada ifanyike kikamilifu.
Pia chama kikuu cha ushirika
pamoja na vyama vya msingi wazuie kuwepo kwa makato ya hovyo ambayo
yalishaondolewa na Serikali ili kuhakikisha mkulima haumizwi kwa
kupunguzwa kwa malipo yake.
Amewataka viongozi hao
wasimamie mtiririko wa fedha kutoka kwa wafanyabiashara kwenda kwa
mkulima na wahakikishe zinaingizwa katika akaunti za wakulima. Pia
sheria ya ununuzi isimamiwe baada ya mnunuzi kupewa zabuni anatakiwa
alipe ndani ya siku nne. “Sheria hii itaondoa watu wa kati na kumwezesha
mkulima kulipwa fedha zake kwa wakati.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa
amesema amesema wanunuzi wote wametakiwa wahakikishe wakulima wanalipwa
kwa wakati. “Bei ya chini katika mnada wa korosho uliofanyika Mtwara
ilikuwa sh. 2,409 na bei ya juu ilikuwa 2,559 na hali inaonesha uhitaji
wa korosho duniani ni mkubwa kutokana na ubora wake.”
Amesema chama cha ushirika cha
TANECU waliingiza sokoni tani 13,000 huku mahitaji yakiwa ni tani
40,000 na chama cha ushirika cha MAMCU walipelela sokoni tani 7,000 na
mahitaji yalikuwa tani 22,000 hivyo wafanyabiashara wengi jana walikosa
korosho.
Akizungumziakuhusu kilimo cha
zao la korosho, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa mkoa wa Mtwara
kuwa wasibweteke kwani mikoa mingine nayo imeanza kulima korosho, hivyo
waweke mikakati mizuri ili zao la korosho liendelee kuwa zao kuu la
biashara kwa mkoa.
Amesema Serikali kwa upande
wake, itaendelea kuweka mazingira rafiki na miundombinu wezeshi kwa
ajili ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza mkoani Mtwara.
“Tusisahau kuwaMkoa wa Mtwara
ni korosho na korosho ndiyo mkoa. Hili linadhihirishwa na usemi wa
wenyeji kuwa korosho ni dhahabu ya kijani. Mtwara ndiyo mzalishaji
mkubwa wa korosho Tanzania, huzalisha zaidi ya asilimia 65 ya korosho
zote nchini.”
Kadhalika, Waziri Mkuu
ametumia fursa hiyo kuwaasa wawekezaji wote kwamba waondoe hofu kuhusu
kuwekeza Mtwara kwa sababu mkoa wa Mtwara wa sasa ni tofauti na Mtwara
ile waliyokuwa wanaisikia zamani, uchumi wake unakuwa.
Waziri Mkuu amesema ushiriki
wao kwenye kongamano hilo unaonesha utayari walionao katika kuiunga
mkono Serikali kwa lengo la kuwaletea maendeleo na kujenga Tanzania ya
Uchumi wa Viwanda ambayo wote wanaitamani.
Kongamano hili na mengine
yaliyofanyika kwenye mikoa mbalimbali ni utekelezaji wa agizo la Waziri
Mkuu alilolitoa wakati anafungua Kongamano la tatu la uwezeshaji
wananchi kiuchumi jijini Dodoma Juni 18, 2018, ambapo aliagiza mikoa
yote kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa.
“Niendelee kusisitiza tena kwa mikoa ambayo bado haijatekeleza agizo hili la kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji ifanye hivyo mapema.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amesema licha ya Serikali kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miradi ya
kijamii katika Mkoa wa Mtwara, pia imewekeza kwenye miradi mikubwa ya
kimkakati ambayo inachochea kukua kwa uchumi kwa haraka.
Waziri Mkuu ameitaja miradi
hiyo ni pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege na bandari ya Mtwara;
ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mtwara hadi Nanyumbu mpakani na
Msumbiji; ufufuaji na ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho.
Miradi mingine ni ujenzi wa
reli kutoka Mtwara hadi Songea kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe
kutoka Mchuchuma na chuma kutoka Liganga na kuongeza uzalishaji wa umeme
kwa kutumia gesi asilia na vyanzo vingine.
Ufunguzi huo umehudhuriwa
na Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki,
Waziri wa Kilimo Josephat Hasunga, Waziri wa Viwanda na Biashara,
Innocent Bashungwa,Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Christina Mndeme na watendaji wengine wa Serikali.
No comments :
Post a Comment